Home / Makala / KILIMO CHA MAHINDIKINAVYOKUZA UCHUMI WA RUVUMA.

KILIMO CHA MAHINDIKINAVYOKUZA UCHUMI WA RUVUMA.

MKOA wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa yenye fursa nyingi ambazo zinaweza kukuza uchumi wa mtu binafsi na taifa kwa haraka.

Asilimia 90 ya wakazi wa mkoa huo wanajishughulisha na kilimo. Zao la mahindi ni miongoni mwa mazao ambayo yanazalishwa kwa wingi huku changamoto kubwa ikiwa ni soko la mazao hayo. Takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2015 zinaonesha kuwa wastani wa pato la mtu mmoja (per capital income) katika mkoa wa Ruvuma ni Sh 2,415,486. Kulingana na takwimu hizo za NBS, mkoa wa Ruvuma unashika nafasi ya tatu katika uchumi.

Nafasi ya kwanza inashikwa na mkoa wa Dar es Salaam na kufuatiwa na mkoa wa Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dk Binilith Mahenge anasema mkoa wake unaendelea kupiga hatua kubwa katika ukuaji wa uchumi unaokwenda sanjari na uboreshaji wa maisha ya watu. “Nawatia moyo wananchi wa mkoa wa Ruvuma kutokana na kazi na ari ya kujituma, hasa katika kilimo ndiyo siri ya mafanikio ya ukuaji wa uchumi,’’ anasema Dk Mahenge.

Dk Mahenge anasema mkoa wa Ruvuma una fursa nyingi za kiuchumi ambazo zinaweza kuufanya mkoa huo kuongoza kiuchumi hapa nchini. Takwimu za uzalishaji katika sekta ya kilimo za mkoa wa Ruvuma katika msimu wa mwaka 2015/2016 zinaonesha kuwa uzalishaji halisi wa mazao ya chakula ulikuwa ni tani 1,955,424. Hata hivyo, mahitaji halisi ya chakula katika mkoa wa Ruvuma anasema ni wastani wa tani 469,172 ambapo mkoa una chakula cha ziada cha tani 1,486,252.

Zao la mahindi ndilo ambalo linategemewa kwa chakula na biashara na wananchi wa mkoa wa Ruvuma na kutokana na mkoa kuwa mmoja wa mikoa inayozalisha kwa wingi mahindi serikali iliingiza Ruvuma miongoni mwa mikoa minne ambayo ni magwiji katika uzalishaji wa mahindi (The big Four). Dk Mahenge anasema mkoa wake ni wazalishaji wakuu wa zao la mahindi, hali ambayo anasema inauwezesha kutoa ziada ya chakula ambacho kinatumika kunusuru maeneo yenye upungufu wa chakula.

Kwa mujibu wa Dk Mahenge, katika msimu wa mwaka 2015/2016 mkoa uliweza kuzalisha hekta 266,770 za mahindi na hadi kufikia Juni 2016 mahindi yaliovunwa yalikuwa kiasi cha tani 168,201 ukilinganisha na mavuno ya tani 689,123 zilizopatikana msimu wa mwaka 2014/2015.

Katika msimu wa mwaka 2016/2017, mkoa wa Ruvuma umedhamiria kulima jumla ya hekta 964,740 za mazao ya chakula na biashara zinazotarajiwa kutoa mavuno ya tani 2,424,985 ambapo kati ya hizo, mazao ya chakula ni hekta 774,080 zinatarajiwa kutoa mavuno ya tani 2,229,183 na mazao ya biashara ni hekta 190,660 zinazotarajia kutoa mavuno ya tani 195,802.

“Maandalizi ya kilimo yanaendelea, wakulima wameanza jitihada za kusafisha mashamba na maandalizi ya pembejeo za kilimo ambazo ni mbegu bora, mbolea ya kupandia na mbolea ya kukuzia,’’ anasema Dk Mahenge. Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa huyo, tayari Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imeleta waraka utakaotumika kutoa pembejeo za ruzuku katika msimu wa mwaka 2016/2017.

Hata hivyo, anaitaja changamoto kubwa katika suala la pembejeo zenye ruzuku ya serikali hasa mbegu ni msimu wa kilimo katika mkoa wa Ruvuma ambao huanza Novemba 15 ya kila mwaka lakini hadi sasa hakuna kampuni iliyokwishaingiza mbegu bora za ruzuku. “Mkoa unaendelea kufanya mawasiliano na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na kampuni ili kuhakikisha mbegu bora zinawafikia wakulima kwa wakati,’’ anasisitiza Dk Mahenge.

Anasema mkoa wa Ruvuma katika msimu wa mwaka 2016/2017 umepangiwa kupokea kiasi cha tani 2,456 za mbolea ya kupandia, mbolea ya kukuzia tani 2,456 na tani 491 za mbegu bora za mahindi. Ili kuhakikisha hakuna hujuma katika pembejeo za kilimo Dk Mahenge amewaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi katika halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma kusimamia zoezi la ugawaji na kuwachukulia hatua wote ambao watahujumu nia njema ya serikali kuwapatia ruzuku ya pembejeo wananchi wake.

Akizungumzia mfumo wa ununuzi wa zao la mahindi, Dk Mahenge anasema bado Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ndiye mnunuzi mkuu wa mahindi ambapo ameahidi serikali itaendelea kusimamia bei nzuri ya mazao yakiwemo mahindi. Waziri Mkuu, Majaliwa Kasim Majaliwa alipotembelea kituo cha NFRA Kanda ya Songea aliwaagiza kuacha kununua mahindi toka kwa wakulima kupitia mawakala badala yake waanzishe vituo vya kukusanyia na kununulia mahindi vijijini na kununua mahindi kwa wananchi kwa bei ambayo imeelekezwa na serikali.

Kulingana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma agizo la Waziri Mkuu limetekelezwa kikamilifu ambapo NFRA Kanda ya Songea ilianza ununuzi wa mazao ya chakula cha akiba katika mkoa wa Ruvuma Agosti 22, mwaka huu kwa kutumia vituo 26 vilivyopo vijijini. Anaitaja changamoto kubwa ambayo ilikuwepo katika vituo vya ununuzi wa mazao vijijini kuwa ni mwenendo usioridhisha wa wakulima katika baadhi ya vituo vya ununuzi kutopeleka mazao hali iliyosababisha NFRA kununua mahindi wastani wa tani 10,233 tu ukilinganisha na tani 22,000 zilizotarajiwa kununuliwa kimkoa.

Kutokana na ushindani uliopo sokoni katika zao la mahindi, serikali imetoa bei mpya ambapo NFRA baada ya bei kuridhiwa na serikali, kuanzia Novemba 7, 2016 ilitangaza bei mpya ya mahindi toka Sh 510 kwa kilo hadi kufikia Sh 580 kwa kilo kwa vituo vya vijijini.

NFRA pia imetangaza bei ya Sh 600 kwa kilo ya mahindi kwa watakaouzia katika Kituo Kikuu cha NFRA cha Ruhuwiko na kwamba utaratibu wa awali wa kupokea magunia kumi kwa kila mkulima umebadilishwa ambapo sasa wakulima wakubwa na wafanyabiashara wanaruhusiwa kuuza kiasi chochote cha mahindi walichonacho.

Nchini Tanzania, sekta ya kilimo bado ni muhimili wa maendeleo ya uchumi. Sekta hii inachangia kiasi cha nusu ya Pato la Taifa, robo tatu ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi na chanzo cha chakula na utoaji wa fursa za ajira zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania.

Kilimo kina uhusiano na sekta zisizo kuwa za kilimo kupitia uhusiano wa usafishaji kwenda kwenye usindikaji wa mazao ya kilimo, matumizi na uuzaji nchi za nje, kutoa malighafi kwa viwanda na soko kwa bidhaa zilizotengenezwa. Tanzania inazalisha takribani asilimia 97 ya mahitaji yake ya chakula. Uzalishaji wa mazao ya chakula unatofautiana mwaka hadi mwaka kutegemea na kiasi cha mvua kilichopatikana katika msimu huo.

source habari leo.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Chakula cha Wahadzabe cha matunda na nungunungu Tanzania

Jamii ya Wahadzabe ni moja kati ya makabila yaliyobaki duniani yanayoendeleza shughuli za uwindaji, inadhaniwa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *