Home / Habari Za Kitaifa / JPM atoa maagizo 5 mazito mafuta ya kula

JPM atoa maagizo 5 mazito mafuta ya kula

RAIS John Magufuli ametoa maagizo matano kwa watendaji wa wizara na idara za serikali, alipofanya ziara ya kushtukiza muda wa saa 6.30 mchana, kufuatilia sakata la mafuta ya kula kwenye Bandari ya Dar es Salaam jana, ikiwemo kuagiza mafuta hayo kutolewa bandarini haraka.

Rais Magufuli alitoa maagizo hayo, baada ya kupokea ripoti ya timu ya uchunguzi juu ya uhalisia na ubora wa mafuta ya kula iliyoongozwa na Profesa Joseph Buchweishaija. Timu hiyo ilifanya uchunguzi katika matangi 43 yenye tani 105,630 za mafuta ya kula, ambapo ilibaini kuwa kati ya matangi hayo, 7 yana na mafuta yaliyoboreshwa (refined oil), 14 yana mafuta yaliyoboreshwa kiasi (semi refined oil), 4 yana mafuta ya kutengenezea sabuni (refined stearin) na 18 ni mafuta ghafi (crude oil).

Matokeo ya ripoti hiyo yameonesha kuwa tofauti na taarifa zilizowasilishwa TRA na kampuni za uagizaji wa mafuta za Vegetable Oil Terminal (VOT), Tanzania Liquid Storage (TLS) na East Coast Oils and Fats Limited (EC), ambazo zilionesha sehemu kubwa ya mafuta hayo ni ghafi ambayo hutozwa kodi asilimia 10, imebainika kuwa kuna kiasi kikubwa cha mafuta yasiyo ghafi na ambayo yanapaswa kutozwa kodi asilimia 25. Katika ziara hiyo bandarini jana, Rais Magufuli alipokea taarifa kutoka kwa watendaji wake, akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Elisante Ole Gabriel, Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Ben Usaje na wengineo. Usaje alimweleza Rais Magufuli kuwa wafanyabiashara walidanganya, kwa kusema kuwa mafuta yote waliyoyaingiza yalikuwa ghafi, kauli ambayo TRA waliitilia shaka.

Kwa mujibu wa Usaje, Mei 12, mwaka huu, TRA walichukua sampuli tatu kutoka katika kila tangi kati ya matangi 13 yaliyokuwepo eneo hilo la kuhifadhia mafuta bandarini hapo. Baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Magufuli aliagiza kwamba matangi mawili (ambayo ni namba 4 na 12) ambayo yana viwango vya mafuta safi (double refined oil) yalipiwe chaji ya asilimia 25, matangi manne ambayo yana malighafi ya kutengeneza sabuni yachajiwe asilimia 10 na yaliyobaki ambayo ni mafuta ghafi, yalipiwe chaji ya asilimia 10 kama sheria inavyosema. Akifafanua, kwa upande wa Tanzania Liquid Storage (TLS), Rais Magufuli alisema kuwa tangi namba 3 ambalo lina mafuta yaliyosafishwa (refined oil), yalipiwe asilimia 25 na yaliyobaki yalipiwe asilimia 10.

Kwa upande wa sampuli za mafuta ya East Coast Oils & Fats Ltd, Rais Magufuli alisema kuwa mafuta mengine yote ni yale yaliyosafishwa kiasi (semi-refined oil) ambayo yanachajiwa asilimia 25, lakini pia matangi manne ambayo ni ECB1, ECB2, ECB 9 na EC3, ambayo ni mafuta safi (double refined oil) yachajiwe asilimia 25. Alisema baada ya taratibu zote kukamilika, mafuta hayo yanaweza kwenda sokoni, kwa kuwa serikali imejiridhisha kuwa hayana kemikali hatarishi kwa afya ya binadamu. Mbali na agizo hilo la kutaka mafuta hayo yalipiwe, Rais Magufuli pia aliziagiza mamlaka husika, kuwapiga faini wafanyabiashara ambao wamedanganya katika taarifa zao.

Alisema kama mfanyabiashara alisema mafuta aliyoyaleta ni ghafi na kisha ikabainika kuwa ni semi refined au double refined, basi alipie kwanza chaji ya asilimia 25 na kisha faini ifuate. Katika kutilia mkazo umuhimu wa afya za wananchi, Rais Magufuli alisema kuwa hataki kuona katika kipindi cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, watu wanalishwa mafuta yasiyofaa. “Sheria yetu ni mbovu sana, ambayo ni ya mwaka 2015. Nakuagiza Waziri wa Viwanda uipeleke sheria hiyo bungeni kwenye Bunge hili ili ifanyiwe marekebisho haraka. Haiwezekani mafuta ghafi yachajiwe chini kuliko semi refined na double refined oil.

“Nchi kama Malaysia, chaji ya mafuta ghafi ni kubwa sana kwa ajili ya kutoruhusu biashara hii ya mafuta ghafi, kwa hiyo nataka sheria hii ifanyiwe marekebisho haraka ili kulinda viwanda vya ndani,” aliagiza Rais Magufuli. Rais Magufuli aliinyoshea kidole Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa kusema kuwa wakati mwingine Bunge hupitisha sheria, lakini zikifika kwenye ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali maamuzi ya Bunge hubadilishwa kabla ya sheria husika kusainiwa.

Aidha, kutokana na kazi nzuri aliyoifanya Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa wa TRA, Usaje, Rais Magufuli aliigiza Wizara ya Fedha na Mipango kumpandisha cheo ili awe Kamishna kamili. Alisema agizo hilo litekelezwe ndani ya wiki, kwa kuwa Usaje amefanya kazi kubwa kwa ajili ya Watanzania na yenye maslahi kwa Taifa. Alizitaka idara za serikali ikiwemo Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Shirika la Viwango nchini (TBS), kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kutanguliza maslahi ya taifa. Alizitaka idara hizo, kutoa majibu halisi ya uchunguzi wao na siyo vinginevyo. “Kama uchunguzi unasema ni dawa za kulevya sema ni dawa za kulevya na siyo unga wa muhogo,” alisisitiza Rais Magufuli.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *