Home / Habari Za Kitaifa / MAJALIWA ASISITIZA UZALENDO KWA VIONGOZI

MAJALIWA ASISITIZA UZALENDO KWA VIONGOZI

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka viongozi kuwa wazalendo na kuwakumbusha kutoathiri usalama wa Taifa wakati wanapotekeleza shughuli zao. Majaliwa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kozi fupi ya tano (Capstone 2018) katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi(NDC), inayowashirikisha viongozi kutoka taasisi mbalimbali za serikali.

“Chuo hiki kilianzishwa kwa lengo la kulisaidia Taifa kujenga uwezo wa viongozi ili wanaohitimu mafunzo wawe na uchambuzi wa kina na wa kimkakati ili kuweza kutatua mambo mbalimbali ya usalama wa Taifa na matatizo yanayotakiwa kushughulikiwa kimkakati,” alisema. Aliongeza kuwa, “Chuo hiki kilianzishwa ili kuwaleta washiriki kutoka taasisi zote za Serikali na sekta binafsi waweze kujadili mambo mbalimbali ya kimkakati ili wanapokuwa wanatekeleza wajibu wao watambue kuwa ni kwa kiasi gani matokeo ya maamuzi yao yataathiri mambo ya kijamii, kiuchumi, uhusiano wa kidiplomasia na siasa za ndani kwa ujumla wake”.

Alisema, ushirikiano kuhusu kutatua matatizo uanze wakati wa mafunzo hayo na uendelee hata hapo baadaye watakaporejea kwenye maeneo yao ya kazi na kuwataka washiriki kuhakikisha watakaporudi kwenye maeneo yao ya utendaji wawe wamebadilika kimtazamo, kihoja, kiushauri pamoja na utoaji maamuzi. “Sisi viongozi wenu tunatarajia kuona kuwa mtakapohitimu mafunzo haya mtakuwa mmebadilika kimtizamo na kwamba taasisi zenu zitakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuzungumza lugha moja”.

Majaliwa alisema, suala hilo ni muhimu katika kusukuma maendeleo ya nchi kwa haraka hususan wakati huu ambao Serikali inalenga kukuza uchumi wa viwanda na kuwataka viongozi hao kutambua kwamba changamoto za sasa ni mtambuka na hivyo, si rahisi kutatuliwa na taasisi moja moja. “Changamoto hizi zimebadili hali ya nchi yetu ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mazingira, ongezeko la watu, uhaba wa ajira, makosa ya kimtandao, ugaidi, na mengine mengi ambayo yote zinahitaji mikakati ya pamoja ili kuweza kukabiliana nayo” alisema.

Mkuu wa Chuo hicho, Luteni Jenerali Paul Massao alisema mafunzo hayo yatajikita katika mambo mbalimbali ikiwemo masuala ya menejimenti na kufanya maamuzi kuhusu masuala ya kitaifa kwa vitendo. Pia yatahusisha midhara na ufundishaji wa washiriki na itahusu kuwapa washiriki stadi na uelewa juu ya mkakati na stratejia kuu ya ulinzi wa Taifa na umuhimu wa uelewa na uamuzi wa pamoja wa vyombo vyote vya dola na Taifa na watendaji wake katika suala la ulinzi.

“Katika kipindi ambapo kuna mtizamo tofauti wa masuala ya usalama, kwa sasa msingi wa usalama ni kwa mtu binafsi na jamii, Taifa linajikita zaidi kuwa na viongozi wanaojali zaidi kulinda maslahi ya Taifa ndani na nje,” alisema. Alisema, kila janga la mtu binafsi kama njaa, magonjwa, kukosa kazi, mfumuko wa bei, rushwa na kupanda kwa gharama za maisha ni sababu zinazoweza kuondoa hali ya afya kisiasa, hivyo ukuaji wa uchumi, ajira na kutokomeza umaskini ni sababu ambazo huimarisha msimamo wa ndani wa kisiasa.

“Suala la mambo ya usalama wa Taia lisiachwe kama uwanja unaohusu sekta ya ulinzi pekee, kila mmoja wetu kwa nafasi yake tukijumuisha wasio wanausalama washiriki katika njia moja au nyingine kuhakikisha usalama wa Taifa kutokana na changamoto zinazojitokeza duniani katika karne hii ya 21,” alisema.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *