Home / Habari Za Kitaifa / Ndalichako: Waajiri msikataze watumishi kwenda kusoma

Ndalichako: Waajiri msikataze watumishi kwenda kusoma

BENKI ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeipa Taasisi ya Chuo Kikuu cha Sayansi cha Nelson Mandela cha Arusha Sh bilioni 8.2 kwa ajili ya kufadhili wanafunzi wanaokwenda katika chuo hicho kupata ujuzi na elimu mbalimbali za utafiti kwenye chuo hicho.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako wakati akizindua mradi wa kukijengea uwezo chuo hicho, uliofadhiliwa na AfDB.

Profesa Ndalichako alisema fedha hizo zimetolewa na AfDB kama ruzuku kwa serikali zenye lengo la kutaka wafanyakazi wote kote nchini wenye sifa kujiunga na chuo hicho kupata elimu na ujuzi kwa faida ya Watanzania.

Alieleza kuwa ufadhili huo wenye vifaa vya kisasa vya utafiti na maabara unapaswa kutumiwa na wafanyakazi walioajiriwa na wasioajiriwa wenye sifa za kujiunga na chuo hicho, ambao wanapaswa kutumia fedha hizo kwa maslahi yao na nchi kwa ujumla.

Alisema wafanyakazi 96 waliopata ufadhili wa masomo katika chuo hicho ambao 66 ni wa ngazi ya Uzamili na 30 ni wa Uzamivu, ni wachache, hivyo kuwataka waajiri nchini kuwaruhusu wafanyakazi kujiunga na chuo hicho kupata elimu zaidi bila ya kipingamizi.

Alisema nchi inahitaji wataalamu wa kutosha katika fani mbalimbali kwa kuwa waliopo hawatoshi.

Alisema itashangaza kuona mwajiri anamkataza mfanyakazi kujiunga na chuo hicho kupata elimu iliyofadhiliwa kwa asilimia mia moja na wafadhili.

Alisema na kutoa onyo kwa waajiri kuacha kuwakataza wafanyakazi kwenda kusoma pindi wanapopata nafasi ya kujiunga na chuo hicho.

Alisema ikiwa watakuwepo watakaoendelea kuzuia wafanyakazi wao wasiende kusoma chuoni hapo, atawachukulia hatua.

“Tunakwenda katika uchumi wa viwanda na tunahitaji wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali na kama kutakuwa na mtu anakwamisha jitihada hizo huyo hatufai katika serikali hii ya awamu ya tano,” alieleza.

Ofisa Mfawidhi wa AfDB nchini, Hamis Simba, alisema benki hiyo iko katika hatua ya kwanza ya kufadhili kiasi hicho cha fedha kwa muda wa miaka mitano kuanzia mwaka huu na kwamba iwapo fedha hizo zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, haitasita kutoa kiasi kingine cha fedha kwa awamu ya pili ya mradi.

Simba alisema lengo la AfDB ni kutaka Afrika kuwa na wataalamu wengi zaidi katika fani mbalimbali ili kuinua uchumi wa Afrika na ndio maana inatoa misaada katika vyuo mbalimbali Afrika kwa ajili ya kuwafadhili wafanyakazi na wanafunzi kusomea masomo ya kitafiti.

Alisema mradi huo unajengea uwezo taasisi hiyo kwa kulenga kuongeza uwezo katika nyanja za ufundishaji, utafiti, upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na udhamini wa masomo.

Mwenyekiti wa Bodi ya chuo hicho, Profesa David Mwakyusa alisema fedha hizo zimekuja katika wakati muafaka kwani chuo hicho kilikuwa kinakabiliwa na uhaba wa wanafunzi kwa sababu mwaka 2014 kilikuwa na wanafunzi wasiozidi 10.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *