Home / Habari Za Kitaifa / Serikali yapania kuanzisha kampuni gesi ya heliumu

Serikali yapania kuanzisha kampuni gesi ya heliumu

TANZANIA ina mpango wa kuanzisha kampuni ya serikali itakayoshughulika na gesi ya heliumu kukabiliana na kampuni za ndani na za kimataifa zinazoshughulika na gesi hiyo huku ikitaka Shirika la Taifa ya Maendeleo ya Petroli (TPDC) kutojishughulisha na biashara ya gesi hiyo.

Karibu mwaka mmoja sasa baada ya watafiti kugundua akiba ya gesi hiyo katika Bonde la Ufa ambayo upatikanaji wake ni nadra, serikali imetangaza kuwa itaanzisha kampuni ya kitaifa ya gesi ya heliumu itakayokuwa na jukumu la kutoa leseni, utafiti, uchimbaji na uzalishaji wa gesi hiyo.

Huku kukiwa na upungufu mkubwa wa upatikanaji wa gesi hiyo duniani, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema wakati akizungumza kwenye Mkutano wa Mwaka wa Wafanyakazi wa Wizara yake, “Tunahitaji Kampuni Maalumu ili kusimamia biashara hiyo yote.” Amezuia TPDC kujihusisha na biashara ya gesi ya heliumu kwa kile alichoita “kutokuwa na utaalamu na uwezo” wa kujiingiza katika biashara ya gesi hiyo.

“TPDC haijakamilisha majukumu yake ya utafutaji mafuta na gesi ya asili na uzalishaji… haina utaalamu na gesi ya helium,” alisema na kufafanua kwamba kampuni hiyo ya kitaifa ya mafuta iendelee kujikita na jukumu lake la msingi la kutafiti upatikanaji wa mafuta. TPDC ilianzishwa kwa Sheria ya Kampuni ya Umma Namba 17 ya mwaka 1969, ni kampuni ya kitaifa ya serikali inajishughulisha na utoaji leseni ya maendeleo ya nishati nchini.

Timu ya utafiti imekadiria kwamba sehemu moja tu ya akiba hiyo hapa nchini, inaweza kuwa na futi za ujazo wa bilioni 54, ambacho ni kiasi cha kutosha cha kujaza zaidi ya vipimo vya skana za tiba (MRI) milioni 1.2. Ugunduzi huo kwa ujazo mmoja ni sawa na mara mbili ya kiasi cha gesi ya heliumu nchini Marekani kinachokadiriwa kuwa sawa na futi za ujazo bilioni 24.2.

“TPDC inatakiwa kushughulika na mafuta na siyo helium,” alisisitiza Waziri. Ofisa mmoja wa Wizara alisema TPDC ilipanga kuipatia leseni kampuni ya Mafuta ya Heritage Tanzania kuingia katika biashara ya gesi ya helium baada ya Kampuni ya Helium One kusimamishwa kufanya utafiti na TPDC. Profesa Muhongo alikuwa na wasiwasi kwamba iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa ili kukabiliana na tatizo hilo, nchi haitanufaika na akiba kubwa ya gesi hiyo iliyo nayo.

Aliwaelekeza Kamishna wa Madini na Katibu Mkuu anayehusika na madini kukamilisha utaratibu na Kampuni ya Helium One kuhusu uchimbaji na uzalishaji wa gesi hiyo huku ikisubiriwa kuanzishwa kwa Wakala wa Taifa wa Gesi ya Heliumu.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *