Home / Habari Za Kitaifa / Waliokula mil 359/- za barabara zawakwama

Waliokula mil 359/- za barabara zawakwama

BODI ya Mfuko wa Barabara imeziamuru halmashauri saba nchini zilizotumia zaidi ya Sh milioni 359.5 zilizotolewa kwa ajili ya kujengea barabara, lakini zikazitumia kununua madawati na kujengea maabara kuzirudisha mara moja katika mfuko huo.

Halmashauri hizo ni Karagwe Sh milioni 55.5, Kyerwa Sh milioni 36.8, Ushetu Sh milioni 15.7, Masasi Mji Sh milioni 31.3, Nanyumbu Sh milioni 110.7, Kilolo Sh milioni 102.3 na Songea ya Mji Sh milioni 7.3, na zinatakiwa kurudishwa fedha hizo kabla ya Oktoba 30, mwaka huu. Hayo yalisemwa mjini Dodoma jana na Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), Joseph Haule wakati akiwasilisha taarifa ya ukaguzi wa kiufundi na fedha kwa kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja kwa mwaka wa fedha 2014/15 na 2015/16.

“Kwa zile halmashauri za wilaya zilizotumia fedha za Mfuko wa Barabara kwa matumizi mengine kama vile kutengenezea madawati na ujenzi wa maabara, wakaguzi wa halmashauri husika wahakikishe zinarudisha haraka katika akaunti ya Mfuko wa Barabara ya Dharura,” alisema Haule na kufafanua kuwa halmashauri hizo zilikiuka Sheria ya Fedha ya Mwaka 2001, Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 na Sheria ya Tozo za Barabara na Mafuta na Kanuni zake.

Pia kuna halmashauri ambazo zililipia jumla ya Sh milioni 87.1 kwenye kazi hewa ambazo hazijafanyika ambazo ni pamoja na Mtwara ambayo ililipa Sh milioni 46.2, Tanga Mjini Sh milioni 12.1, Monduli Sh milioni 6.6, na Moshi Sh milioni 12.2 nazo zinatakiwa kulipa fedha hizo. Halmashauri ya Gairo ambayo miradi mingi haijatekelezwa kadiri ya mikataba ya makubaliano, ilipewa nafasi ya kufika mbele ya Bodi ya Mfuko, lakini ilichelewa kufika.

“Halmashauri ya Kalambo, mkandarasi wake aliidhinisha malipo ya Sh milioni 15.4 ya kupima kifusi ambacho hakijashindiliwa kinyume cha mkataba unaotaka kuidhinisha malipo kifusi kilichoshindiliwa,” alisema na kubainisha kuwa Halmashauri ya Kakonko ilihamisha Sh milioni 13.7 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya mradi wa matengenezo ya barabara na kutekelezea mradi mwingine, kinyume cha mkataba wa makubaliano. “Halmashauri ya Kondoa ilipewa zaidi ya Sh milioni 60 kwa ajili ya kujenga maeneo korofi na ikajenga chini ya kiwango na hivyo kuisababishia hasara kubwa serikali,” alisema.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

wakulima tanzania

Wakulima Tanzania watafuta masuluhisho kwa changamoto zao

Wakulima nchini Tanzania wameonya kuwa huenda nchi hiyo ikaingia kwenye baa la njaa kutokana na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *