Home / Habari Za Kitaifa / GEREZA LA KEKONFAINI MILIONI 30/-

GEREZA LA KEKONFAINI MILIONI 30/-

NAIBU Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira amezitoza faini ya Sh milioni 30 Gereza la Keko kwa kosa la kutiririsha majitaka yanayozalishwa gerezani hapo na kuhatarisha maisha ya binadamu na viumbe hai wengine.

Akiwa katika ziara nyingine ya ukaguzi wa mazingira jijini Dar es Salaam, Mpina alilitaka Baraza hilo kutoa agizo kwa Mkuu wa Gereza kujenga miundombinu ya majitaka ambayo ni rafiki kwa mazingira sambamba na kulipa faini hiyo kwa muda uliotajwa.

“Taasisi za Serikali zinapaswa kuwa mfano kwa kutii sheria za nchi hususan Sheria ya Mazingira nimeshasema mara nyingi na ninarudia hapa tena taasisi za serikali haziruhusiwi kuchafua mazingira kwa namna yoyote ile kwa mujibu wa sheria. “ anasema Mpina.

Aidha ameitaka Manispaa ya Temeke kusimamia kwa makini masuala ya usafi wa mazingira katika maeneo ya Keko na kuwachukulia hatua wananchi wote wanaotiririsha majitaka katika mifereji ya maji ya mvua.

Akitoa ufafanuzi wa adhabu hiyo Mwanasheria wa Baraza la Mazingira, Suguta Heche alisema kuwa taasisi za serikali na mashirika ya umma yana wajibu wa kufuata sheria za nchi hususani sheria za mazingira na ukiukwaji wa sheria hizo utaambatana na adhabu kama zinatolewa kwa mashirika na kampuni binafsi.

Awali Naibu Waziri Mpina alitembelea kiwanda cha kutengeneza dawa cha Keko Pharmaceutical Limited na kutoridhishwa na uharibifu wa mazingira unaofanywa na kiwanda hicho wa kutiririsha majitaka katika makazi bila kutibiwa pamoja na kutokuwa na kibali cha utiririshaji, hivyo kuwatoza faini ya Sh milioni 20 inayopaswa kulipwa ndani ya wiki mbili.

Mpina alielekeza usafi wa mazingira kufanyika katika mifereji ya maji ya mvua na kuwaasa wakazi wa maeneo jirani kutokutupa takataka katika maeneo hayo.

Kwa upande wake Selemani Ndugwana, Meneja udhibiti na Ubora wa kiwanda hicho cha dawa alipokea adhabu hiyo, na kusema kwamba ni kubwa sana wanaomba serikali iwapunguzie adhabu hiyo, kwa kuwa ni kosa la mara ya kwanza.

Akiwakilisha wakazi wa eneo la Keko, Mtendaji wa Kata hiyo Samweli Magali alisema kero ya uchafuzi wa mazingira inayotokana na kiwanda hicho cha dawa ni kubwa na ni hatarishi kwa afya za wakazi wa eneo hilo.

SOURCE HABARI LEO

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *