Home / Habari Za Kitaifa / TPDC YAANZA MCHAKATO UJENZI BOMBA LA GESI DAR-UGANDA

TPDC YAANZA MCHAKATO UJENZI BOMBA LA GESI DAR-UGANDA

WAKATI Tanzania na Uganda zikiweka mambo sawa katika ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda kwenda Tanga, Tanzania, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) nalo limeanza mchakato wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Dar es Salaam kwenda Uganda.

Imetangaza zabuni ya kumpata Mshauri Mwelekezi, hatua ambayo ni sehemu ya mikakati ya Tanzania kuhakikisha inafanya biashara ya gesi katika nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ikianza na Uganda. Uganda ilitangaza rasmi ushirikiano huo na Tanzania katika kuingiza gesi asilia kwa lengo la kupunguza gharama za utengenezaji wa bidhaa za chuma katika viwanda vyake.

Zabuni hiyo iliyotangazwa hivi karibuni, inatoa nafasi ya siku 30 kwa ajili ya kampuni mbalimbali zinazoweza kufanya kazi hizo kujitokeza kuomba kisha taratibu za kisheria kufuatwa. Katika tangazo hilo lililotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba, limeeleza kuwa Serikali imetenga fedha kupitia shirika hilo katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kazi hiyo.

Imeeleza kuwa mshauri mwelekezi ana kazi ya kufanya utafiti katika njia ya bomba hilo, kuangalia mahitaji ya gesi hiyo, wateja wa gesi asili na masoko kama uzalishaji umeme na viwanda. Pia kupendekeza na kutoa ushauri kuhusu fidia kwa maeneo litakakopita bomba hilo kwa mali, vifaa mbalimbali na makazi, njia mojawapo ya kupita bomba hilo kutoka Dar es Salaam mpaka Tanga kupitia Bagamoyo au Chalinze na masuala mengine yatakayowezesha ujenzi wa bomba hilo la gesi asilia.

Awali, Musomba alisema upembuzi huo utatoa taswira halisi ya jinsi mradi huo utakavyokuwa, biashara ikoje na kuona utekelezaji wake kama unawezekana au la, kutokana na kuwa kuna nchi nyingine za Afrika Mashariki zina gesi asilia pia. Alibainisha kuwa katika utekelezaji huo, pia utafanyika upembuzi yakinifu kuhuisha ule wa awali wa ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Dar es Salaam mpaka Tanga uliofanyika mwaka 2011 ili kuwezesha kwenda na wakati kuangalia uwezo wake kama bomba linaweza kudumu kwa muda gani.

Waziri wa Nishati nchini Uganda, Irene Muloni alithibitisha kuwapo kwa ushirikiano huo. Alisema Uganda inaihitaji sana gesi asilia ambayon itatumika katika viwanda vyake vya uzalishaji bidhaa za chuma. Aliiambia Kamati ya Bunge ya Rasilimali za Asili katika Bunge la Uganda kuwa mazungumzo na Tanzania, yanaendelea vyema ili hatimaye Uganda ianze kutumia gesi asilia kutoka nchi hiyo jirani.

“Kama tunavyojenga bomba la mafuta, tutajenga pia bomba la gesi asilia kutoka Tanzania mpaka Magharibi mwa Uganda, mpango ambao tunaamini utasaidia ujenzi wa viwanda vya chuma,“ alisema Muloni alisema Uganda ina zaidi ya tani milioni 300 za chuma katika maeneo mbalimbali hususan katika wilaya zilizopo magharibi mwa nchi hiyo za Kisoro na Kabale.

Hata hivyo, kwa sababu ya sekta ya chuma haiendelei kwani na wamekuwa wakitumia fedha nyingi kwa ajili ya kuingiza bidhaa zinazotokana na chuma kutoka China. Kwa mujibu wa utafiti wa Agosti mwaka 2015, Uganda ilitumia takribani Dola za Marekani milioni 280 (Sawa na Sh trillioni moja za Uganda) katika mwaka 2011 ili kuingiza bidhaa za chuma. Katika mwaka huo, serikali ilizuia kuuzwa nje ya nchi bidhaa za chuma ambazo hazikuwa zimechakatwa. Kiwanda cha Phosphates kilichopo Tororo, Mashariki mwa Uganda kinatarajiwa kutengeneza chuma kwa ajili ya rasilimali za kutengeneza bodi za magari.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *