Home / Habari Za Kitaifa / Maandalizi mradi wa Stiegler’s Gorge yaiva

Maandalizi mradi wa Stiegler’s Gorge yaiva

ZABUNI ya uuzaji wa miti kwenye eneo ambalo litatumika kwa ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwenye maporomoko ya Mto Rufi ji ya Stiegler’s Gorge zimefunguliwa jana.

Kufunguliwa kwa zabuni hizo kunatokana na muda uliotangazwa wa kimataifa wa siku 21 kukamilika juzi tangu Aprili 25, mwaka huu. Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS), Profesa Dos Santos Silayo aliliambia HabariLeo katika mahojiano maalumu jana kuwa idadi na majina ya walioomba zabuni hiyo yatajulikana wakati wowote baaada ya kuzipitia na kuzichambua. Profesa Silayo alisema kuwa kufunguliwa kwa zabuni hizo ni hatua muhimu katika kutekeleza ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme unaotarajia kuanza Julai, mwaka huu.

Alisema kuwa eneo ambalo linapaswa kuondolewa miti ili kupisha mradi huo, limegawanyika katika vitalu (blocks) sita. Alisema kitalu kidogo kabisa kina ukubwa wa hekta 12,000. “Masharti ya msingi ni kwamba, miti hii itauzwa kwenye vitalu; na vitalu tulivyo navyo ni sita, hivyo eneo lote ambalo linapaswa kuondolewa miti lina ukubwa wa hekta 148, 000,” alieleza Profesa Silayo.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu huyo wa TFS, eneo hilo la hekta 148,000 ndilo litakalojaa maji lakini eneo litakalochimbwa bwawa lenyewe litakuwa na ukubwa wa hekta 200. Alisema kuwa ujenzi wa mradi huo unatarajia kuchukua miaka mitatu hadi kukamilika ingawa kazi za awali kama vile kujenga eneo la mdomo la bwawa linaweza kukamilika kwa muda wa miezi mitatu. Kutokana na umuhimu wa mradi huo, Profesa Silayo alisema kuwa washindi wa zabuni watatakiwa kuvuna miti yote ya biashara na isiyo ya biashara ili eneo libaki wazi kwa ajili ya shughuli za ujenzi wa mradi.

Ikumbukwe kwamba ujenzi wa mradi huo ni moja ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli katika kuimarisha miundombinu na upatikanaji wa nishati ya umeme nchini kwa ajili ya uchumi wa viwanda. Mara kadhaa, Rais Magufuli amekuwa akisisitiza azma ya serikali yake ya kutekeleza ujenzi wa mradi huo ambao utazalisha megawati 2,100.

Alipokuwa akizundua Kituo cha Kufua Umeme cha Kinyerezi II chenye uwezo wa kuzalisha megawati 240 Aprili 3, mwaka huu, Rais Magufuli alisema kuwa mahitaji ya umeme nchini kwa sasa ni megawati 1,400, lakini kwa kujumlisha na megawati zilizopo, uzalishaji umefikia megawati 1,513.3 ambayo aliyataja kuwa ni mafanikio makubwa. Alisema asilimia 60 ya Watanzania bado hawajaunganishwa kwenye nishati hiyo na badala yake wanaendelea kutumia kuni, mkaa na mafuta ya taa kwa kuwa bei ya umeme iko juu na wananchi wengi hawaimudu. Ili taifa lijitosheleze kwa nishati hiyo, Serikali imekuwa ikisisitiza mara kadhaa kuwa lengo lake ni kuzalisha megawati 5,000 za umeme ifikapo mwaka 2020 na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *