Home / Habari Za Kitaifa / CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu mkoani Kigoma na wa udiwani kwenye kata 38 nchi nzima. Ushindi huo wa ubunge unamwezesha mgombea wake, Christopher Chiza kurejea bungeni.

Licha ya ushindi huo mkubwa, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amekiri chama chake kukumbana na ushindani mkali kwenye uchaguzi huo wa jimbo la Buyungu. Alisema, uchaguzi haukuwa mwepesi kwa kuwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Kasuku Bilago alikuwa amefanya mambo mazuri kwenye jimbo hilo, ambayo wapinzani wao kwenye uchaguzi walikuwa wakiyatumia kwenye kampeni zao. Alisema, CCM iliamua kuongeza na kuimarisha mbinu za ushindi katika kunadi sera zake kwa wananchi na kufanikiwa kuwavutia na mwisho wa siku wananchi hao walimpigia kura mgombea wa CCM.

Alisema, CCM ilifanya mikutano ya wazi, ya ndani na mikutano ya mtu mmoja mmoja huku ikiwatumia viongozi wake wakongwe katika kumnadi mgombea wake. Alisema, yeye mwenyewe alizizungukia kata zote za uchaguzi huku akitumia muda wake mwingi kwenye jimbo la Buyungu, ambapo alishiriki mikutano ya wazi, ya ndani na alifanya mkutano wa moja kwa moja na wananchi na kusikiliza hoja zao. Alisema, “CCM imejifunza mengi kwenye uchaguzi huu ule wa kata na ule wa jimbo, kuna maeneo ambayo hatukuwahi kushinda uchaguzi wa kata, ila kwa sasa tumeshinda na kuchukua kata hizo, hii haikuwa kazi ya kawaida”.

Aliongeza, “sio kwamba tumeshinda kwa asilimia 100 sasa ndio basi tumemaliza kazi, hapana, bado tunajipanga kuhakikisha kile tulichowaahidi wananchi hawa ndio tunakitekeleza ili waendelee kuwa na imani nasi zaidi”. Alisema, viongozi wa CCM wote waliokuwa kwenye kampeni hizo pamoja na yeye mwenyewe walikuwa na jukumu la kusikiliza maswali na hoja za wananchi, kisha kuzijibu na kujibu maswali hapo kwa hapo. Aliitaja Kata ya Lyoma iliyopo Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza kuwa kwa miaka 17 imekuwa chini ya Chama cha Wananchi(CUF), lakini kwenye uchaguzi huo CCM imeichukua kata hiyo.

Aliitaja kata nyingine ya Mivungano ambayo ni moja kati ya kata sita za jimbo la Monduli mkoani Arusha, ambayo yenyewe ilisimamisha mgombea, huku nyingine tano CCM ikipita bila ya kupingwa. Alisema katika kata hiyo, CCM imeshinda ingawa kulikuwa na ushindani mkali. Pia aliitaja kata ya Balai iliyopo wilaya Karatu mkoa wa Arusha, ambayo CCM kwa miaka 25 haikuwahi kushinda, lakini kwenye uchaguzi huo imeshinda. Alisema, “Buyungu pale ambapo mgombea wetu naye alikuwa mtu makini ametuletea ushindi wa asilimia 58, ameshindana na wa upinzani kwa kuwa yule wa upinzani alikuwa akitumia zaidi mafanikio ya Mbunge aliyepita ambae watu walikuwa wakimpenda sana”.

Alimzungumzia Mbunge wa mwanzo wa jimbo hilo, aliyefariki dunia kuwa wananchi walikuwa wakipenda kazi zake kwa kusema: ”Wapinzani wamemtumia huyu akiwa kaburini kudai kura, na kuna wakati niliwaambia kuwa sio vizuri kufanya hivyo, ila mnajua kwa kumtumia marehemu kwa mfano wa mambo mazuri sio tatizo kwa kuwa hata Mwalimu Nyerere tunamtumia kutangaza mazuri ila walimtumia sana kunadi sera zao lakini wananchi walituamini sisi zaidi,”alisema.

Dk Bashiru alitoa ushauri kwa wanasiasa wa upinzani, kuhakikisha kuwa wanakwenda kwenye majimbo yao wakati wa uchaguzi na kupiga kampeni na sio kufanya kampeni kwa njia ya mitandao ya kijamii. Pia Bashiru alituma salamu za rambirambi kwa wanazuoni wote wa hapa nchini na Afrika nzima kwa ujumla za kifo cha mwanazuoni na mwanamapinduzi wa masuala ya maendeleo, Profesa Samir Amiri wa Misri. Wakati huohuo, Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Buyungu, Lusubilo Mwakabibi, amemtangaza rasmi Chiza kuwa mbunge wa jimbo hilo baada ya kuwashinda wagombea wengine tisa wa vyama vya upinzani waliojitokeza.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, alisema Chiza amechaguliwa kuwa mbunge baada ya kupata kura 24,578 sawa na asilimia 58.7 ya kura 42,356 zilizopigwa na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Elia Frederick Michael alipata kura 16,910 sawa na asilimia 40.4 ya kura zilizopigwa. Mwakabibi alisema jumla ya kura zilizopigwa zilikuwa 42,356, kura halali zilikuwa 41,841 na kura 515 ziliharibika. Idadi ya wapiga kura ilipungua kwa kiasi kikubwa, ambapo watu 61,980 walitarajiwa kupiga kura kwa mujibu wa orodha ya wapiga kura katika daftari la mwaka 2015.

Msimamizi huyo wa uchaguzi akitangaza matokeo ya vyama vingine vilivyoshiriki katika uchaguzi huo, alisema kuwa mgombea wa Chama cha ACT-Wazalendo, Jonathan Misezero alipata kura 100, Salum Khamisi wa CUF kura 122, Philipo Fumbo – DP 22, Hamisi Kwezi wa Demokrasia Makini kura 11. Wengine ni Hamisi Kiswaga wa NRA kura 17, Kamana Mrenda wa UMD kura 12, Safari Mbeba wa UPDP kura 18 na Amina Mcheka wa AFP akiwa mwanamke pekee katika uchaguzi huo alipata kura 51 sawa na asilimia 0.12 ya kura zote.

Msimamizi wa uchaguzi alitangaza matokeo hayo saa 11:30 alfajiri katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya Kakonko, zilizopo kilometa tatu kutoka mjini Kakonko. Mgombea wa CHADEMA, Elia Frederick aliondoka eneo la kuhesabia kura kabla ya matokeo hayajakamilika kujumlishwa. Alisema kuwa hakubaliani na matokeo hayo, kwani hakutendewa haki, kwani baadhi ya fomu za matokeo alizonazo ni tofauti na fomu zilizobandikwa vituoni. Alidai kuwa kupitia mawakala wake waliokuwa wakimtumia matokeo kwa meseji, alijumlisha na kupata jumla ya kura 22,000 dhidi ya kura 18,000 za mgombea wa CCM.

Alisema aliamua kuondoa eneo la kutangaza matokeo kabla ya matokeo rasmi kutangazwa kwa sababu msimamizi wa uchaguzi, alishaamua kumtangaza Chiza kama mshindi. Kwa upande wake, Chiza alimshukuru Mungu kwa kufanikisha kuwa mbunge wa jimbo hilo. Alisema kwamba kazi kubwa aliyokuwa nayo sasa ni kuwatumikia wananchi wa jimbo la Buyungu katika utumishi uliotukuka. Alisema kuwa atasimamia ahadi zake, alizotoa kwenye kampeni lakini pia kufuatilia changamoto zlizojitokeza katika shida za wananchi ikiwemo matatizo ya maji, huduma za afya na mahitaji mengi ambayo yalijitokeza wakati wa mchakato wa kampeni.

Matokeo ya uchaguzi katika baadhi ya kata nchini ni kama ifuatavyo:- Mkoani Manyara katika kata ya Bagara jimbo la Babati Mjini, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Fortunatus Fwema alimtangaza mshindi wa kata hiyo kuwa Nicodemu Tlaghasi (CCM) aliyepata kura 2,708 sawa na asilimia 64, mgombea wa Chadema kura 1,455 asilimia 34 na mgombea wa UPDP kura 83 asilimia 2.

Katika Halmashauri ya wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Msimamizi wa uchaguzi huo, Denis Londo alimtangaza mgombea wa CCM, Jorvin Muya kuwa ndiye mshindi kwa kupata kura 1, 746, wakati mgombea wa Chadema alipata kura 383. Mkoani Mara katika Kata ya Turwa wilayani Tarime, Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi kata hiyo, Peter Julias alimtangaza mshindi wa kata hiyo kuwa ni Chacha Mwita (CCM) aliyepata kura 1,401, wakati mgombea wa Chadema alipata kura 1,121 na wa NCCR-Mageuzi 17.

Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Elias Mpanda alibainisha kuwa mkoani humo kati ya kata 20, CCM imeibuka kidedea bila mpinzani katika kata 13, huku ikishinda kwa kishindo katika kata saba zilizobaki. Katika Kata ya Kaloleni, mgombea wa CCM, Emmanuel Kessy alishinda na kutangazwa kuwa mshindi kwa kupata kura 947, wakati kura za wagombea wa vyama vingine ni Chadema kura 380, Demokrasia Makini kura 4 na NRA kura 3.

Katika kata ya Osunyai, mgombea wa CCM, Elirehema Nnko alitangazwa mshindi kwa kupata kura 3,227 huku Chadema kura 991, TLP kura 33, Demokrasia Makini kura 25, NRA kura 17 na NCCR Mageuzi 14. Kata ya Daraja Mbili, mgombea wa CCM, Prosper Msofe alishinda kwa kupata kura 3,497 wakati mgombea wa Chadema kura 944.

Katika kata ya Songoro, mgombea wa CCM, Charles Nnko alishinda kwa kupata kura 4,018 na wa Chadema kura 278. Mkoani Singida katika kata ya Unyambwa Jimbo la Singida Mjini, mgombea wa CCM, Abdulaziz Labu alishinda kwa kupata kuzoa kura 1,574 wakati mgombea wa Chadema kura136 na wa CUF kura 573. Mkoani Mtwara (CCM) katika kata ya Makonga Halmashauri ya Mji wa Newala, Msimamizi wa Uchaguzi, Andrew Mgaya alimtangaza mgombea wa CCM, Makungwa Juma kuwa mshindi kwa kupata kura 1,589 wakati mgombea wa CUF kura 822 na wa Chadema kura 104.

Katika kata ya Nanguruwe Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Mgaya alimtangaza Walla Elisha wa CCM kuwa mshindi kwa kupata kura 1,789 wakati mgombea wa Chadema kura 657. Kata ya Nalingu mkoani humo, mgombea wa CCM, Shaibu Mtavanga alitangazwa kuwa mshindi baada ya kupata kura 962 wakati mgombea wa CUF kura 841. Mkoani Songwe katika jimbo la Songwe, Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo la Songwe, alimtangaza Emilian Siwingwa wa CCM kuwa mshindi wa kiti cha udiwani katika Kata ya Mpona wilayani Songwe.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *