Home / Habari Za Kitaifa / Kinana- Si ajabu mimi kung’atuka

Kinana- Si ajabu mimi kung’atuka

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi Taifa (CCM), Dk John Magufuli, ameridhia ombi la Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahaman Kinana la kung’atuka katika nafasi hiyo.

Akizungumza katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) na Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, jana, Rais Magufuli alikiri kuwa amekuwa akipokea maombi ya kung’atuka kutoka kwa Kinana mara kwa mara na kuyakatalia.

“Huyu kweli ameshaomba zaidi ya mara mbili, na zile zingine alikuwa anaomba kisirisiri namkatalia, hata tukazungumza akiweka hilo, naanzisha mambo mengine, lakini nikatambua juhudi kubwa, kwa kujiuliza hivi ni makatibu wakuu wangapi, wamekuwa wa CCM tangu tupate uhuru,” alisema Dk Magufuli.

Alisema anafahamu kuwa walikuwepo makatibu wakuu wengine ambao hata yeye alikuwa bado hajaanza shule na kila mmoja alifanya kazi yake na kumaliza muda.

“Lakini nikatambua pia umri wa Kinana, nikamuita Dk Shein (Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Zanzibar) akaniambia kwa kweli tumkubalie, nikamuuliza na Mangula (Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara), akasema tukumkubalie, kuchoka kupo,” alieleza.

Alisema katika kikao hicho cha jana, aliamua kumuita Kinana kama Katibu Mkuu Taifa, akifikiri kuwa huenda akabadilisha mawazo lakini hali haikuwa hivyo.

“Nikamuambia bwana nataka nibadilishe uendelee, akakataa, sasa nimeridhika na nimejiridhisha kwa dhati ya moyo kwa kazi kubwa aliyofanya ndugu yetu, nimeridhia nimkubalie amalize muda wake wa ukatibu mkuu tutafute Katibu Mkuu mwingine,” alisisitiza Dk Magufuli.

Kinana alisema ni lazima jamii ikakubali kuwa kuna wakati wa kufanya kazi na wakati wa kupumzika.

“Naelewa ugumu mnaoupata, wa kutonikubalia, nakubali tu, najua nimepata massage nyingi zinauliza kama siwezi kubadili mawazo, tumekuwa na makatibu wengi tangu CCM izaliwe, tumekuwa na makatibu wakuu saba, hivyo si ajabu wa sasa naye aachie ngazi apatikane mwingine,” alisema.

Alimshukuru Dk Magufuli, Dk Shein na Mangula kwa kumkubalia ombi lake hilo la kuachia nafasi hiyo ya ukatibu mkuu wa CCM.

“Mara nyingi nakwenda kwa mzee Mangula kuzungumza, ni mmoja wa watu niliowatumia kumshawishi kwa sababu anazungumza na mwenyekiti wangu, nikimuomba anisaidie kushawishi. Nashukuru ulipoulizwa (Mangula) na mwenyekiti unasemaje ukawa upande wangu, japo mwenyekiti alikukasirikia kidogo. Nashukuru kwa kunielewa na kutambua kuwa kila lililo na mwanzo lina mwisho,” alisema.

Kinana alishika wadhifa huo wa ukatibu mkuu CCM tangu mwaka 2012 akichukua nafasi ya Wilson Mukama.

Wengine waliowahi kushika wadhifa huo ni pamoja na Pius Msekwa mwaka 1977 hadi 1980, Daudi Mwakawago mwaka 1980 hadi 1982, Rashid Kawawa mwaka 1982 hadi 1990, Horace Kolimba mwaka 1990 hadi 1994.

Wengine ni Lawrence Gama mwaka 1994 hadi 1996, Philip Mangula mwaka 1996 hadi 2006, Yusuf Makamba mwaka 2006 hadi 2011 na Wilson Mukama mwaka 2011 hadi 2012.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *