Home / Michezo / Kepa Arrizabalaga: Chelsea wamnunua kipa wa Athletic Bilbao kwa uhamisho uliovunja rekodi ya dunia

Kepa Arrizabalaga: Chelsea wamnunua kipa wa Athletic Bilbao kwa uhamisho uliovunja rekodi ya dunia

Chelsea wamevunja rekodi ya dunia katika ununuzi wa mlinda lango kwa kumnunua kipa Kepa Arrizabalaga kutoka klabu ya Athletic Bilbao ya Uhispania kwa £71m.

Mlinda lango huyo mwenye miaka 23 amenunuliwa kujaza nafasi ya Thibaut Courtois ambaye anakaribia kukamilisha uhamisho wake kutoka Stamford Bridge kwenda Real Madrid ya Uhispania.

Ada hiyo imezidi £66.8m ambazo Liverpool walilipa mwezi Julai kumchukua kipa wa Brazil Alisson.

Courtois, ambaye huchezea timu ya taifa ya Ubelgiji, alikosa kurejea mazoezini Jumattau huku tetesi zikimhusisha na kuhamia Real Madrid. Mchezaji huyo mwenye miaka 26 alikuwa ametarajiwa kujiunga na wenzake kwa mazoezi ya kuanza msimu Jumatatu lakini hakufika.

Jumatano, Chelsea walitoa taarifa kueleza kuwa wameafikiana na Real Madrid kuhusu uhamisho wa Mbelgiji huyo.

Kepa alikuwa amecheza mechi 53 La Liga akichezea Athletic Bilbao

Kepa ametia saini mkataba wa miaka saba katika klabu ya Chelsea.

Kepa kipa msaidizi wa De Gea

Kepa ni kipa nambari mbili katika timu ya taifa ya Uhispania, akiwa nyuma ya kipa wa Manchester United David de Gea, na amechezea timu ya taifa mechi moja pekee.

Alikuwa amekaa misimu miwili katika kikosi cha kwanza cha Bilbao na kuwalindia lango katika mechi 53 La Liga.

Chelsea wamevunja rekodi yao ya ununuzi wa mchezaji, kwani uhamisho wake umegharimu zaidi ya £60m walizolipa kumnunua mshambuliaji Mhispania Alvaro Morata kutoka Real Madrid Julai mwaka 2017.

“Kuna mambo mengi sana ambayo yamenivutia katika klabu hii – mataji ambayo wameshinda, wachezaji walio katika klabu hii, jiji lenyewe, na Ligi Kuu ya England,” amesema Kepa.

“Ni mambo mengi tu, na nina furaha kwamba Chelsea wameamua kuwa na imani nami na kunipokea.”

Courtois aliibuka kipa bora wa michuano ya Kombe la Dunia Urusi akichezea Ubelgiji

Januari, Kepa alitia saini mkataba mpya wa muda mrefu ambao ungemuweka katika klabu ya Athletic Bilbao hadi mwaka 2025, huku taarifa zikienea wakati huo kwamba alikuwa anatafutwa na Real Madrid.

Yeye ndiye mchezaji wa pili muhimu kuihama klabu hiyo baada ya Manchester City kumchukua beki Mfaransa Aymeric Laporte kwa £57m mwezi Januari.

Rekodi iliyodumu siku 20 pekee

Kabla ya Alisson kuhamia Liverpool kutoka Roma mwezi Julai, Gianluigi Buffon alikuwa ameshikilia rekodi ya kuwa kipa ghali zaidi duniani kwa miaka 17.

Buffon aomba msamaha kwa niaba ya Italia na kustaafu kimataifa

Kipa wa Brazil Alisson kuchukua mahala pake Loris Karius Liverpool

Mwitaliano huyo mwenye miaka 40 aliondoka Juventus majira ya sasa ya joto na kuhamia Paris St-Germain. Alikuwa ameweka rekodi ya euro 53m aliponunuliwa na Juve kutoka Parma mnamo 3 Julai 2001.

Rekodi yake ilidumu siku 6,225, lakini ya Alisson imevunjwa katika kipindi cha siku 20 pekee.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Nyota wa Afrika wamkumbuka mmiliki wa Leicester City Vichai Srivaddhanaprabha

Riyad Mahrez (kushoto) ni mmoja ya walitoa heshima zao kwa Vichai Srivaddhanaprabha Wachezaji wa Kiafrika …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *