Home / Habari Za Kitaifa / Wamkubali Magufuli

Wamkubali Magufuli

rais magufuli

Wasomi, wanasiasa, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida, wamezungumzia gawio la Sh bilioni 736.36 lililotolewa kwa serikali kupitia taasisi, kampuni, mashirika na wakala wake kwa mwaka wa 2017/18.

Juzi Rais John Magufuli alipokea mfano wa hundi za gawio la kiasi hicho cha fedha, licha ya kupongeza, aliagiza mashirika ambayo hayajatoa gawio, kufuatiliwa kwa undani ili kubainisha sababu za kushindwa kwao huko.

HabariLeo katika mahojiano yake na makundi mbalimbali ya watu kuhusu gawio hilo, wengi walipongeza na kushauri hatua zaidi zichukuliwe kusaidia ongezeko la gawio hilo.

Wasemavyo wasomi Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Profesa Honest Ngowi alibainisha kuwa kiasi hicho cha fedha kinaridhisha, ikilinganishwa na miaka ya nyuma, hatua inayoashiria kuwa gawio zaidi linaweza kupatikana.

Alisema kwa kuwa fedha iliyokusanywa itasaidia kuboresha sekta za afya, elimu, miundombinu na huduma nyingine za kijamii, ni dhahiri kuwa kuna haja ya kuongeza namna ya kuhakikisha zinapatikana fedha zaidi.

“Mashirika yamekuwa yakitoa gawio ila kwa mwaka huu naona kuna nyongeza kwa baadhi ya mashirika, fedha hizi zisaidie shughuli mbalimbali zitakazochagiza kukuza uchumi, ila pia ni wakati kwa zile kampuni, taasisi za serikali ambazo hazijachangia kujitahidi kufanya hivyo,” alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Benson Banna amesema, gawio lililopatikana mwaka huu linaashiria kuwa hapo awali fedha zilikuwa hazipelekwi zote na hakukuwa na mkakati madhubuti wa kuzikusanya.

Amesema gawio la mwaka huu linaashiria uwepo wa mikakati thabiti wa kuyabana mashirika katika utendaji wa kazi na kuhakikisha yanawasilisha mapato.

“Sio kwamba miaka ya nyuma hakukuwa na gawio, kulikuwa na utolewaji wa magawio haya, ila sasa kwa mwaka tumeshuhudia ongezeko, sasa ningependa kuisihi serikali kuendelea kubana zaidi ili gawio mwaka ujao liongezeke,” amesema.

Wafanyabiashara wanena

Nao wafanyabiashara waliozungumza na gazeti hili, walisema wameguswa na mchango huo wa sekta ya umma katika kukuza uchumi. Ally Mfuruki ni mmoja wa wafanyabiashara wakubwa nchini, ambaye alisema hatua hiyo ya sekta ya umma kuchangia gawio kubwa kama hilo, inatia moyo katika kusukuma gurudumu la maendeleo, tofauti na awali ambapo sekta binafsi ilikuwa ndio mchangiaji mkubwa. Alisema sekta ya umma ina mchango mkubwa na inahitaji mikakati itakayozaa matunda kwenye upatikanaji wake wa mapato. “Shilingi bilioni 736.36 si haba, ni kiasi kizuri tu na nina imani kuwa fedha zaidi zitaendelea kukusanywa na mwishowe sekta binafsi tunachangia kwa njia ya kodi na hiyo ya umma nayo inakuwa inaendelea kuchangia zaidi na zaidi,” alisema. Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Sembeye alisema kiasi hicho kinachangia kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nchi na alipongeza uwazi katika kutangaza gawio. “Sekta binafsi imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa pato la serikali kwa njia ya kodi na kwa mkakati wa kupata mapato kutokea sekta ya umma kama hivi, ni mzuri zaidi na hasa ikizingatia kuwa gawio linaongezeka,” alisema. Wasemavyo wananchi Mkazi wa Msasani, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Edward Mwaumbya aliliambia gazeti hili kuwa kwa muda mrefu amekuwa akisikia zaidi benki za National Microfinance Bank (NMB) na CRDB zikitoa gawio, lakini ilimfurahisha juzi aliposikia mashirika ya serikali kuwa yametoa gawio. “Jana (juzi) nilisikia TANAPA, TCRA, TPA, Sumatra na wengineo wakitoa gawio kwa serikali, hatua hiyo inaashiria kuwa serikali ya Magufuli inafuatilia utendaji wa ofisi zake na kuwa kama hii ikiendelea basi fedha zaidi zitapatikana,” alisema. Mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, Aisia Mkasi alisema ni dhahiri kuwa fedha hizo, zitaongeza utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi na alitaka zikasaidie zaidi sekta ya afya. Rais Magufuli akizungumza juzi baada ya kupokea hundi ya gawio hilo, alioneshwa kusikitishwa na baadhi ya kampuni kushindwa kutoa gawio kwa serikali. Alisema anashangaa kuna mashirika zaidi ya 90 yanayostahili kutoa gawio, lakini hayafanyi hivyo. Rais alisema gawio la Sh bilioni 736.36 lililotolewa ni kiasi kidogo, ikilinganishwa na uwekezaji uliofanywa na serikali wa Sh trilioni 49.05 uliofanywa na serikali. Kutokana na hali hiyo, alimwagiza Msajili wa Hazina, Athuman Mbuttuka kuhakikisha mashirika yanatoa gawio kwa serikali huku akitaka kwa yale yatakayoshindwa, yafutwe au uongozi kubadilishwa.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *