Home / Habari Za Kitaifa / Bunge laagiza tathmini matunzo faru Fausta

Bunge laagiza tathmini matunzo faru Fausta

BUNGE limeitaka serikali kutathimini gharama za matunzo zinazotumika kumtunza faru Fausta aliyepo katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro baada ya kubainika kuwa matunzo hayo yanagharimu Sh milioni 768 kwa mwaka.

Spika Ndugai aliiomba serikali kufanya tathimini hiyo wakati akijibu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakanjoka (Chadema) aliyetaka kujua msimamo wa Spika kuhusu ukubwa wa gharama za malezi ya faru huyo.

Mwakanjoka aliomba mwongozo huo baada ya awali Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe kueleza sababu za msingi za serikali kuendelea kumtunza faru huyo pamoja na matunzo hayo kugharimu fedha nyingi.

Profesa Maghembe alilazimika kutoa majibu hayo katika swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema) aliyehoji sababu za serikali kutumia Sh milioni 64 kila mwezi kumtunza faru Fausta.

Waziri akijibu alisema; “Ni kweli yupo faru Fausta katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro. Faru huyu amezeeka kweli na amekuwa akisumbuliwa na maradhi mbalimbali.”

“Hata hivyo, tumekuwa tunalazimika kuendelea kumtunza kwa vile zipo tafiti mbalimbali zinaendelea kufanywa kwake ili kusaidia katika kujua namna sahihi za maisha ya wanyama hawa ambao wamekuwa adimu sana duniani.

“Ni muhimu kupata takwimu za wanyama hawa ili tujue namna nzuri ya kuwatunza, ingawa ni kweli kuwa matunzo ya faru Fausta yana gharama kubwa ambazo kimsingi ndio gharama zenyewe za uhifadhi,” alifafanua Profesa Maghembe.

Alisema serikali inafanya hivyo kwa nia njema kwa vile gharama hizo zina thamani halisi za maisha ya wanyama hao adimu duniani.

Majibu hayo ndiyo yaliyomfanya Mwakanjoka kuomba mwongozo huo wa Spika ili kujua kama zipo sababu kwa serikali kuendelea kutumia kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa faru huyo mzee badala ya kuzielekeza kwenye matatizo ya wananchi.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *