Home / Habari Za Kitaifa / Ekari 366 zarasimishwa kwa ‘wavamizi’ Dar

Ekari 366 zarasimishwa kwa ‘wavamizi’ Dar

SERIKALI imerasimisha ardhi yenye ekari 366 eneo la Somji iliyopo katika Mtaa wa Dovya, Kata ya Bunju jijini Dar es Salaam kwenda kwa wananchi wa eneo hilo na kuwahakikishia kuwapatia hati halali za umiliki wa eneo hilo.

Hatua hiyo inatokana na kuwepo kwa mgogoro wa muda mrefu wa umiliki wa eneo hilo baada ya wananchi kuvamia eneo hilo ambalo awali lilikuwa la Somji na baadaye kutwaliwa na serikali kwa manufaa ya umma. Kutokana na hatua hiyo ya serikali, wananchi waliovamia eneo hilo maarufu kwa Somji, hawataondolewa wala kuvunjiwa, litatakiwa kupimwa na kupangwa na kila aliyejenga kutakiwa kulipa kodi ya ardhi.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipofanya ziara katika eneo hilo na kuzungumza na wananchi kwa lengo la kutatua mgogoro huo uliodumu muda mrefu. Lukuvi alisema ardhi ya Somji ilitwaliwa kwa manufaa ya umma kuanzia mwaka 1975, lakini kwa mujibu wa sheria ya mwaka huo, lazima mmiliki huyo alipwe fidia na serikali haijalipa.

Alisema mwaka 2003, Somji alifungua kesi kuishtaki serikali, lengo lake Mahakama ifunge mamlaka ya Rais ya kuitwaa ardhi hiyo, na kesi iliendelea na uamuzi kutolewa Aprili 30, 2010 ambayo Somji na wenzake walishindwa. “Mahakama ilikubali uamuzi wa Rais kuchukua eneo hilo, lakini kwa Somji alitakiwa kulipwa fidia, hivyo hati yake ni fidia na serikali kuendelea na ardhi hiyo,” alifafanua Lukuvi kuhusu mgongo huo na kuongeza kuwa kwa sasa ardhi hiyo ilikuwa ni ya serikali.

Alisema baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kufuatilia suala hilo, anaelekeza mipaka ya eneo la hilo lililojulikana kwa Somji kuanzia mwaka 1952 ifukuliwe ijulikane na timu ya watalamu wa Manispaa na wizara itafanya kazi hiyo huku ikihakikisha ifikapo Septemba mwaka huu, kazi hiyo iwe imekamilika na wananchi kupatiwa hati zao kihalali. Lukuvi alisema baada ya upimaji na upangaji kufanyika, kila mkazi wa eneo hilo aliyejenga anapaswa kulipa fidia kwa Somji kwa mujibu wa gharama ya ardhi. Aliwataka wakazi wa eneo hilo kuunda kamati ili kazi zote zifanywe kwa ushirikiano na Kamati ya Wananchi na Ofisi ya Mipango Miji ya Manispaa ya Kinondoni lazima ibainishe kwamba baada ya kufutwa kwa umiliki wa ardhi hiyo kama kuna mipango mingine na Kamati ya Wananchi ifahamu.

Alisema timu hiyo pia ibainishe kama kuna upimaji wowote mpya ulifanyika hapo, watu wenye hati au ofa wakabidhi katika kamati hiyo ili ijulikane walizipataje na kama ni halali. Lukuvi alisema wakazi wote wenye chochote waorodheshe, wakitaja pia historia zao na kuonesha majengo yao kwa kuwa serikali imeamua eneo hilo lazima lipimwe lipangwe na kumilikisha, lakini upimaji ufanywe kisasa, bila kumvunjia yeyote nyumba lengo ni kumilikisha urasimishaji.

Alisema kila mmoja atakayepimiwa na kupewa kipande chake cha hati atambue kuwa serikali haitotoa fedha ya kumlipa fidia Somji, bali ni kila mkazi na anayeona hana uwezo aseme nyumba yake ivunjwe ili Somji alipwe. Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi alitoa rai kwa matapeli kwamba wakithubutu kuingia katika eneo hilo kuwatapeli wananchi hao atakwashughulikia kwa mujibu wa sheria. Aliwataka wananchi hao kutosita kutoa taarifa kwa mtu yeyote atakayevamia katika eneo hilo.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

wakulima tanzania

Wakulima Tanzania watafuta masuluhisho kwa changamoto zao

Wakulima nchini Tanzania wameonya kuwa huenda nchi hiyo ikaingia kwenye baa la njaa kutokana na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *