Home / Habari Za Kitaifa / RC aagiza mkandarasi akamatwe

RC aagiza mkandarasi akamatwe

MKUU wa Mkoa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo kumkamata mkandarasi aliyepewa kazi ya kujenga Kituo cha Afya cha Mima, wilayani Mpwapwa.

Mkandarasi huyo Kampuni ya Globe Pace East Africa Limited alipewa dhamana ya kujenga kituo hicho lakini imekitelekeza, hivyo kuisababishia Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa hasara ya Sh milioni 86.

Dk Mahenge ametoa agizo hilo wilayani Mpwapwa mkoa wa Dodoma kata ya Mima alipofanya ziara ya kikazi kukagua ujenzi wa kituo hicho.

Pia Dk Mahenge ameagiza kuundwa kwa tume na kuchunguza namna upatikanaji wa mkataba uliompa kazi mkandarasi huyo kama ulifuata utaratibu wa sheria ya manunuzi.

Alisema, serikali ilitoa Sh milioni 500 kwa ajili wa ujenzi wa kituo hicho, ambacho kilitegemewa kukamilika ujenzi wake Februari mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa alipowauliza wataalamu wa halmashauri hiyo akiwemo Mkurugenzi Mtendaji, Mganga Mkuu wa wilaya, Ofisa Manunuzi na Mhandisi wa Ujenzi juu ya upatikanaji wa mkandarasi huyo katika kutekeleza mradi huo, wote walikosa majibu ya kueleweka na hivyo ikamlazimu mkuu huyo wa mkoa kutafuta undani wa tatizo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa zahanati hiyo, Jenny Maswaga alisema, mradi huo ulianza kutekelezwa Oktoba 26 mwaka 2017 chini ya Mkandarasi wa Kampuni Glob Space East Afrika Limited, ambaye aliomba kulipwa Sh milioni 250 kama malipo ya awali kwa ajili ya ununuzi wa vifaa.

Maswaga amesema, baada ya mradi kufikia asilimia 30, mkandarasi aliondoka katika kituo cha kazi na kusababisha Kamati ya Ufundi ya Wilaya kuingia mkataba na mafundi wa kituo na kusimamiwa na wataalamu wa halmashauri.

Maswaga alisema mradi huo uliolenga kujenga majengo sita ambayo ni nyumba ya mtumishi, maabara, wodi ya watoto, wodi ya wazazi na chumba cha kuhifadhia maiti ambayo yalitakiwa kukamilika Juni 20, mwaka huu na hayajakamilika.

Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri amesema, kamati yake ya ulinzi na usalama tangu awali haikuridhishwa na mkandarasi huyo, hivyo waliwashauri wataalamu wa halmasahauri ya wilaya kujiridhisha na mkandarasi huyo kabla hawajampa kazi hiyo.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Dk Said Mawji amesema walipokea maelekezo kutoka Ofisi ya Rais na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuwa mkandarasi huyo ndiye atakayetekeleza mradi huo.

Pia Ofisa Ugavi na Manunuzi wa wilaya hiyo, Albert Anaclet amesema, baada ya kupokea maelekezo kutoka Tamisemi, walimtaka mkandarasi huyo kukidhi vigezo ili aweze kulipwa kiasi hicho cha fedha na mkandarasi huyo alitimiza masharti hayo ndipo alipoweza kujaza mkataba huo.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *