Home / Habari Za Kitaifa / Kodi mafuta ghafi kuongezwa

Kodi mafuta ghafi kuongezwa

SERIKALI imelieleza Bunge kuwa itaongeza kodi kwenye mafuta ghafi yanayoingizwa nchini kutoka asilimia 10 hadi 25.

Wizara ya Kilimo pia imewasilisha Wizara ya Fedha na Mipango mapendekezo ya kuboresha mfumo wa kodi na tozo kwa lengo la kuboresha mazingira ya uwekezaji na uendeshaji biashara kwenye shughuli za kilimo.

Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba amesema, kodi ya mafuta ghafi inaongezwa ili kuhamasisha uwekezaji katika mazao ya mafuta na kwamba, ongezeko hilo litatumika kuendeleza uzalishaji wa mbegu za mafuta.

Amewaeleza wabunge kuwa, uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta za alizeti, karanga, ufuta, mawese na soya umeongezeka kwa viwango tofauti.

“Kuongezeka kwa uzalishaji kumechangiwa na kuongezeka kwa hamasa kwa wakulima kutokana na uwepo wa soko la uhakika, ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi pamoja na uwekezaji katika viwanda vidogo na vya kati vya kusindika mazao hayo katika mikoa ya Manyara, Singida, Dodoma, Mbeya, Katavi, Lindi, Mtwara, Iringa, Njombe, Rukwa na Kigoma” amesema Waziri Tizeba bungeni.

Amesema, inalenga kuhamasisha uzalishaji alizeti kutoka tani 3,112,500 mwaka 2016/2017 hadi tani 9,337,500 ifikapo mwaka 2021/2022 sanjari na kuongeza tija kutoka tani 1.5 hadi tani 3 kwa hekta.

“Vilevile Wizara itahamasisha uzalishaji, usambazaji na matumizi ya mbegu bora hususan zinazotoa mafuta mengi na kuongeza upatikanaji wa pembejeo kwa wakati” alisema Dk. Tizeba.

Mfumo wa kodi na tozo

Waziri Tizeba amesema, mapendekezo yaliyowasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango yana lengo la kutoa unafuu wa kodi katika vifungashio vya mazao na mbegu za mazao ya kilimo, mabomba ya kunyunyizia dawa, mashine na mitambo ya usindikaji mazao, miundombinu ya uzalishaji na hifadhi za mazao ya bustani na kulinda wazalishaji wa ndani dhidi ya ushindani wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

“Mpango wa Wizara ni kuhakikisha kero zote zinazokwamisha maendeleo ya tasnia ya mazao ya kilimo zinashughulikiwa” amesema Dk. Tizeba.

Kwa mujibu wa Waziri Tizeba, katika mwaka 2018/2019 Wizara Kilimo itaendelea kuchambua na kubaini ada na tozo ambazo bado ni kero kwa wakulima nchini na itazifuta.

Amesema, lengo la kufanya hivyo ni kubakiza ada na tozo zenye mahusiano ya moja kwa moja na uendelezaji wa mazao husika ikiwa ni pamoja na kuendeleza utafiti wa mazao.

“Kwa msingi huo Wizara inapendekeza kufuta ada na tozo 21 ambazo kwa mwaka 2017/2018 zimeonekana ama kuwa kero kwa wakulima au vikwazo kwa maendeleo ya sekta ya kilimo. Ada na tozo zinazopendekezwa kufutwa ni tatu katika tasnia ya chai, tatu tasnia ya kahawa, mbili tasnia ya tumbaku na tozo moja moja kwa tasnia ya sukari na pamba. ” amesema Dk. Tizeba.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

wakulima tanzania

Wakulima Tanzania watafuta masuluhisho kwa changamoto zao

Wakulima nchini Tanzania wameonya kuwa huenda nchi hiyo ikaingia kwenye baa la njaa kutokana na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *