Home / Habari Za Kitaifa / MKAPA ATAKA FIKRA MPYA, BIDII

MKAPA ATAKA FIKRA MPYA, BIDII

Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa amesema ili taifa liweze kupiga hatua kiuchumi, lazima watu wabadilishwe fikra zao wapende kufanya kazi kwa bidii.

Amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na serikali kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji huku akisisitiza watendaji kukamilisha maandalizi ya mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa wakati ili makundi haya yafanye shughuli zao bila kugombana.

Mkapa amesema hayo wakati akihutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza katika kilele cha Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane kwenye viwanja vya Nyakabindi, wilayani Bariadi katika Mkoa wa Simiyu.

Rais huyu mstaafu ambaye alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Rais John Magufuli kufunga maonesho hayo yaliyoanza tangu Agosti mosi, alisema maendeleo katika nchi hutegemea jinsi watu wanavyopenda kufanya kazi.

Akimshukuru Rais Magufuli kwa kumteua amwakilishe kufunga maonesho hayo, Mkapa ambaye aliongozana na mkewe, Mama Anna ametaka kila mtu kufanya kazi kwa bidii.

Akisisitiza umuhimu wa watu kupenda kazi, alisema serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato, kuhamasisha wananchi kulipa kodi, kubana matumizi yasiyo ya lazima na kujenga misingi kuelekea uchumi wa viwanda hususani vinavyotokana na sekta ya kilimo, uvuvi, mifugo na rasilimali nyingine.

Alisema kaulimbiu ya maonesho ya mwaka huu ya ‘Wekeza katika Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa Maendeleo ya Viwanda’, inatoa ujumbe muhimu na kukumbusha kuwa uchumi wa kati unaweza kufikiwa kwa kuongeza uwekezaji katika kilimo, mifugo na uvuvi.

Aliwafahamisha wananchi kuwa serikali imeondoa zuio la kuuza mazao nje ya nchi ikiwa ni namna mojawapo ya kuongeza soko la mazao ya wakulima nchini.

“Hata hivyo, yatauzwa kwa kufuata taratibu na kanuni za nchi,” alisema na kukumbusha wakulima kuhifadhi chakula cha kutosha wakati wa kuuza kujihakikishia usalama wa chakula katika kaya zao.

Vile vile alisema serikali inaendelea kuimarisha upatikanaji wa mbolea nchini na inao mkakati wa kuongeza uzalishaji pamba kutoka tani 121,000 hadi tani milioni moja ifikapo mwaka 2020 kwa kuongeza matumizi ya mbegu bora na kufuata kilimo bora cha pamba.

Alisema wizara kupitia Bodi ya Pamba itatakiwa kutenga maeneo maalumu ya kuzalisha mbegu bora kutimiza azma ya serikali ya kufanya zao la pamba lichangie ukuaji wa viwanda.

Akizungumzia maonesho hayo, Mkapa alisema idadi kubwa ya wananchi waliotembelea mabanda ni kielelezo tosha cha usimamizi makini wa viongozi waliopewa dhamana ya usimamizi.

“Katika kipindi changu cha uongozi, nilibahatika kutembelea nchi za kiafrika na hata kufungua sherehe kama hizi, sijawahi kukuta umati kama huu,” alisema. Alisema ameona jinsi wizara, taasisi, wakala, halmashauri na vikundi vya wajasiriamali vilivyojipanga kikamilifu kufanikisha maonesho na sherehe hizo zilizofana.

Alisisitiza: “Nimeona jitihada, endeleeni kutoa elimu ya kilimo bora na cha kisasa, ufugaji na uvuvi. Ni matumiani yangu kuwa maonesho yataendelea kuboreshwa kila mwaka yafikie kiwango cha kimataifa. Kiwanja hiki (Nyakabindi) kiendelee kutumika kama darasa la wakulima.”

Amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kikamilifu kubadili kilimo kiwe cha kisasa na ufugaji uwe wenye tija na endelevu kwa maendeleo ya taifa.

Amesisitiza kuwa kila mmoja akitimiza wajibu ipasavyo Tanzania ya viwanda itawezekana na nchi itasonga kuelekea uchumi wa kati.

Alisema ngao ya taifa ina vielelezo vya mkulima na mfanyakazi na wakati huo huo Chama Cha Mapinduzi (CCM) alama yake ni jembe (mkulima) na nyundo (mfanyakazi). Alisema katika nchi, sikukuu mbili zinazothibitisha msingi wa taifa ni Mei Mosi na Nanenane.

“Nimeshukuru kuona mshikamano na wingi uliojitokeza kuthibitisha kuwa Tanzania ni nchi ya wakulima na wafanyakazi,” amesema.

Mkapa ambaye alihitimisha hotuba yake kwa salamu ya ‘Magufuli oyeee’ huku akihoji hadhira ‘Nani kama Magufuli’, alimshukuru kwa kumuomba awe mgeni rasmi.

Alishukuru viongozi wa mikoa mitatu inayounda Kanda ya Ziwa Mashariki; Mara, Simiyu na Shinyanga na Katibu wa CCM, Dk Bashiru Ally kwa kuhudhuria sherehe hizo ambazo alisema zinapaswa ifike hatua mataifa ya jirani yaanze kuja kujifunza kutoka Simiyu.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa, mashirika ya kimataifa, mabalozi wa Msumbiji na Angola.

Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO), Dk Fred Kafeero aliipongeza serikali kwa kuboresha kilimo na akasema wadau wa maendeleo wataendelea kushirikiana na serikali kuhamasisha uwekezaji kwenye kilimo. “Kilimo kinalipa, kinaondoa umasikini, kinabadili uchumi wa nchi,” alisema.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *