Home / Makala / LUNGU: MWANASHERIA ALIYELUNDIKWA VYEO KABLA YA KUWA RAIS

LUNGU: MWANASHERIA ALIYELUNDIKWA VYEO KABLA YA KUWA RAIS

AGOSTI 11 mwaka huu, Wazambia walipiga kura ili kumchagua rais pamoja na wabunge. Kama ilivyotazamiwa, mshindi wa uchaguzi huo alikuwa si mwingine bali ni Edgar Lungu mwenye umri wa miaka 60.

Kuibuka kwa Lungu kama rais wa sita wa Zambia, kunaanzia kwenye uchaguzi wa mwaka 2011 ambapo Chama cha Patriotic Front (PF), ambacho mgombea wake alikuwa Michael Sata (king cobra) kilichaguliwa na wananchi kuongoza Zambia huku kikipata viti 61 kati ya viti 150 vya bunge la Zambia.

Kutokana na kifo cha Sata kilichojiri Oktoba mwaka 2014, uchaguzi wa mapema ulifanyika Janauri 2015 ili kuchagua mtu mwingine ambaye angeshika nafasi yake katika kumalizia miaka mitano iliyokuwa imebaki kwa mujibu wa katiba ya Zambia. Ndipo jina la Lungu ambaye wakati wa utawala wa Sata alishika nafasi za Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Ulinzi na Sheria likachomoza na kuwa mgombea wa PF na kama ilivyotazmiwa akaibuka mshindi.

Katika uchaguzi huo wa mapema Lungu alimshinda mshindani wake mkubwa, Hakainde Hichilema (54) wa chama cha United Party for National Development (UPND). Katika uchaguzi huo, Lungu alipata asilimia 48.3 huku Hichilema akipata asilimia 46.7 na asilimia 5 wakigawana wagombea wengine.

Katika uchaguzi wa mwaka huu ushindani mkali ulikuwa tena baina ya Lungu wa PF aliyekuwa ameongoza Zambia kwa kipindi cha mwaka mmoja tu na nusu na Hichilema wa UPND huku aliyekuwa mgombea mwanamke pekee katika kinyang’anyiro hicho, Edith Nawakwi Zewelani wa chama cha Forum for Democracy and Development akishika nafasi ya tatu. Lungu alishiriki uchaguzi wa mwaka huu huku akipambana na upinzani mkubwa kufuatia uchumi wa nchi hiyo kuyumba kutokana na kuanguka kwa soko la shaba ambayo imekuwa uti wa mgongo wa Zambia.

Sehemu kubwa ya shaba ya Zambia imekuwa ikiuzwa China ambako inasemekana kiwango kilichokwishanunuliwa ni kikubwa na kutohitajika kwa wingi kwa sasa. Hata hivyo, mabadiliko ambayo amekuwa akiyafanya Lungu katika kuboresha katiba ya nchi hiyo, mambo ambayo yaliwashinda watangulizi wake huko nyuma, yalimpa chati Lungu na kufanikiwa kutetea kiti chake. Lungu alishinda urais wa mwezi Agosti kwa kupata kura 1,860,877, sawa na asilimia 50.35 ya kura zote dhidi Hichilema aliyepata kura 1,760,347sawa na silimia 47.63.

Lungu ni nani?

Mtu huyu, ofisa mwandamizi, mwanasheria, mtu muungwana na mwanasiasa, alizaliwa Novemba 11, mwaka 1956 katika hospitali ya Ndola iliyoko kwenye ukanda wa shaba. Mkewe ni Esther Lungu na wawili hao wana watoto sita. Alisoma masomo yake ya sekondari katika shule ya Mukuba kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Zambia ambapo alisoma sheria na kufuzu akiwa mmoja wa wanafunzi bora, Oktoba 17, 1981.

Baadaye alijiunga na Shule ya Sheria (ZIALE) na mwaka 1983 alipata cheti kinachomruhusu kufanya sheria nchini Zambia. Lungu alichelewa kukamilisha kozi yake katika chuo cha ZIALE hadi mwaka 1983 kwa sababu baada ya kutoka chuoni alijikuta akiwa na majukumu mengine kama mwanasheria katika Wizara ya Sheria, chama cha madini ya Shaba cha Zambia Consolidated Copper Mines (ZCCM) na benki ya Barclays.

Lungu pia alijiunga na kampuni ya wanasheria ya Andre Masiye iliyoko Lusaka, kisha alikwenda katika mafunzo ya kijeshi katika kambi Miltez iliyoko Kabwe ambayo ni sawa na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Tanzania (Zambia National Service).

Aliporejea kutoka mafunzo ya kijeshi akaendelea na shughuli za kisheria kabla ya kugeukia siasa. Safari yake ya kisiasa ilianza pale alipojiunga na chama cha United Party for National Development chini ya uongozi wa Anderson Mazoka, alikokaa kwa muda mfupi kabla ya kuhamia chama cha Patriotic Front (PF) kilichokuwa kinaongozwa na mwanzilishi wake, Michael Sata ambacho wakati huo hakikuwa na umaarufu mkubwa.

Katika uchaguzi wa mwaka 2001, aligombea ubunge wa jimbo la Chawama lakiki akakosa. Hata hivyo, aliendelea kubakia kama mjumbe wa Kamati Kuu ya PF na mwaka 2011, aligombea tena ubunge wa Chawama na safari hii alishinda. Katika kipindi cha ‘Acha watu waseme’ katika Radio Phoenix mara kwa mara Rais Sata alikaririwa akisema: “Asante sana mwanasheria wangu Edgar Lungu, na watu wengine walioniombea mazuri …” Lungu pia anakumbukwa kwa jinsi alivyosaidia familia za watu 30 ambao ni ndugu wa wachezaji wa timu ya taifa ya Zambia waliokufa katika ajali ya Aprili mwaka 1993 nchini Gabon kuweza kulipwa kifuta machozi cha Kwacha bilioni 16 na serikali.

Katika kesi hiyo iliyochukua miaka11, inaelezwa kwamba Lungu akiwa na mwanasheria mwenzake, Sakwiba Sikota walilazimika muda mwingi kutumia pesa zao za mfukoni ili kuona watu waliopoteza wapendwa wao waliokuwa katika safari ya kulitumikia taifa wanapata kifuta machozi. Kupanda kwa Lungu Lungu anaelezwa kama mwanasiasa aliyepanda haraka sana kwani Septemba 2011 baada ya Rais Sata kupata ushindi wa kihistoria alimteua Lungu kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Katika muda usiozidi mwaka, Rais Sata tena alimteua Lungu kuwa Waziri wa Ulinzi. Pamoja na majukumu haya, Lungu aliendelea kama kawaida yake kila siku kwenda nyumbani kutoka ofisi na baadaye kwenye jimbo lake, Chawama, ambako alifanya kila kitu kuanzia kutatua migogoro ya ardhi, ya ndoa na tofauti binafsi miongoni mwa wapiga kura wake. Kadhalika alisimamia ujenzi wa miradi ya barabara, afya, shughuli za polisi na kadhalika.

Katika kile kilichowashangaza wengi ni pale Rais Sata alipomuomba Lungu kuongoza nchi wakati yeye alipokuwa anakwenda China kuonana na rais mpya wa nchi hiyo wakati huo Xi Jinping, hali iliyoonesha kwamba alikuwa na imani kubwa na Lungu. Baadaye Lungu alipewa majukumu zaidi alipoteuliwa kuwa Waziri wa Sheria na Katibu Mkuu wa chama cha PF, mbali na kuendelea kuwa Waziri wa Ulinzi.

Inadhaniwa kwamba ni kutokana na kulundikiwa majukumu mengi kiasi hcho na kuonekana kuyamudu kilichofanya Kamati Kuu ya PF kuamini kwamba mtu huyu ndiye alikuwa mrithi ‘halali’ wa Rais Sata wakati habari zilipoenea kwamba amefariki dunia akiwa katika hospitali, London nchini Uingereza Oktoba 28, 2014 na siyo aliyekuwa Makamu wa Rais, Guy Scott.

Makala haya yameandikwa na Hamisi Kibari kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari.

SOURCE HABARI LEO.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Chakula cha Wahadzabe cha matunda na nungunungu Tanzania

Jamii ya Wahadzabe ni moja kati ya makabila yaliyobaki duniani yanayoendeleza shughuli za uwindaji, inadhaniwa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *