Home / Michezo / Ubingwa wazidi kunoga Simba baada ya ushindi wa 1-0

Ubingwa wazidi kunoga Simba baada ya ushindi wa 1-0

MABINGWA wa Ligi Kuu Bara, Simba wameendelea kuweka heshima ya kutopoteza mchezo baada ya kushinda bao 1-0 dhidi ya Singida United kwenye uwanja wa Namfua, Singida.

Huu ni mchezo wa tatu mfululizo kwa mabingwa hao kupata ushindi mwembamba wa bao moja, baada ya ule wa Yanga na Ndanda iliyofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, awali ilikuwa ikishinda kuanzia mabao mawili mpaka matano katika mechi moja. Ushindi huo unamaanisha Singida imeshindwa kupata pointi hata moja kwa Simba msimu huu baada ya kufungwa mabao 4-0 kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Bao pekee la Simba katika mchezo wa jana lilifungwa na beki Shomari Kapombe katika dakika ya 24 baada ya kutumia makosa ya mabeki wa United baada ya kugongana wenyewe na kuacha mpira ukizagaa eneo la hatari.

Baada ya kufungwa bao hilo Singida iliamka na kuanza kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa wapinzani wao huku beki Shafiq Batambuzi akikosa nafasi ya wazi dakika ya 29 na kufanya kwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao hilo. Kipindi cha pili kilianza kwa vijana wa kocha Hans van Pluijm kulisakama lango la Simba huku wakikosa nafasi za wazi ambapo mshambuliaji Papi Kambale alikosa nafasi ya wazi baada ya kupokea pasi kutoka kwa Deus Kaseke. Simba walifanya mabadiliko ya kumtoa mshambuliaji Laudit Mavugo na kuingia Haruna Niyonzima ambaye alirejea kwa mara ya kwanza baada ya kuwa majeruhi muda mrefu.

Pamoja na kujaza viungo eneo la kati, bado Simba ilionekana kuzidiwa katika eneo hilo na kuandamwa muda wote wakati Singida wakihitaji kusawazisha. Singida ilifanya mabadiliko ya kumtoa Kambale ambaye alionekana kutokuwa na mchezo mzuri jana na kuingia Danny Usengimana ambaye pia alifuata nyayo hizohizo za kukosa nafasi za wazi. Wakati mchezo ukielekea mchezaji James Kotei alifanyiwa mabadiliko na kuingia Said Ndemla, kabla ya dakika ya 84 kutoka Emmanuel Okwi na kuingia Shiza Kichuya. Kwa matokeo hayo Simba imeendelea kuwaka rekodi yake ya kutopoteza mchezo na kujikita kileleni zaidi kwa pointi 68 ikifuatiwa na Azam FC wenye 52.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Nyota wa Afrika wamkumbuka mmiliki wa Leicester City Vichai Srivaddhanaprabha

Riyad Mahrez (kushoto) ni mmoja ya walitoa heshima zao kwa Vichai Srivaddhanaprabha Wachezaji wa Kiafrika …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *