Home / Afya / Ndoa za ukoo mmoja hatari Kwa magonjwa ya kurithi

Ndoa za ukoo mmoja hatari Kwa magonjwa ya kurithi

MAGONJWA ya urithi ni aina ya magonjwa yanayosababishwa na hitilafu kwenye vinasaba na hivyo kurithiwa kutoka kwa wazazi.

Hitilafu hizi zinaweza kutokea kwenye kinasaba cha aina moja au vinasaba vingi kwa pamoja na aina ya ugonjwa itategemea vinasaba gani vimeathirika. Mfano wa magonjwa yanayosababishwa na hitilafu kwenye vinasaba ni pamoja na ugonjwa wa seli mundu (sickle cell disease), haemophilia (tatizo la damu kutoganda) na baadhi ya magonjwa ya mifupa.

Magonjwa mengine ya kurithi husababishwa na mchanganyiko wa hitilafu kwenye vinasaba pamoja na mazingira ya mtu. Kwa mfano ugonjwa wa kisukari, shinikizo la juu la damu na baadhi ya saratani. Mfumo wa kurithisha magonjwa haya ni mgumu kuutambua kwa sababu ya kuhusisha vitu vingi. Kila chembechembe hai ya mwili wa binadamu ina vinasaba kutoka kwa baba na mama kwa uwiano sawa (nusu kwa nusu). Vinasaba hivi ndiyo vinatengeneza sifa mbalimbali za muonekano wa mtu kwa nje kama vile rangi ya macho, rangi ya ngozi na urefu; na sifa za ndani kama vile kemikali za mwilini, ufanyaji kazi wa viungo pamoja na uwezekano wa kupata magonjwa ya aina fulani.

Vinasaba vinavyoweza kuleta ugonjwa vinarithishwa kwa watoto na hata hivyo kuugua ugonjwa husika kwa mtoto aliyerithi vinasaba hivyo hutegemea aina ya hitilafu na kama vinasaba alivyotoa kwa mzazi ambaye hana hitilafu vinaweza kuzuia asipate ugonjwa. Hivyo basi upo uwezekano wa kuwa na vinasaba vya ugonjwa fulani lakini usiugue huo ugonjwa. Zipo aina kuu tatu za kupata ugonjwa kutokana na kurithi vinasaba vya ugonjwa huo kutoka kwa wazazi. Aina ya kwanza ni ile ambayo nusu ya vinasaba vilivyoathirika vinasababisha ugonjwa kutokea hata kama nusu nyingine kutoka kwa mzazi wa pili haina tatizo. Ili kupata ugonjwa wa aina hii, ni lazima mzazi mmoja au wote wawili wawe wanaugua ugonjwa husika.

Endapo mzazi mmoja anaugua na mmoja haugui (hana vinasaba vya ugonjwa huo), mtoto anayezaliwa ana uwezekano wa asilimia 50 ya kupata ugonjwa husika. Magonjwa yanayorithiswa kwa aina hii si mara nyingi kutokea mfano ni ugonjwa wa viungo vya mwili unaojulikana kama Marfan Syndrome. Mfano kwa kurithi ugonjwa D Aina ya pili ni ile ambayo ili ugonjwa utokee ni lazima vinasaba kutoka kwa baba na kutoka kwa mama viwe vimebeba hitilafu. Wazazi ambao wana vinasaba vya ugonjwa lakini hawaugui, wana uwezekano kwa asilima 25 ya kupata mtoto mwenye ugonjwa husika na watoto wengine kuwa na vinasaba vyenye hitilafu bila kuugua (carriers).

Endapo mzazi mmoja hana vinasaba vya ugonjwa huo, hakuna mtoto atakayeugua japokuwa kuna ambao watakuwa na vinasaba vyenye ugonjwa. Mfano wa ugonjwa unaorithiwa kwa njia hii ni seli mundu. Mfano wa kurithi ugonjwa D Aina ya tatu ni ya kurithi hitilafu iliyopo kwenye vinasaba vinavyobeba sifa ya jinsia. Magonjwa mengi ya aina hii huwapata wanaume zaidi kuliko wanawake kwa sababu vinasaba vya jinsia kwa wanaume ni XY na kwa wanawake ni XX, hivyo endapo hitilafu ipo kwenye kinasaba X, ni rahisi kujitokeza kwa mwanaume kwa kuwa ana X moja wakati kwa mwanamke X ya pili inaweza kumlinda asipate ugonjwa husika. Mfano wa ugonjwa unaorithiwa kwa jinsi hii ni haemophilia.

Magonjwa ya kurithi yanatokea kwa wingi kwenye jamii ambazo zina kawaida ya kupata watoto baina ya watu wa familia/koo zenye uhusiano, kwa sababu vinasaba vyenye ugonjwa vinaendelea kurithishwa kwenye vizazi. Vinasaba vya ugonjwa vinaweza kuwepo kwenye familia/ukoo mmoja lakini inapokuwa kwa upande wa mzazi mmoja, ugonjwa husika unaweza usijitokeze katika vizazi. Hata hivyo endapo watu wawili wa ukoo huo watazaa mtoto kunakuwa na uwezekano wa ugonjwa huo kujitokeza. Hii ni sababu mojawapo ya ushauri wa kutokupata watoto baina ya ndugu.

Magonjwa mengi ya kurithi hugundulika wakati wa utoto, kwa wale ambao wameathirika nayo. Hata hivyo si rahisi kugundua wale ambao wana vinasaba lakini hawana ugonjwa kwa kuwa wanaweza kuendelea na maisha yao kama kawaida. Vipimo vya kutambua vinasaba vya magonjwa ya kurithi havifanyiki mara kwa mara, kwa sababu magonjwa mengi hayatokei kwa kiasi kikubwa kwenye jamii isipokuwa machache kama vile seli mundu.

Iwapo kwenye familia kuna watoto au ndugu wanaougua aina moja ya ugonjwa ni vizuri kutambua endapo ugonjwa huo ni kati ya magonjwa ya kurithi. Vilevile endapo mmoja wa wanafamilia amegundulika kuwa na ugonjwa wa kurithi, ni vizuri ndugu wa kuzaliwa wakapime kuona kama wana vinasaba vya ugonjwa huu. Hii inasaidia hasa kwa magonjwa ambayo yanajitokeza kwa wingi kwenye jamii au kwenye eneo fulani.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

WANAWAKE WATAKIWA KUNYONYESHA WATOTO MAZIWA YAO PEKEE

WANAWAKE wametakiwa kunyonyesha watoto maziwa ya mama pekee bila kuwapa maji, kinywaji au chakula kingine …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *