Home / Habari Za Kitaifa / CHINA YAMKABIDHI MAKONDA OFISI ZA WALIMU

CHINA YAMKABIDHI MAKONDA OFISI ZA WALIMU

paul makonda

UBALOZI wa China nchini umemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda majengo mawili kati ya matano ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono kampeni ya ujenzi wa ofisi za walimu.

Makonda alianzisha kampeni ya ujenzi wa ofisi za walimu Februari mwaka huu, baada ya kubaini uhaba wa ofisi za walimu 402 Dar es Salaam na ubalozi huo uliahidi kujenga ofisi tano za walimu, kila halmashauri ofisi moja.

Akizungumza wakati akipokea jengo la ofisi lililojengwa katika Shule ya Sekondari Makumbusho wilaya ya Kinondoni, Makonda ameushukuru ubalozi huo na kusema kuwa umekuwa wa kwanza kushiriki katika kampeni ya ujenzi wa ofisi hizo.

Makonda amesema wapo watu waliobeza kampeni hiyo na kusema haitekelezeki lakini mpaka sasa jumla ya ofisi 50 zipo katika hatua mbalimbali huku mbili za ubalozi huo zikiwa zimekamilika kwa asilimia 100.

“Watu walianza kusema huyu jamaa kiherehere hata serikali haijawaza kujenga yeye anajifanya anaweza tuone kama itajengwa hata ofisi moja, lakini leo zipo 50 kwenye hatua mbalimbali na mbili tayari zimekamilika kwa hiyo ni vyema wakatambua tunafanya kazi na zinatekelezeka,” amesema Makonda.

Alisema alifikia hatua ya kuanza kampeni hiyo kuweka mazingira mazuri kwa walimu na pia ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Walimu wasipokuwa na ofisi nzuri wanaolaumiwa ni CCM, kwenye ilani tuliahidi kutekeleza na kiongozi unayetambua huwezi kubweteka kusubiri serikali tumefanya juhudi za kutafuta wadau na leo tunaanza kuona matokeo,” amesema.

Alisema Rais John Magufuli alipotoa ahadi ya elimu bure alitaka kuondoa kero kwa wazazi kwa kuwa wengi wamekuwa wakihangaika kutafuta ada kwa ajili ya watoto wao.

Makonda amewataka walimu wa mkoa huo kuhakikisha wanajitoa kusaidia wanafunzi kufikia malengo yao.

Alisema kila kero za walimu zitashughulikiwa kwa kuwa ameshawaagiza maofisa elimu na wakuu wa shule kushughulikia stahiki zao.

Kwa upande wake Balozi wa China nchini alisema serikali yake imetoa dola za Marekani 90,000 kuhakikisha waliomo wanakuwa na mazingira bora na serikali itaendelea kuunga mkono jitihada mbalimbali za serikali ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na kuboresha sekta ya elimu.

Pia alisema ubalozi huo utaendelea kukamilisha ofisi tatu zilizobakia kama walivyoahidi kukamilisha idadi ya ofisi tano walizoahidi.

Alisema kwa kuwa Rais Magufuli alitoa ahadi nzuri ya kutoa elimu bure ni muhimu kwa wadau kushiriki.

Alisema wataendelea kushiriki na wamejenga shule mbili katika jiji la Dodoma na Dar es Salaam na wamesaidia kujenga maktaba ya kisasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *