Home / Habari za Kimataifa / Kunayo mipaka kati ya dini na siasa Tanzania?

Kunayo mipaka kati ya dini na siasa Tanzania?

Rais Magufuli baada ya kushiriki Sakramenti Takatifu katika ibada iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Petro Parokia ya Oysterbay jijini Dar es Salaam mnamo 31 Desemba
Mwaka 2018 hatimaye umeanza. Wengi wamekuwa wakiusubiri kwa hamu wakidhani kwamba, huenda kuanza kwa mwaka mpya kunaweza kuleta mambo mapya au afueni katika baadhi ya mambo ambayo kwao pengine yalikuwa na ugumu kwa mwaka uliopita.

Kuanza kwa mwaka huu, katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki, kuna mambo ambayo tayari yamegusa hisia za wengi.

Takriban idadi kubwa ya nchi hizi zinaonekana hazijaanza mwaka vizuri.

Mathalan, kule nchini Kenya, ajali ya basi baada ya kugongana uso kwa uso na lori na kusababisha vifo vya takriban watu 40 na wengine kujeruhiwa.

Haikuwa habari nzuri kwa ajali hiyo ambayo imetokea siku moja tu kabla ya kuanza mwaka huu.

Msiba huu mbali na kugusa nyoyo za wengi, lakini pia ilimgusa rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta ambaye alituma salamu zake za rambirambi kwa taifa lakini zaidi kwa wafiwa.

Kana kwamba hiyo haitoshi, nako nchini Uganda, tumeshuhudia kifo cha polisi, hii ikiwa ni mwendelezo wa matukio ya namna hiyo ambayo yamekuwa yakilenga askari nchini humo.

Maandamano dhidi ya Kabila
Nchini DRC nako, waliamua kuukaribisha mwaka kwa namna yake, nayo haikuwa nyingine bali kufanya maandamano yanayopinga kuendelea kwa Rais Joseph Kabila kuwepo madarakani.

Maandamano hayo yalisababisha vifo vya watu wanane.

Nchini Tanzania hali ilikuwa tofauti kidogo. Viongozi wa dini nchini humo, kwa pamoja waliamua kutumia sikukuu ya Krismasi na ile ya Mwaka Mpya, kuhutubia amani lakini zaidi kuinyooshea kidole serikali kwa maana ya kuikosoa katika baadhi ya mambo.

Aliyefungua ukurasa huo si mwengine, bali ni askofu wa kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zakaria Kakobe ambae amenukuliwa akiitaka serikali itoe fursa kwa vyamba vya upinzani kutekeleza wajibu wake.

Watu 36 walifariki katika ajali iliyohusisha lori la basi la uchukuzi wa abiria eneo la Migaa barabara ya kutoka Nakuru kwenda Eldoret nchini Kenya
Hii ni baada ya serikali kupiga marufuku mikutano ya hadhara kwa vyama vya kisiasa.

Hatua ambayo, wengi wanaiona kama ni ukandamizwaji wa demokrasia.

Hata hivyo, kauli za viongozi hawa wa dini kwa serikali haikupokewa vizuri.

Serikali kuwaonya viongozi wa kidini
Inaonekana tayari kumeibuka mvutano baina ya serikali na baadhi ya viongozi wa dini ambao kwa nyakati tofauti wamenukuliwa wakionyesha kuwa na mtizamo tofauti na serikali, hasa katika suala zima la kuikosoa katika baadhi ya mambo.

Serikali ya Tanzania imewatahadharisha viongozi hao wa dini kwa kuwa wanaingilia siasa. Hivyo kuwataka wakae mbali kabisa masuala ya kisiasa.

Lowassa: Kuna dalili za ‘udikteta’ serikalini Tanzania
Kauli hii ya serikali inaonekana kuzua mjadala mkali nchini, huku baadhi wakihoji ni ipi mipaka ya dini na siasa? Au ni wapi au ni wakati gani ambapo viongozi wa dini wanaruhusiwa kuzungumzia siasa na ni wakati gani ambapo hawaruhusiwi?

Tayari, baadhi wameshuhudia wakati fulani wanasiasa wakikimbilia kwa viongozi wa dini na kuwataka wazungumze na wafuasi wao baadhi ya mambo ya siasa.

Na sio hivyo tu, baadhi ya wanasiasa wameonekana mara kadhaa wakikimbilia katika nyumba za ibada hasa wanapoona mambo yamewafika kooni, aidha kwa kutaka kuombewa au kuwaomba viongozi wa dini kutumia ushawishi wao kwa wafuasi wao ili wawapigie kura.

Ni kwa sababu hiyo, ndio maana msimamo wa serikali dhidi ya viongozi wa dini unaonekana kupokelewa kwa hisia tofauti.

Ingawa wapo wanaoungana na serikali kwa kuona kwamba viongozi wa dini jukumu lao ni la kiroho zaidi hivyo wajikite katika masuala kama vile ya ndoa, kutoa sadaka na kuhimiza watu kufanya ibada.

Maalim Seifn anaamini viongozi wa kidini wana haki kuikosoa serikali
Lakini pia wapo wasiokubaliana na fikra hiyo. Kwa mfano, Maalim Seif ambaye ni katibu mkuu wa Chama cha Wananchi CUF ameshauri viongozi hao waachwe wazungumze kwa sababu bila shaka watakuwa wameona kasoro za kiutendaji serikalini.

Akinukuliwa na moja wa gazeti maarufu nchini Tanzania, Maalim ambaye pia amewahi kuwa makamu wa rais wa kwanza Katika serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar amesema viongozi wa dini bila shaka itakuwa wamehisi kuna kasoro ndani ya serikali ndiyo maana wameamua kutoa dukuduku.

Ni mara ya kwanza?
Hata hivyo, ikumbukwe kwamba, hii sio mara ya kwanza kwa viongozi wa dini kuibuka na kuanza kuinyooshea vidole serikali iliyopo madarakani.

Hayo yametokea katika awamu zote, ikiwemo serikali ya awamu ya nne ambayo ndio imetoka madarakani.

Vitisho vya kuyafuta mashirika ya kidini vyazua hisia Tanzania
Mara kadhaa viongozi wa dini walionyesha kutoridhishwa kwao kwa jinsi mambo yanavyokwenda.

Na hii pia sio mara ya kwanza kwa mjadala wa viongozi wa dini kulaumiwa kwa misingi ya kuchanganya dini na siasa kuibuka.

Ingawa wapo wanaoamini kwamba, viwili hivi katu haziwezi kuepukika kwani uhusiano wake ni wa karibu sana, aidha kimoja kipo kwa mwengine, au kingine kimemmeza mwenzake.

Siasa katika mahubiri
Pierre Whalon, ambaye ni askofu wa mkusanyiko wa makanisa katika nchi za Ulaya anasema, kwa mara kadhaa amekuwa akifuatwa na watu na kuambiwa aache kuingiza siasa katika mahubiri yake.

Hata hivyo, anasema, muhimu ifahamike katika historia ya binadamu kwamba siasa na dini ni vitu viwili ambavyo haviwezi kutenganishwa.

“Kwa maana hiyo, haiwezekani kutenganisha dini na siasa, na yeyote anayejaribu kufanya hivyo, aidha anadanganya au hajafikiria vizuri,” anasema mchungaji huyo katika moja ya makala zake yenye kichwa, ‘Religion and Politics Are Inseparable: Get Over.’ (Dini na Siasa haziwezi Kutenganishwa: Kubali hayo).

Suala la dini na siasa ni la muda mrefu sana, na halijazua mjadala katika nchi za Kiafrika pekee, bali hata katika zilizoendelea ambazo wengi wanaamini kwamba ndipo kwenye ukomavu wa demokrasia.

Sababu ya CCM kuendelea kuongoza Tanzania
Swali hili pia limejitokeza katika kitabu kiitwacho, Religious Convictions and Political Choice (Itikadi za Kidini na Uamuzi wa Kisiasa), kilichoandikwa na Kent Greenawalt.

Swali hilo hilo, limejibiwa katika kitabu cha zaidi ya kurasa 200, lakini mwisho wa siku, imeonyesha dhahiri kwamba, siasa na dini vina ukaribu mkubwa sana, na imani ya dini siku zote ina ushawishi mkubwa sana hata kwa wanasiasa wenyewe.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Mbunge Bobi Wine akamatwa Uganda baada ya dereva wake kuuawa

  Boni Wine Mbunge nchini Uganda Robert Kyagulanyi maarufu kama Boni Wine amekamatwa na polisi …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *