Home / Habari Za Kitaifa / Uteuzi wa Vita Kawawa watenguliwa

Uteuzi wa Vita Kawawa watenguliwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, kuwakamata viongozi wanne wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku (WETCU) pamoja na kufunga ofisi za chama hicho hadi uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za chama hicho utakapokamilika.

Pia amevunja Bodi ya WETCU pamoja na Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) kwa sababu ya kushindwa kusimamia zao hilo pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo katika kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Isike Mwanakiyungi mkoani Tabora, ambako alisema Rais John Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa TTB, Vita Kawawa na Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo, Wilfred Mushi.

Viongozi wa WETCU ambao Waziri Mkuu ameagiza wakamatwe ni Mwenyekiti Mkandara Mkandara, Makamu Mwenyekiti Msafiri Kassim, Mkaguzi wa Ndani na Mhasibu Mkuu.

Pia amewasimamisha kazi watumishi wa kitengo cha uhasibu wa chama hicho hadi uchunguzi utakapokamilika.

“Kuanzia sasa watumishi wote wa kitengo cha uhasibu pamoja menejimenti, nimewasimamisha kazi pamoja na Mrajisi wa Mkoa wa Tabora, Deogratius Rugangila. Kamanda hakikisha ofisi hazifunguliwi kuanzia sasa hadi hapo timu ya ukaguzi itakapokamilisha kazi yake,” alisisitiza.

Waziri Mkuu alisema kwa muda mrefu wakulima wameteseka na zao hilo kukosa tija kwa sababu ya usimamizi mbovu wa viongozi wa ushirika na Bodi ya Tumbaku Tanzania, jambo ambalo serikali haiwezi kulivumilia.

Alisema, “Hatuwezi kuwa na ushirika ambao hauwasaidii wanachama. WETCU walipokea shilingi bilioni kumi na tano ambazo walizikatia risiti na hazijaonekana. Pia waliwalipa wazabuni shilingi bilioni kumi ambazo hawajazikatia risiti.”

“Wakati wanachama ambao ni wakulima wakiendelea kuteseka, WETCU walinunua gari la shilingi milioni mia mbili sitini na tisa kinyume cha maelekezo ya Mkutano Mkuu wa wadau ambao ulipitisha zitumike shilingi milioni orobaini tu,” aliongeza.

Alisema chama hicho kimesababisha kupungua kwa uzalishaji kwa kiasi kikubwa kutokana na kuwa na menejimemti mbovu, jambo ambalo limechangia wakulima wa tumbaku kukosa tija.

Alisema WETCU imekithiri kwa matumizi mabaya ya fedha, ambapo alitolea mfano suala la ukarabati wa ofisi tatu ikiwemo ya makao makuu, ambayo ilipangwa ikarabatiwe kwa Sh milioni 33 wakatumia Sh milioni 170 na ofisi za Tabora na Urambo zilipangiwa Sh milioni tano kila moja na hazikukarabatiwa.

Pia Waziri Mkuu amepiga marufuku ununuzi wa mbolea kutoka nje ya nchi wakati ikiwa inazalishwa nchini.

Aidha, amepiga marufuku matumizi ya dola ya Marekani katika sekta ya tumbaku na badala yake zitumike fedha ya Tanzania kwa sababu kitendo hicho kimekuwa kiwanyonya wakulima.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, wakuu wa wilaya zote za mkoa huo pamoja na maofisa kilimo na ushirika, kuhakikisha wanasimamia vizuri zao hili ili liweze kuwa na tija kwa wakulima na Taifa kwa ujumla.

Pia aliwaagiza maofisa kilimo waende vijijini na kuwatambua wakulima wa tumbaku katika kila kijiji na kuwasajili. “Kuanzia leo maofisa ushirika wabadilishe mienendo ya kazi nataka wasimamie zao la tumbaku kwa umakini zaidi,” aliagiza.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *