Home / Habari Za Kitaifa / Lugola: Nataka Mtambo au Bil 2/= NIDA

Lugola: Nataka Mtambo au Bil 2/= NIDA

Serikali imetoa wiki mbili kwa Kampuni ya Iris Corporation Berhard ya Malaysia, kurudisha Sh bilioni 32 zilizotolewa au kuleta mtambo wa kutengeneza kadi ghafi za Vitambulisho vya Taifa baada ya kushindwa kutekeleza jambo hilo kwa miaka mitatu sasa.

Pia kampuni saba zilizokuwa katika mradi wa vitambulisho vya taifa zimeitwa, kujieleza kutokana na tuhuma za kutumia Sh bilioni 28.5 ‘kifisadi’ sambamba na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dickson Mwaimu kutakiwa kufika kutoa maelezo yanayojitosheleza kwenye tuhuma za ufisadi wa Sh bilioni 32 kwa ajili ya ununuzi wa mtambo.

Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini hapa, na kueleza kuwa wamekutana na watendaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, akiwemo Kaimu Mkurugenzi Mkuu na viongozi waandamizi.

Alisema lengo lilikuwa ni kufanya kikao na Kampuni ya Iris Corporation Berhard ya Malaysia, ambapo hivi karibuni alifanya ukaguzi na kubaini Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa walilipa Sh bilioni 32 kwa kampuni ya Iris ili walete mtambo wa kutengeneza kadi ghafi ili kuongeza ufanisi wa kuongeza kasi ya utoaji vitambulisho.

Alisema licha ya fedha hizo kulipwa miaka mitatu iliyopita, lakini mpaka sasa mtambo huo haujaletwa.

“Niliagiza waje Dodoma wajieleze kwa nini mtambo huo haujaletwa, tumekubaliana tuwape wiki mbili bodi ikae waje na majibu kama wanarudisha fedha zetu au watuletee mtambo, tumekubaliana baada ya hapo tutaendelea na kinachofuata, hizi ni fedha za walipakodi ama zirudi au mtambo upatikane,” alisema Lugola.

“Sisi shida yetu ni mtambo, wakileta tutaupokea na wakiamua kuleta fedha itabidi tuzungumze wamekaa nazo miaka mitatu lazima penalti ipigwe dhidi yao,” alisema na kuongeza kuwa, Kampuni ya Iris iliwahi kuandika barua kwa NIDA wakidhani mtambo huo unatakiwa kuwepo Malaysia na utakuwa ukizalisha kadi na kuzileta nchini.

Pia alisema katika kikao hicho, wamepokea taarifa ya mamlaka ya PPRA katika kuchambua kwa kina katika mradi wa ununuzi wa mfumo wa usajili wa watu kwenye mradi wa Sh bilioni 180.

Alisema kwenye mradi kulikuwa na kampuni mbalimbali, zilizopata kazi na zipo kampuni zilizolipwa fedha kifisadi.

“Wale wote ambao wanajijua walihusika na ufisadi wa fedha za wananchi na fedha za umma, siku zao zinahesabika na wale wote waliojifanya ni wapiga dili wa fedha za umma hawatasalimika, wafanye maamuzi na wajisalimishe kwa kurudisha fedha ama sivyo hatua kali za kisheria zitawaandama,” alisema Lugola ambaye tangu ashike wadhifa huo Julai mosi, mwaka huu, amekuwa akiwasha moto kwa taasisi zilizo chini yake.

“Ninaanza na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa wasiwahusishe viongozi wa sasa, hawahusiki na yaliyofanywa na watangulizi wao,” alisema na kuongeza kuwa zipo kampuni zilizolipwa fedha kifisadi kwenye mradi wa vitambulisho vya taifa.

Alizitaja kampuni hizo ni Gotham International Limited inayodaiwa Sh bilioni 2.8, Iris Corporation Berhard Sh bilioni 22.9, Gwiholoto Impex Limited Sh milioni 946.4, Sykes Travel Agent Sh milioni 5.9, Dk Shija Paul Rimoy Sh milioni 27, Aste Insurance inayodaiwa Sh bilioni 1.2 na BMTL Sh milioni 569.1.

Alisema kampuni hizo zinadaiwa Sh bilioni 28.5. Alisema kampuni hizo zilitakiwa kufika Dodoma kujieleza Agosti 3, mwaka huu saa tatu asubuhi.

Alisema ni jambo la kushangaza kuona wakati serikali inajitahidi wananchi wapate vitambulisho vya Taifa, lakini kuna baadhi ya watu wanapiga dili.

Aidha, aliagiza aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Dickson Maimu afike Dodoma kujieleza sambamba na Jacky Gotham.

“Wafike ili watoe maelezo yanayojitosheleza hasa kwenye ule mtambo wa shilingi bilioni 32 inaonekana fedha imetolewa lakini mtambo haujaletwa,” alisema Lugola na kuagiza watu hao waandikiwe barua na hata kupigiwa simu na wasifanye jaribio lolote la kutofika siku hiyo.

Wakati alipotakiwa kutoa ufafanuzi na waandishi wa habari kwa namna gani kampuni hizo zilihusika kwenye ‘ufisadi’ huo, alisema Kampuni ya Iris walikuwa makandarasi na walihusika katika kuleta mtambo, Kampuni ya Gotham alikuwa mshauri mwelekezi na aliweza kulipwa fedha za dharura kwenye viwango ambavyo si sahihi.

Pia Aste Insurance magari yaliyohusika walilipwa malipo hewa ya bima, Kampuni ya Shija ililipwa malipo hewa ya kodi na Kampuni ya Skykes malipo hewa ya tiketi za ndege.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *