Home / Habari Za Kitaifa / Viongozi Kanisa Katoliki wamruka Askofu mchakato wa Katiba Mpya

Viongozi Kanisa Katoliki wamruka Askofu mchakato wa Katiba Mpya

SIKU chache baada ya Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge, Ngara mkoani Kagera, Severine Niwemugizi kusikika akidai Katiba mpya ndiyo kipaumbele cha sasa kwa wananchi, viongozi wa juu wa kanisa hilo wametoa msimamo rasmi wa kanisa hilo.

Viongozi hao ni pamoja na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Kadinali Polycarp Pengo na Balozi wa Vatican nchini, Askofu Marek Solczynski. Viongozi hao wa kanisa hilo nchini wamewataka waumini wa kanisa hilo na Watanzania kwa ujumla kuyachukulia maoni hayo kuwa si msimamo wa Kanisa Katoliki.

Akizungumza Dar es Salaam jana Kadinali Pengo alisema kuwa kauli iliyotolewa hivi karibuni na Askofu Niwemugizi ni maoni binafsi na si msimamo wa Kanisa Katoliki nchini. Mwadhama Kadinali Pengo alisisitiza hilo wakati akitoa ufafanuzi juu ya sintofahamu iliyojitokeza miongoni mwa Watanzania na waumini wa Kanisa hilo kutokana na kauli ya Askofu Niwemugizi.

“Napenda kutamka moja kwa moja kwamba huo si msimamo wa Kanisa na hauwezi kuwa msimamo wa kanisa kwa sababu sisi tuna taratibu zetu za kuishauri serikali au kuzungumzia masuala ya jamii,” alisema.

Alisema kutokana na nafasi ya Uaskofu aliyonayo Askofu Niwemugizi, kauli yake inaweza kutafsiriwa kuwa ndiyo msimamo wa Kanisa Katoliki au wa Jimbo la Rulenge, Ngara lakini kimsingi kauli hiyo imekosa vigezo vya kuichukulia kama msimamo wa Kanisa au jimbo anakotoka.

Akizungumzia juu ya suala la Katiba Mpya ambalo baadhi ya wanaharakati na wanasiasa wanajaribu kuligeuza kuwa ajenda kuu kwa sasa, Kadinali Pengo alisema yeye binafsi kipaumbele chake ni kuona huduma za jamii kama zile elimu na afya zinaendelea kuboreshwa kwa kasi kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli inavyofanya.

“Mtu akiniambia priority (kipaumbele) ya Tanzania ni Katiba Mpya inabidi anithibitishie huo ukipaumbele maana siwezi kuona mtoto anakufa kwa njaa au kwa kukosa dawa eti kwa sababu ya Katiba Mpya.

Kwangu mimi Katiba ni kitu ambacho kije baadaye, si cha haraka. “Wanasiasa wasiache watoto wetu wafe kwa njaa kisa malumbano ya Katiba. Wasiache watoto wakose shule kwa sababu hela zote zimeishia kwenye malumbano juu ya Katiba,” alisisitiza Kadinali Pengo.

Kwa upande wake Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu Solczynski hakutofautiana na kauli ya Kadinali Pengo kwa kusema kuwa pamoja na kwamba Askofu Niwemugizi ana haki ya kutoa maoni yake lakini tatizo linakuja pale watu wakaposhindwa kung’amua kuwa ni maoni binafsi au ni ya Kanisa.

Alisisitiza kuwa Kanisa lina taratibu zake za kutoa maoni kwa masuala ya kijamii na kwa Serikali. “Hayo ni maoni yake binafsi na wala yasihusishwe na Kanisa Katoliki,” alisema Balozi Askofu Merek.

Hivi karibuni Askofu Niwemugizi alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kipaumbele cha kwanza cha Watanzania ni Katiba Mpya na kuongeza yeye binafsi ni miongoni mwa watu walioipinga Katiba Inayopendekezwa.

Hata hivyo, wachambuzi wa mambo wanasema, pamoja na mjadala mkubwa ulioibuka na baadhi ya wanasiasa kususia mchakato wa kukamilisha Katiba Mpya, wataalamu wa sheria wanasema Katiba Inayopendekezwa ilikuwa ni bora kuliko ya sasa ikiwemo kuruhusu wagombea kuhoji mahakamani matokeo mbalimbali ikiwemo ya urais.

Wakili wa Mahakama Kuu, James Nandonde alisema; “Hata mimi ukiniuliza leo tuache kufanya mageuzi ya msingi katika jamii ili kuwa na uchumi imara au tuanze kushughulika na Katiba Mpya, nitakwambia tuachane na Katiba.

“Nakumbuka ile Katiba Inayopendekezwa ilikuwa na masuala makubwa yenye maslahi kwa nchi ikiwemo kipengele cha kupinga matokeo ya urais lakini kwa kuwa kuna watu walikuwa na maslahi yao binafsi, wakatoka nje ya Bunge na kukwamisha mchakato ule. “Sioni uharaka wa leo tuache mengine yote turejee kwenye mchakato huu,” alisema Nandonde.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *