Home / Makala / ‘MITANDAO YA KIJAMII NI AJIRA, ITUMIKE KWA MANUFAA’

‘MITANDAO YA KIJAMII NI AJIRA, ITUMIKE KWA MANUFAA’

“NAKUMBUKA wakati tunaanza kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa kumchagua Rais wa Awamu ya Tano, CCM ilikuwa haitakiwi kwenye magazeti, radio na televisheni ikawa haipewi kipaumbele mtu mmoja ndio akaning’ata sikio kwamba ebu tafuta blogu ufanye nao kazi, kweli ilisaidia sana hadi tukafanikiwa kuchukua dola,” ni maneno ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alipokuwa akifunga mkutano wa wamiliki na waendeshaji wa blogu (TNB).

Bila shaka Waziri Nape ambaye kipindi hicho alikuwa anashika nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM alipitia ripoti ya takwimu za Mamlaka ya Kuratibu Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kuona idadi ya watumiaji wa intaneti kupitia simu za mikononi. Takwimu zilizotolewa TCRA zinaonesha matumizi ya intaneti nchini hadi Juni 2010 ni asilimia 99 ya wanakaya/mtu mmoja mmoja wapatao 483,204 ambao hawa wote ndio hujishughulisha na matumizi ya intaneti.

Ingawa mamlaka imesema hakuna tafiti zinazojishughulisha kueleza hasa matumizi ya intaneti yameisaidiaje Tanzania katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo, kiuhalisia, yapo manufaa. Ndiyo maana hata CCM waliona fursa na kuamua kutumia njia ya mtandao kufikia watu.

Vivyo hivyo kibiashara, kijamii na kiutamaduni, matumizi ya intaneti yana mchango wake. Ingawa zipo shuhuda za kuonesha athari za mitandao ya kijamii, lakini upande mwingine wa shilingi, imesaidia sana kufikisha ujumbe juu ya masuala ya elimu, biashara, kuburudisha na hata kuonya kulingana na mahitaji ya mhusika. Ili kudhibiti athari, ndiyo maana imetungwa na kupitishwa sheria ya mitandao iliyoanza kutumika Septemba, mosi, 2015.

Miongoni mwa mambo ambayo sheria inasisitiza, ni watumiaji kuepuka kusambaza ujumbe wa uchochezi ama ushawishi wa kisiasa unaoweza kuleta athari kwa jamii kupitia mitandao. Kuepuka kusambaza au kutunga ujumbe unaoleta uchochezi wa kidini unaoweza kusababisha kuvuruga amani na maelewano kwa jamii kupitia mitandao.

Mambo mengine ambayo sheria inakataza ni kusambaza picha ama video za utupu ama zilizokosa maadili kwa jamii kupitia mitandao mbalimbali, kusambaza picha ama video za uchochezi wa kidini ama kisiasa kupitia makundi mbalimbali ama mitandao ya kijamii. Pia sheria imehadharisha juu ya kutumia mtandao kwa utapeli kupitia ‘brand’ ama jina la mtu. Kwa ujumla, sheria hizi zinalenga kuhakikisha mitandao inaendelea kutumika kwa faida na si kwa hasara.

Kwa kuzingatia faida ya mitandao ya kijamii na hasa blogu, ndiyo maana Waziri Nape ameahidi kuwa serikali itaanzisha tuzo za umahiri kwa waandishi wa husika. Shindano linatarajiwa kuanza mwakani. Kwa mujibu wa Nape, lengo la tuzo hizo ni kusaidia blogu za Tanzania kubobea katika nyanja tofauti ikiwemo kilimo, mifugo, viwanda, hifadhi ya jamii kwa nia ya kuipa heshima tasnia ya habari nchini.

Anasema serikali imeanza mazungumzo na kampuni na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kudhamini tuzo hizo kuhakikisha kuwa washindi wanapatikana kwa uwazi. “Tuzo hizo zitakuwa za kwanza kwa namna zitakavyoendeshwa kwa uwazi hivyo makampuni zaidi yanakaribishwa kuweza kuzidhamini mashindano hayo yatakayojielekeza kwenye nyanja tofauti,” anasema Nape.

Katika mkutano huo wa TBN wenye kaulimbiu ‘Mitandao ya kijamii ni ajira, itumike kwa manufaa’, wamiliki na waendesha blogu wanahimizwa kutumia fursa ya mtandao wa kijamii kuijenga Tanzania, ikiwa ni pamoja na kuishauri na kuikosoa serikali. TBN yenye wanachama zaidi ya 100 ambao ni wamiliki na waendeshaji wa blogu Tanzania bara na Zanzibar, ilisajiliwa rasmi Aprili, 2015 kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani.

Katika ufunguzi wa mkutano wa wanablogu hao, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dk Hassan Abbas anawapongeza kwa kusema, chama kinaendana na malengo yake ya usajili. Anasema: Kuna vyama vimesajiliwa muda mrefu lakini hata kuwakutanisha wanachama havijawahi, kwenu hii ni hatua kubwa na mimi nitawapa ushirikiano wa kutosha pale mtakapohitaji. Mkurugenzi huyu wa Maelezo pia anaeleza namna anavyotambua na kuheshimu mchango wa blogu kama vyombo vingine vya habari.

Anaahidi kuwaandikia barua maofisa habari wote wa mikoa, wilaya na halmashauri ili kuwapa ushirikiano pale wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao. Mwenyekiti wa muda wa TBN, Joachim Mushi anaeleza kuridhishwa na ushirikiano wa serikali kupitia taasisi zake, ikiwemo TCRA katika kuwezesha chama kukamilisha mchakato wa usajili wake.

“Kimsingi, lazima tukubali kuwa mitandao hii imekuwa tegemeo kubwa la vyanzo vya habari na kusambaza taarifa mbalimbali tena kwa muda mfupi, hivyo kuna kila sababu ya kuendelea kuwanoa wanaoiendesha ili kupunguza matumizi mabaya ya mitandao hii,” anasema Mushi. Mushi anasema TBN inaamini njia pekee ya kupambana na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ni kuendelea kutoa elimu kwa waendeshaji na watumiaji ili mwisho wa siku wasikubali kutumika vibaya au kuitumia vibaya mitandao hii katika kutoa taarifa.

Kwa dunia ya sasa hakuna atakayepinga kuwa mitandao hii imekuwa ikielimisha umma, ikikosoa jamii na kiburudisha juu ya masuala anuai ya kijamii. Takwimu zinaonesha hadi Desemba 31, 2011, Afrika inakadiriwa ilikuwa na zaidi ya watumiaji milioni 139 wa mtandao wa intaneti kati ya raia wake wote bilioni moja wanaokadiriwa kuishi ndani ya bara hili ambalo ni la pili kwa kuwa na watu wengi duniani likilifuata bara la Asia ambalo linakadiriwa kuwa na watu wapatao bilioni 3.8.

SOURCE HABARI LEO

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Chakula cha Wahadzabe cha matunda na nungunungu Tanzania

Jamii ya Wahadzabe ni moja kati ya makabila yaliyobaki duniani yanayoendeleza shughuli za uwindaji, inadhaniwa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *