Home / Habari Za Kitaifa / MAMA SALMA- WASIOSAJILI WATOTO WACHUKULIWE HATUA

MAMA SALMA- WASIOSAJILI WATOTO WACHUKULIWE HATUA

MKE wa Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Salma Kikwete ameitaka serikali kuchukua hatua kali kwa wazazi ama walezi ambao hawawasajili watoto wao ili wapate vyeti vya kuzaliwa, kwa kuwa wanawanyima haki yao ya msingi, na kuwasababishia matatizo siku zijazo.

Salma ametoa ushauri huo mwishoni mwa wiki, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu na Takwimu, yaliyoadhimishwa katika Shule ya Sekondari ya Wama Nakayama Kibiti mkoani Pwani.

Pia aliutaka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), kutumia njia mbalimbali kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi wote nchini, kwani watakapopata elimu ya kutosha watakuwa chachu ya kuleta mabadiliko.

“Natoa mwito kwa wananchi, hususan wazazi kutumia fursa hii adhimu ili kusajili watoto wote wanaozaliwa. Kutomsajili mtoto ni kumnyima haki yake na kuinyima serikali taarifa za mtoto wako.

“Wakati umefika sasa kuwataka wazazi ambao hawatumii fursa hii kujieleza na pale inapobidi kuchukuliwa hatua. Utambulisho wa watoto ni haki yake msiwanyime watoto haki hii,” amesema.

Amesema usajili wa matukio muhimu ya binadamu ni suala linalofanyika nchini kwetu kama ilivyo katika nchi zote duniani kwa lengo la kutaka kufahamu uhalisia wa taarifa za wananchi tulionao ili kupanga mipango bora ya kuwahudumia.

Alisema kuongezeka kwa muingiliano wa watu kutoka mataifa mbalimbali, kumefanya suala la utambuzi kuwa muhimu ili kuweza kubaini wale wanaostahili huduma mbalimbali katika kila nchi.

“Aidha mahitaji ya kuthibitisha umri ili kupata huduma mbalimbali za kijamii yameongezeka katika miaka ya karibuni mijini na vijijini.

“Huduma mbalimbali zinazolenga makundi maalumu kama vile watoto, vijana na hata wazee zinahitaji kuthibitisha umri wa anayehudumiwa,” alisema.

Alisema shule hiyo yenye watoto 337 ambao ni wa kike, wengi wao ni yatima na wanaotoka katika familia maskini.

Alisema kati ya idadi hiyo ya wanafunzi, ni wanafunzi 30 ambao wanalipiwa na wazazi wao, wengine wanafadhiliwa na taasisi yake ya Wama.

Mwenyekiti wa Bodi ya Rita, Profesa Hamis Dihenga amesema, kwa kiasi kikubwa, wamefanikiwa kusajili watoto chini ya miaka mitano, na sasa wanaangalia ni jinsi gani watasajili watoto kuanzia miaka mitano hadi 18 na wengineo.

Amesema Rita inataka kujipanga ili kipindi cha miaka miwili ijayo, wasiwe na malimbikizo ya kupata vyeti vya kuzaliwa.

Alisisitiza kuwa hivi sasa wana malimbikizo ya watu wenye umri mkubwa, kwani wengi wao hawana vyeti.

Katika maadhimisho hayo, Rita ilitoa vyeti 161 kwa wanafunzi wa shule hiyo, na vyeti vingine vitaendelea kupelekwa ili kuondoa usumbufu kwa wanafunzi hao ambao wengi wao hawana vyeti vya kuzaliwa.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *