Home / Habari Za Kitaifa / WASIFU WA MTOTO ALIEPOKEA PhD KWA NIABA YA MAMA YAKE WABAINISHWA

WASIFU WA MTOTO ALIEPOKEA PhD KWA NIABA YA MAMA YAKE WABAINISHWA

TAMAR Mbogho (11) aliyepokea cheti cha Shahada ya Udaktari wa Falsafa (PhD) ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa niaba ya marehemu mama yake mzazi, Sophia Swai, imebainika kuwa kabla ya kwenda kuhudhuria mahafahali hayo ya mwishoni mwa wiki, alitaka kufahamu hatma ya cheti cha mama yake hata kabla ya maziko.

Mahafali hayo yaliyofanyika Novemba 25, mwaka huu Kampasi ya Solomon Mahlangu Mazimbu, ambako mbali na wahitimu wengine, wanafunzi 61 walifuzu na kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Falsafa ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.

Baba mzazi wa Tamar, Aaron Mbogho ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mwanga mkoa wa Kilimanjaro, alisema jana wakati akizungumza na gazeti hili, na kuweka bayana siri ya mwanawe huyo kwenda kupokea PhD ya mama yake.

Mbogho aliliambia gazeti hili kuwa mwanawe huyo alimuuliza swali kuwa, “hivi baba naruhusiwa kupokea cheti cha mama yangu huko chuoni?” Mkuu huyo wa Wilaya alisema kwamba kutokana na swali la mwanawe, aliamua kuufikia uongozi wa chuo na kutaka ufafanuzi ndipo ikaamuliwa aruhusiwe kwenda kuipokea hiyo PhD “posthumous degree’ ya marehemu mama yake.

Kwa mujibu wa Mbogho, mkewe Sophia Faustin Swai, alifariki dunia Mei 21, 2016, wakati huo akiwa ameshahitimu masomo yake kikamilifu na kwamba Tamar ni mtoto wa pekee wa marehemu.

Alisema Tamar alimaliza darasa la sita katika shule ya msingi Green Bird Academy ya Mwanga alikohamia muhula huu wa mwisho akitokea St Mary’s Mbeya alikosoma kuanzia darasa la awali hadi la sita na akiwa anaongoza wa kwanza darasani.

Kwa mujibu wa Mbogho, mtoto huyu alikuwa na mpango mkakati na mama yake aliyemwambia asome haraka ili kabla hajafikia miaka 25 awe na PhD yake.

“Ili kuitekeleza hiyo ndoto ya mama yake, Tamar hana mpango wa kusoma darasa la saba mwakani, bali ataenda kidato cha kwanza,” alisema Mbogho.

Alisema hiyo imewezekana baada ya kufanya mtihani Oktoba 1, 2016 katika Shule ya Sekondari St. Maria Goretti na kufaulu vizuri na kupata nafasi ya kujiunga na shule hiyo Januari, 2017.

Lengo ni ili amalize kidato cha nne akiwa na umri wa miaka 14, kidato cha sita akiwa na miaka 16, shahada ya kwanza akiwa na miaka 19, Shahada ya Uzamili akiwa na miaka 21 na ya Shahada ya Uzamivu (PhD) akiwa na umri wa miaka 24.

“Iwapo akirushwa tena madarasa asisome kidato cha tano na sita, basi ataipata PhD yake akiwa na miaka 22 tu ili kumuenzi mke wangu, nimejiandaa kugharimia shule yake aende haraka haraka,” alifafanua Mbogho.

Hata hivyo, Tamar anapenda asomee shahada zake nchini Australia au Marekani ambako alianzia shule ya awali alipokuwa na miaka mitatu na Mungu ampe uzima ili atimize ndoto zake.

SOURCE HABARILEO.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *