Home / Habari Za Kitaifa / Mshahara wa Waziri ulivyoshikiliwa

Mshahara wa Waziri ulivyoshikiliwa

MSHAHARA wa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage juzi ulishikiliwa mara kadhaa na wabunge waliokuwa wakionesha ukali wao kuhusu ufufuaji wa viwanda nchini na mradi unganishi wa mchuchuma na Liganga.

Aidha, wabunge hao walikuwa wanataka kujua hali na kauli za serikali kuhusu malipo ya fidia kwa wananchi walioacha ardhi yao bila maendeleo kwa taribani miaka 15 kupisha ujenzi wa maeneo maalumu ya kiuchumi. Pia wabunge hao walitaka kujua mikakati mahususi ya serikali ya kulinda viwanda hivyo. Ushikiliaji wa mshahara wa waziri kwa kutoa shilingi katika mshahara wake ni kanuni inayotumika na wabunge kutaka kauli mahsusi za serikali kuhusu mambo yanayoumiza kichwa katika maeneo yao au kitaifa.

Kutokana na ushikiliaji huo wa shilingi, mawaziri kadhaa walilazimika kusimama kutoa maelezo na kutoa kauli zinazoonesha uthabiti wa serikali katika utekelezaji wa majukumu yake. Hata hivyo, Bajeti ya wizara hiyo ilipita juzi baada ya sehemu kubwa ya wabunge kuridhika na kauli za serikali na kurejesha shilingi. Mawaziri ambao walisimama kutetea urejeshaji wa shilingi ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama ambaye pia ni mnadhimu bungeni, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.

Aliyeanzisha hekaheka hizo ni Mbunge wa Viti Maalumu, Hawa Chakoma (CCM) ambaye alisema kwamba malipo kwa fidia za watu waliopisha maeneo maalumu yamekaa kwa muda mrefu. Pamoja na maelezo ya waziri mwenyewe na Waziri Jenista, Mbunge huyo aliing’oa shilingi na kutaka maelezo mahsusi huku akiungwa mkono na wabunge zaidi ya 15 wa upande wa CCM akiwemo mbunge wa Bagamoyo, Shukuru Kawambwa (CCM). Baada ya vuta nikuvute serikali ilisema kwamba itaendelea kulipa fedha hizo na mbunge kuirejesha shilingi kwa maelezo kwamba fedha hizo zilizotengwa kwa fidia zifanyiwe ‘fencing’ ili zitumike kwa kazi hiyo hiyo.

Mbunge mwingine aliyeshika shilingi ni mbunge wa Kahama, Mjini Jumanne Kishimba (CCM) ambaye alitaka mkakati mahususi wa kulinda viwanda vya ndani. Pamoja na maelezo ya Waziri Mwijage na kwenye hotuba yake ya bajeti mbunge huyo alishikilia shilingi mpaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliposimama na kutoa maelezo nini watafanya kuhakikisha kwamba viwanda vya ndani vinalindwa. Aidha alisema katika bajeti kuu ataeleza mikakati ya serikali ya kulinda viwanda vya ndani.

Mbunge wa Viti maalumu, Kiteto Koshuma (CCM) yeye aliondoa shilingi akitaka maelezo ya viwanda vinavyofufuliwa akitaka idadi yake na kusema kwanini serikali isiangalie viwanda 62 vinavyojiendesha kwa kusuasua. Mvutano mkubwa ulikuwa katika eneo hilo ambapo aliungwa mkono na wabunge kadhaa wakiwemo wa upinzani ambao walitaka mji wa Morogoro kurejeshewa heshima yake ya viwanda kwa viwanda vyote kufufuliwa. Awali wakichangia kuhusu ufufuaji wa viwanda wabunge wa Morogoro wakiwemo wa upinzani walitaka serikali kujielekeza katika kufufua viwanda vya Morogoro na wale waliotumia viwanda hivyo kukopa na kisha kuvitelekeza kuchukuliwa hatua.

Mbunge Devotha Minja, Joseph Haule (Chadema) na wabunge wa CCM walisema haionekani njema ya serikali hasa kwa kuona kwamba hadhi ya Morogoro iliyowekwa tangu enzi za Mwalimu kwa kuwa katikati inatelekezwa. Mwijage katika majibu yake alitoa maelekezo ya hatua mbalimbali zinazofanywa katika kukabiliana na tatizo hilo la viwanda 156 vilivyobainishwa na kusema kwamba kiwanda kama cha ceramic hakipo kabisa kwa kuwa aliyekinunua alikabiliwa na tatizo la mkpoo wa TIB na mali zake kuuzwa. Hata hivyo amesema kwamba bado anaendelea na utaratibu wa kufufua viwanda. Naibu Waziri, Abdallah Ulega alisema kwamba serikali inafanya juhudi zote kuhakikisha kwamba viwanda vya ngozi vinafufuliwa na kuongeza kwamba imerejesha kiwanda cha ngozi, Mwanza na Tripple S cha Shinyanga pia vinatafitiwa wabia wengine.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

wakulima tanzania

Wakulima Tanzania watafuta masuluhisho kwa changamoto zao

Wakulima nchini Tanzania wameonya kuwa huenda nchi hiyo ikaingia kwenye baa la njaa kutokana na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *