Home / Habari Za Kitaifa / Hifadhi ya Serengeti yafurika watalii

Hifadhi ya Serengeti yafurika watalii

HIFADHI kongwe na maarufu ya Serengeti ambayo ni ya pili kwa ukubwa Tanzania, imeendelea kupata neema kubwa ya watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani, wanaopishana kila kukicha katika Uwanja mdogo wa ndege wa Seronera, ndani ya hifadhi hiyo.

Hayo yamethibitishwa na Ofisa Utalii, Evans Magomba alipokuwa anazungumzia hali ya utalii hivi karibuni, huku akisisitiza kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la safari za ndege zinazosafirisha watalii.

Ongezeko hilo la karibu kila mwaka sasa, linatajwa kusababishwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na uwepo wa wanyama wa kila aina, lakini pia kuwapo kwa tukio la kipekee duniani na kuhama kwa maelfu ya wanyama aina ya nyumbu kutoka Hifadhi ya Serengeti na kwenda nchi jirani ya Kenya na kisha kurejea nyumbani baada ya mzunguko wa safari ya umbali wa takribani maili 500.

Katika kuvutia watalii, Hifadhi ya Serengeti ambayo ni moja ya hifadhi maarufu za Tanzania iliyopo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), inafuatiwa na Hifadhi ya Ngorongoro na Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu zaidi barani Afrika.

“Serengeti inafurika watalii. Ni habari njema na hii inatupa ni changamoto kwetu kuongeza huduma bora kwa wageni,” alisema Magomba. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, kati ya Januari na Septemba mwaka 2017, jumla ya ndege 3,724 zilitua katika uwanja wenye pilika nyingi wa Seronera uliopo katikati ya hifadhi yenye uwanda mpana ya Serengeti.

Kwa miezi ya Julai, Agosti na Septemba, 2017, kulikuwa na idadi ya safari za ndege 1,742 zilitoa katika hifadhi hiyo ikilinganishwa na idadi ya safari za ndege 1,238 zilizotua katika miezi kama hiyo mwaka 2016.

Ndege zilizotua katika viwanja vingine ndani ya hifadhi hiyo vya Kogatende na Lobo, ambako kuna maeneo ya vivutio ya wanyama aina ya nyumbu wanaohama kila mwaka kwenda nchi jirani na kurejea, pia zimeongezeka.

Kumekuwa na idadi ya ndege zilizotua 564 Julai mwaka huu pekee katika kiwanja cha Kogatende, ikilinganishwa na idadi ya safari za ndege 110 zilizotua Lobo katika mwezi huo. Ofisa Mwandamizi wa Uhamasishaji Utalii katika Hifadhi ya Serengeti, Susuma Kusekwa alisema kuhama kwa nyumbu ni sehemu ya mambo yanayovutia watalii, lakini kuna mambo mengine zaidi yanayoongeza hamasa ya kutembelea hifadhi hiyo.

“Si rahisi kuona wanyama katika majira yote ya mwaka, lakini watu wanafurika kutokana na kufikika kwa urahisi na pia kuimarishwa na kuongeza kwa maeneo ya makazi kwa ajili ya watalii,” alisema.

Hifadhi ya Serengeti Hifadhi ya Serengeti ni eneo kubwa la mbuga na misitu iliyopo katika eneo la kilometa za mraba 14,763 Kaskazini mwa Tanzania, hasa katika mikoa ya Mara na Arusha ikipakana na nchi jirani ya ya Kenya.

Ni hifadhi yenye idadi kubwa ya wanyamapori, lakini ikijipatia umaarufu mkubwa kutokana na kitendo cha wanyama aina ya nyumbu zaidi ya milioni mbili kuhama nchi kutoka Serengeti kwenda Hifadhi ya Masai Mara, Kenya.

Tukio lao la kuvuka mpaka huwa la karibu nusu mwaka na linatajwa kuwa ni moja ya maajabu kumi ya asili ya ulimwengu ya kusafiri. Uhamaji wao unaihusisha safari ya takribani maili 500, umekuwa kivutio na hata filamu na programu nyingi za televisheni duniani zimekuwa zikionesha tukio hilo. Mbali ya nyumbu, aina nyingine ya wanyama wanaoongeza mvuto kwa watalii katika hifadhi ya Serengeti ni pamoja na tembo, simba, chui, fisi, kifaru na nyati.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *