Home / Habari Za Kitaifa / SAMIA AWAONYA WANAOWAZUNGUSHA WAWEKEZAJI.

SAMIA AWAONYA WANAOWAZUNGUSHA WAWEKEZAJI.

SERIKALI itawachukulia hatua kali watumishi wake wanaozungusha wawekezaji kiasi cha kuwafanya waondoke na kunyima fursa ya wananchi kupata maendeleo kwa kutumia rasilimali zilipo nchini.

Hayo yameelezwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan (pichani) kwenye maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu yaliyofanyika jana katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

“Tumeshuhudia kukimbiwa na wawekezaji kadhaa kwa sababu mwekezaji anakuja anataka kuwekeza Tanzania, miaka mitatu hajapata jawabu kama ndio wekeza au toka nenda zako, anazungushwa anapigwa taasisi moja kwenda nyingine, hili lifike mwisho,” alisema.

Samia alisema serikali itakuwa makini sana kusimamia suala hilo kwa nguvu, kutokana na kwamba kumekuwa na upotevu mkubwa wa uwezeshaji katika uchumi wa nchi.

Alitaja pia kuwa tatizo la rushwa kuwa moja ya sababu inayowakimbiza baadhi ya wawekezaji wenye nia ya kuja kuwekeza nchini na kwamba wekezaji wanaotajwa kukimbia kuwekeza nchini wengi wao ni wanaogoma kutoa rushwa ili kupata majibu ya kama wanaruhusiwa au hawaruhusiwi kuwekeza na hufanya hivyo wanapotakiwa kuhonga.

Samia alisema azma ya serikali ya kufikia uchumi wa viwanda mwaka 2025 kwa kutumia rasilimali za ndani itawezekana kama watumishi waliokabidhiwa dhamana ya kukusanya mapato na kusimamia matumizi ya fedha za Serikali watazingatia maadili ya utendaji kazi na kuweka mbele maslahi ya umma.

“Viongozi wa Umma wasimamie vema watumishi walio chini yao, kuna mtindo katika baadhi ya ofisi za Serikali kufanya kazi zao bila kufuata taratibu zilizoainishwa kwenye mikataba ya huduma kwa wateja…hili ni tatizo kubwa ndani ya Serikali yetu,” alisema.

Aidha, alisema pamoja na changamoto mbalimbali lakini watu wanatakiwa kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho Serikali iko katika hatua za kuleta mabadiliko ili nchi ielekee kule inapotakiwa ielekee na kwamba kunapofanyika mabadiliko lazima maumivu yatatokea.

“…kuna watakaorekebishwa, watakaotumbuliwa na watakaochukuliwa hatua mbalimbali, naomba tujue hii ni hatua ya mpito, tukielekea tunakokutaka taifa letu likikaa kwenye mstari maumivu haya yatakuwa yamekwisha, tuvumilie mabadiliko haya karibu tutafika tunakotaka,” alisema.

Katika hatua nyingine, aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) kufuatilia kwa karibu miradi ya Serikali wakati miradi hiyo inaendelea badala ya kusubiri hadi imalizike jambo ambalo limekuwa likisababisha upotevu wa fedha za umma.

Awali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki alisema, Serikali ilifikia uamuzi wa kuunganisha taasisi hizo kuadhimisha siku ya Maadili na Haki za Binadamu ili kupunguza gharama lakini pia kwa kuwa maadili na haki za binadamu vinashabihiana.

Akizungumzia Mkakati wa Taifa dhidi ya Mapambano ya Rushwa na Mpango wa Utekelezaji wa Awamu ya Tatu (NASCAP III), Waziri Kairuki alisema, umedhamiria kupunguza rushwa katika nyanja zote kwa kufuatilia kwa karibu mambo mbalimbali ikiwemo kuweka kipaumbele kwa sekta na maeneo yenye mazingira shawishi kwa rushwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maadhimisho hayo na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Valentino Mlowola alisema, maadhimisho hayo yanaikumbusha jamii kuwa chachu ya maadili katika uwajibikaji ili kuchochea kasi ya maendeleo. Alisema mpango huo utasaidia kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya rushwa na hivyo kuwahakikishia wananchi huduma bora.

“Ikilinganishwa na mpango mkakati iliyopita wa kwanza na wa pili, kwenye huu tumekuja na maboresho zaidi na tunaona tutashinda hii vita,” alisema.

Alisema azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kutatua kero za wananchi na kuhakikisha wanapata huduma bora. Taasisi zilizoshiriki maadhimisho hayo ni Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, TAKUKURU, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Tume ya Utumishi wa Umma na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA).

SOURCE HABARI LEO

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *