Home / Habari Za Kitaifa / Mwanza tayari kwa uwekezaji

Mwanza tayari kwa uwekezaji

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amewahakikishia wote wanaotaka kuwekeza Mwanza mjini na wilaya zake, kuja kwa wingi na kwamba mkoa umejiandaa kutoa ardhi kwa yeyote aliye tayari kwa ajili hiyo.

Aidha amesema ndani ya mwezi mmoja taratibu zote za uwekezaji kwa maana ya nyaraka muhimu zitakuwa zimekamilika na mwekezaji kuanza shughuli zake.

Mongella alisema hayo jijni hapa wakati alipokuwa akifungua Jukwaa la Biashara Mkoani Mwanza lililoandaliwa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayochapisha magazeti ya Daily News, HabariLeo na SpotiLeo kwa kushirikiana na ofisi yake.

Aliyataja maeneo ambayo yako tayari kwa ajili ya uwekezaji mkoani humo ni pamoja na eneo la Nyamhongolo ambako kuna ekari 189.3 na eneo lililo katika Kata ya Lwanima lenye ekari 1,340 ambazo ziko tayari kwa ajili ya uwekezaji.

Halikadhalika alisema kuna eneo pia la ekari kadhaa linalomilikiwa na Kampuni Hodhi ya Raslimali za Reli (Rahaco) linaloweza pia kutumiwa na wawekezaji.

Halikadhalika alisema tayari mkoa wake uko katika mikakati ya kuendeleza viwanda ambapo ndani ya miezi miwili viwanda viwili vinatazamiwa kuanza kazi kikiwemo kiwanda kingine cha soda.

“Hatuko tena kwenye mikakati. Tumeshaanza na hivyo tunataka muitazame Mwanza kwa jicho tofauti,” alisema Mongella na kuongeza kuwa katika kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji na kuondoa changamoto zinazowakabili, mkoa umeunda kitengo maalumu cha kushughulikia masuala ya uwekezaji na biashara.

“Tunataka Mwekezaji kama ana mgogoro na TRA, kitengo hiki kiende naye moja kwa moja TRA ili wamsaidie, wakajadiliane naye”, alisema huku akifafanua kwamba kabla ya kuundwa kwa kitengo hicho kulikuwa na malalamiko mbalimbali ya wawekezaji mkoani mwake.

“Bila shaka sisi Mwanza ndio wa kwanza kuanzisha kitengo cha uwekezaji ingawa hakiko katika taratibu zetu za kiserikali. Kinajumuisha wahandisi, wachumi, watengeneza mipango na kadhalika,” alisema.

Mongella alielezea matumaini yake ya makubwa ya uchumi wa Mwanza kupanda kutokana na mingo ya mkoa iliyopo pamoja na ya kiserikali hususani pale ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge) utakapokamilika.

Kwa upande wake, Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Serikali (TSN), Dk Jim Yonazi alisema Jukwaa la Biashara ni jambo kubwa, lenye kuleta faida nyingi kiuchumi, sio tu kwa mkoa wa Mwanza bali kwa nchi nzima.

Alisema TSN imeamua kuitisha jukwaa hilo la kiuchumi jijini Mwanza kwa kuwa mkoa wa Mwanza una utayari mkubwa katika kutumia fursa za kiuchumi zilizopo kwa manufaa ya mkoa wenyewe na taifa kwa ujumla.

“Tuko hapa kwa sababu sisi ni wapenda maendeleo na TSN tumeamua kuchagiza maendeleo ya Mwanza,” alisema.

Akiwasilisha salamu za Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Dk Hassan Abbas alisema Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amepongeza kuwepo kwa jukwaa hilo muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Jukwaa la Biashara ambalo jana lilihudhuriwa na watu zaidi 300 liliwashirikisha pia wadau wa maendeleo ambao pia wamelidhamini.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *