Home / Habari Za Kitaifa / Mahakama Kuu yatengua hukumu dhidi ya Lijualikali

Mahakama Kuu yatengua hukumu dhidi ya Lijualikali

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemuachia huru Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali (Chadema) baada ya kutengua hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro ya kifungo cha miezi sita jela.

Lijualikali ambaye amesota rumande kwa miezi mitatu tangu alipohukumiwa Januari 11, mwaka huu, mahakama hiyo pia imetengua kifungo cha nje cha dereva wake, Stephano Alphonce maarufu kama ‘Ngata.

Hatua hiyo imetokana na rufaa iliyokatwa mwanzoni mwa Machi mwaka huu chini ya hati ya dharura ambayo iliwasilishwa na jopo la mawakili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiongozwa na Tundu Lissu.

Uamuzi wa kutengua hukumu hiyo, ulitolewa mahakamani hapo na Jaji Ama-Isario Munisi, huku upande wa serikali ukiwakilishwa na Wakili Faraja Nchimbi.

Katika rufaa hiyo, mrufani kupitia Wakili wake Lissu aliwasilisha hoja saba ikiwemo ya mapungufu yaliyopo katika hati ya mashitaka yaliyokuwa yakimkabili Lijualikali na kwamba Hakimu aliyemhukumu alitumia hoja za upande mmoja.

Akisoma uamuzi huo, Jaji Munisi alisema licha ya warufani kuwasilisha hoja hizo, amekubaliana na hoja moja ya mapungufu ya hati ya mashitaka ambayo itasababisha hoja nyingine zikose nguvu.

Alisema udhaifu wa hati hiyo inatokana na maelezo aliyosema mshtakiwa yalikuwa tofauti na kifungu cha sheria kilichotumika kumshtaki.

Inadaiwa kuwa hakimu aliyemhukumu alimtia hatiani Lijualikali kwa kufanya fujo, alitumia kifungu cha sheria ambacho kilitofautiana na maelezo ya kosa lililomkabili mshtakiwa huyo.

Jaji Munisi alisema anakubaliana na hoja hiyo ya udhaifu wa hati ya mashtaka, hivyo ametengua hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kilombero na mshtakiwa anatakiwa kuwa huru.

Katika hoja nyingine ambazo ziliwasilisha na mrufani, zilibainisha kuwa Lijualikali alikuwa ni mjumbe halali wa kikao ambacho inadaiwa alisababisha vurugu.

Pia hakimu aliyemhukumu alitumia hoja za upande mmoja, jambo ambalo halipo kisheria.

Januari 11, mwaka huu Mahakama ya Wilaya ya Kilombero ilimhukumu kifungo cha miezi sita jela Lijualikali (Chadema) na dereva wake, Alphonce baada ya kupatikana na hatia ya kufanya vurugu kipindi cha uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo mwaka jana.

Katika kesi ya msingi namba 62 ya mwaka 2016, inadaiwa kwamba washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na kosa la kufanya fujo kwa nia ya kuvunja amani.

Inadaiwa Machi 1, mwaka jana majira ya saa nne asubuhi maeneo ya Kibaoni ulipo ukumbi wa Halmashauri ya Kilombero kwa makusudi na isivyo halali walifanya fujo katika maeneo hayo ambapo kulikuwa na uchaguzi wa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *