Home / Habari Za Kitaifa / Mapingamizi ya kodi ya bil 858/- yaifikia TRA

Mapingamizi ya kodi ya bil 858/- yaifikia TRA

KATIKA Mwaka wa Fedha 2015/16, jumla ya pingamizi 140 za kodi kutoka kwa walipa kodi zenye thamani ya shilingi bilioni 858.2 ziliwasilishwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zikipinga kiasi cha kodi kilichokokotolewa na kufanyiwa tathmini na Kamishna wa Kodi, imebainika.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuwapo kwa pingamizi nyingi za kodi ambazo hazishughulikiwi kwa wakati na kutolewa uamuzi, kunatokana na upungufu wa wataalamu na rasilimali watu katika TRA kushughulikia mapingamizi ya kodi ikilinganishwa na idadi ya mapingamizi yaliyoletwa na walipa kodi.

Kadhalika, ukaguzi wa pingamizi za kodi zilizowasilishwa na walipa kodi kwa mwaka wa fedha wa ukaguzi ulibaini kuwa, Mamlaka ya Mapato ilishindwa kukusanya shilingi bilioni 13.7 ambazo ni fedha za amana zinazotokana na malipo yaliyotakiwa kulipwa, ikiwa ni chochote kitakachokuwa kikubwa kati ya moja ya tatu ya kiasi cha kodi kilichofanyiwa tathmini na kutakiwa kulipwa na walipa kodi au kiasi cha kodi ambacho hakipo katika pingamizi, kinyume cha Kifungu Na. 51 (5) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015.

Ripoti hiyo ya CAG imesema kutokukusanywa kwa fedha hizi kunachangia kwa kiasi kikubwa walipa kodi kutumia mwanya huu kukwepa kulipa kodi. “Hii inatokana na kutokuwepo kwa ufanisi katika kushughulikia mifumo ya pingamizi za kodi, hivyo kusababisha mapato ya serikali kutokukusanywa kwa wakati. Hii inasababisha kutokufikiwa kwa makadirio ya makusanyo ya mapato ya serikali, hivyo kuathiri utekelezaji wa mipango ya serikali,” alieleza CAG.

Aliongeza kuwa ukaguzi wake pia wa nyaraka mbalimbali za mapingamizi ya kodi katika mikoa saba, umegundua kuwa maombi ya mapingamizi ya kodi yenye thamani ya shilingi 15,083,331,726 yalikataliwa na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato kutokana na kutokuwepo kwa sababu za msingi zinazoelezea mapingamizi hayo kinyume na Kifungu Na. 51 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015.

“Mapitio zaidi ya ripoti za mapingamizi ya kodi za kila mwezi yameonesha kuwa mapingamizi ya kodi yenye thamani ya shilingi bilioni 1.37 yalitolewa maamuzi na fedha hii ilitakiwa kukusanywa, lakini haikukusanywa na mameneja wa kodi wa mikoa husika na hivyo kufanya jumla ya shilingi bilioni 16.4 kutokukusanywa,” aliongeza.

CAG aliishauri serikali kuongeza jitihada za kushughulikia kesi za mapingamizi ya kodi yaliyoletwa na walipa kodi kwa wakati ili kutoa maamuzi sahihi juu ya kodi sahihi inayopaswa kulipwa kwa wakati. “Hili linawezekana kwa kuongeza idadi ya watumishi wenye utaalamu na ujuzi pamoja na kuwaongezea mafunzo ya kimbinu watumishi wote walio katika Kitengo cha Huduma za Kiufundi,” alisema.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

wakulima tanzania

Wakulima Tanzania watafuta masuluhisho kwa changamoto zao

Wakulima nchini Tanzania wameonya kuwa huenda nchi hiyo ikaingia kwenye baa la njaa kutokana na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *