Home / Habari Za Kitaifa / Shahidi aeleza walivyochagua bodi CUF

Shahidi aeleza walivyochagua bodi CUF

ALIYEKUWA Jaji wa Mahakama ya Zanzibar, Abubakari Khamis Bakari ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwa katika mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi (CUF) uliofanyika Mei 2013 alikuwa mjumbe na kwamba alishiriki kuchagua bodi ya wadhamini wa chama hicho.

Bakari ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar, alidai mbele ya Jaji Wilfred Ndyansobera wakati akitoa ushahidi katika kesi namba 51 ya mwaka 2017, ambapo Mbunge wa Malindi, Ally Saleh anahoji uhalali wa wajumbe walioteuliwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Lipumba na kuidhinishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA). Alidai kuwa bodi hiyo iliyochaguliwa ilipaswa kuisha muda wake Mei, 2018 na kwamba hivi karibuni Katibu wa bodi hiyo aliwasilisha maombi ya kuongeza wajumbe kutokana na waliokuwepo kutokuwa na sifa.

Akiulizwa maswali na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Gabriel Malata ambaye katika kesi hiyo anamwakilisha mdaiwa wa kwanza (RITA), Bakari alidai kwa mujibu wa katiba ya CUF, katibu wa bodi ya wadhamini anayo mamlaka ya kuchagua wajumbe wengine kutokana na sababu mbalimbali.

‘’Mimi ni mwanachama wa CUF tangu mwaka 1993 na ili mahakama iweze kuthibitisha kwamba mimi ni mwanachama halali napaswa kutoa kadi ya uanachama na pia kwa mujibu wa taratibu zetu hauwezi kuwa mjumbe wa baraza kuu kama si mwanachama,’’ alisema Bakari. Pia alidai kuwa bodi hiyo inapaswa kutumikia kwa miaka mitano na kwamba anatambua kuwepo kwa bodi moja.

Malata: Awali ulisema kuwa bodi ya wadhamini inapaswa kumaliza muda wake mwaka 2019 na sasa unasema inapaswa kumaliza muda wake mwaka 2018. Je, kauli ipi ya uongo kati ya hizo na wewe uliapa kusema ukweli kwa kutumia kitabu kitakatifu? Shahidi: Kama nilisema bodi ilipaswa kuisha muda wake mwaka 2019 basi ni ‘slip of tongue’ (akiwa na maana ya kwamba ulimi umeteleza) na sio kauli ya ukweli.

Bakari alisema kuwa kielelezo alichokitoa mahakamani hapo, ambacho ni muhtasari wa mkutano wa baraza kuu, hakina uhusiano na uteuzi wa bodi hiyo, kwa kuwa katika ajenda zote hakuna palipotaja bodi hiyo. Akijibu maswali ya Wakili Majura Magafu, shahidi huyo alidai anajua malalamiko ya mleta maombi ambaye ni Ally Saleh anayetaka kujua bodi iliyopo na nyingine ambazo zinatambulika ipi ni halali.

Alidai kuwa alisoma malalamiko hayo na kwamba katika ukurasa wa Kifungu cha 14 cha hati ya kiapo kilichoandikwa na Saleh, kimeonesha kuwa mwisho wa utendaji wa Bodi ya Wadhamini ni Machi 2017 baada ya kuchaguliwa mwaka 2012. Katika kesi hiyo Namba 51 ya mwaka 2017, Saleh anahoji uhalali wa wajumbe walioteuliwa na Profesa Lipumba na kuidhinishwa na Rita, ambao ni mdaiwa wa tatu mpaka wa 12.

Mbali na wajumbe hao wa kambi ya Lipumba, wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni wajumbe walioteuliwa na kambi ya Maalim Seif Hamad ambao majina yao yalipelekwa Rita ni Abdallah Khatau, Joran Bashange, All Suleiman, Juma Muchi, Mohamed Mohamed na Yohana Mbelwa, ambao katika kesi hiyo ni wadaiwa wa 13 mpaka 18.

Katika kesi hiyo, Mbunge huyo anaiomba mahakama itamke kama mdaiwa wa tatu mpaka wa 12 kwa mujibu wa Sheria chini ya Katiba ya chama hicho ya mwaka 1992 ya Toleo la mwaka 2014, wanastahili kuwa wajumbe wa bodi ya wadhamini.

Pia, anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa wadaiwa wa 13 mpaka wa 18, ambao pia ni miongoni mwa wajumbe wa bodi ya awali ni wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya CUF. Saleh anayewakilishwa na Wakili Mpale Mpoki, amefungua kesi hiyo chini ya hati ya dharura, akieleza kuwa suala hilo linahitaji kuamriwa haraka, kwa kuwa chama hicho kiko katika mgogoro mkubwa na wa hatari kisiasa, kutokana na Rita kusajili wajumbe wapya wa bodi hiyo.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *