Home / Habari Za Kitaifa / Maboresho sekta afya yashindwa kuzuia kasi matumizi tiba asilia

Maboresho sekta afya yashindwa kuzuia kasi matumizi tiba asilia

PAMOJA na maboresho makubwa yanayofanywa na wadau mbalimbali katika uboreshaji wa miundombinu na utoaji huduma katika sekta ya afya bado wananchi wengi wa Mkoa wa Kigoma wameendelea kwenda kupata huduma kwa waganga wa jadi na tiba asilia badala ya kutumia huduma za hospitali.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga wakati akizungumza katika kijiji cha Kalinzi Wilaya ya Kigoma wakati akizindua nyumba za watumishi kwenye sekta ya afya.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa hali hiyo imeendelea kuleta changamoto katika kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu, malaria na Ukimwi mkoani humo.

Alisema kuwa kwa sasa kumekuwa na uboreshaji mkubwa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali mkoani humo na hivyo hakuna budi wananchi wa mkoa huo kutumia hospitali rasmi za serikali na kuachaa na tiba asilia.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa wakati mwingine wananchi wanakuwa wanaugua kifua kikuu lakini watu wengi wamekuwa wakihusianisha magonjwa hayo na imani za kishirikina na kuonya kwamba wengi wanaotumia tiba asilia wamekuwa wakipata madhara zaidi na vifo kwani magonjwa yanayowasumbua ikiwemo kifua kikuu, malaria na Ukimwi ambayo yana tiba zake hospitalini.

Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Benjamin Mkapa, Dk Hellen Sonkoro alisema kuwa jumla ya nyumba 30 zenye thamani ya Sh bilioni 1.7 zimejengwa katika Wilaya za Halmashauri ya Kigoma, Kasulu na Kibondo ili kutoa unafuu wa upatikanaji wa nyumba za kuishi kwa watumishi.

Senkoro alisema kuwa kumekuwa na tatizo kubwa la watumishi katika sekta ya afya na hasa madaktari kuishi kwenye maeneo yao ya kazi hasa vijijini kwa madai ya uhaba wa nyumba za kuishi watumishi na kwamba mpango huo unalenga kusaidia kukabiliana na changamoto hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Wakurugenzi wa Halmashauri ambazo zimekabidhiwa msaada huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Kigoma, Hanji Godigodi alisema kuwa kukabidhiwa kwa nyumba hizo kwao kutasaidia kukabiliana na changamoto kubwa ya watumishi kuishi kwenye maeneo yao ya kazi hasa vijijini ambako ni mbali na vituo vya afya na hospitali za wilaya.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *