Home / Makala / SAMAKI WANAOTOA UMEME, CHANZO ADIMU CHA UTALII NCHINI.

SAMAKI WANAOTOA UMEME, CHANZO ADIMU CHA UTALII NCHINI.

TANZANIA ni miongoni mwa nchi zenye fursa za kipekee za kuchochea utalii wa ikolojia kupitia maziwa yake, hususani Tanganyika na Nyasa.

Maziwa hayo mawili yanatajwa kuwa na aina mbalimbali za samaki wa mapambo ambao baadhi yao wana sifa ya kutoa umeme. Ziwa Tanganyika lina urefu wa kilometa 673 na ni la pili duniani kwa kuwa na kina kirefu. Nafasi ya kwanza inachukuliwa na ziwa Baikar ambalo lipo katika nchi ya Urusi. Kina cha Ziwa Tanganyika ni kilometa 1.47 au meta 1470 na lina kilometa za ukubwa 18,900 na linachukua asilimia 17 ya maji yote baridi duniani.

Ziwa Tanganyika lina utajiri wa viumbe wa majini wa aina mbalimbali wakiwemo samaki, mamba, viboko na viumbe. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Samaki katika maziwa (TAFIRI) unaonesha kuwa ziwa Tanganyika lina aina za samaki zaidi ya 400 ambazo zimekuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi kwa watu wanaoishi mwambao mwa ziwa hilo. Kulingana na sensa ya samaki ya mwaka 1999 iliyofanyika katika ziwa Tanganyika inaonesha kuwa ziwa hilo linakadiriwa kuzalisha samaki kati ya tani 165,000 hadi 200,000 zenye thamani ya dola za Marekani milioni 80 hadi milioni 100.

Kwa upande wa Ziwa Nyasa, limezungukwa na nchi tatu ambazo ni Tanzania, Malawi na Msumbiji. Ziwa hilo lipo kwenye usawa wa meta 500 kutoka usawa wa bahari ambapo kina cha ziwa hilo ni karibu meta 750 na urefu wake ni karibu kilometa 1000. Kulingana na utafiti ambao ulifanywa katika ziwa hilo na Jumuiya ya Nchi zilizo kusini mwa Afrika (SADC) kwa kushirikiana na nchi ya Uingereza kati ya mwaka 1991 hadi 1994 na mwaka 1996 hadi 2000, ziwa hilo lina kiasi cha tani 165,000 za samaki.

Kati ya tani hizo za samaki, tani 35,000 za samaki ni jamii ya samaki wa maji ya juu ambao wanaweza kuvuliwa bila kuathiri uvuvi kila mwaka. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyasa, Oscar Mbyuzi anasema utafiti umebaini ziwa Nyasa lina aina 503 ya samaki wa mapambo ambao hawapatikani sehemu nyingine duniani. Hata hivyo kati ya aina hizo, kama ilivyo katika ziwa Tanganyika, kuna aina ya samaki adimu ambao wana uwezo wa kutoa umeme ambao pia ni samaki wa mapambo wanaofahamika kwa jina la electric fish.

Samaki huyu wa kipekee duniani akitangazwa kikamilifu katika vyombo vya habari na kufahamika ndani na nje ya nchi anaweza kuwa chanzo muhimu cha mapato hivyo kusaidia kukuza uchumi wa taifa. Mhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe ziwa Tanganyika Mkoa wa Kigoma, Noelia Mnyonga anawafahamu vyema samaki wanaotoa umeme waliopo katika ziwa Tanganyika na ziwa Nyasa.

Mnyonga anasema samaki hao ni kivutio adimu na cha kipekee duniani na kwamba wanaweza kuwa chanzo muhimu cha mapato kwenye sekta ya utalii ambayo ni miongoni mwa sekta zinazoongoza kwa kuchangia uchumi wa taifa. “Samaki wanaotoa umeme wakitangazwa kikamilifu ndani na nje ya nchi watalii wengi watamiminika hapa nchini ili kufika kuwaona samaki hao wa ajabu na taifa kupata fedha nyingi za kigeni,’’ anasema Mnyonga.

Anasisitiza kuwa watalii na wasomi wanaweza kufanya utafiti na kujifunza kwa nini samaki hao wanatoa umeme hivyo serikali kuongeza ajira kwa kuwa vijana watapata fursa ya kuwaongoza watalii kuona kivutio hicho Hata hivyo kwa mujibu wa mhifadhi huyo, umeme unaotolewa na samaki hao ni kwa ajili ya kujilinda na maadui katika ziwa na kwamba, samaki wanapowasogelea hutoa umeme ambao hauna madhara kwa binadamu.

Anasema utafiti unatakiwa kufanyika zaidi kuhusu samaki hao kuwa watalii na watafiti wengi wanapenda kujifunza maisha ya viumbe adimu vya nchi kavu na majini wakiwemo samaki hao wanaotoa umeme. Bila shaka watafiti wakipata fursa ya kufika katika maziwa haya mawili wangependa kufanya utafiti wa kina kufahamu idadi ya samaki hao na tabia yao ya kutoa umeme wanaposogelewa na adui.

Utafiti wa awali ambao ulifanywa katika ziwa Tanganyika na mwanasayansi, Erick Fortune kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins cha nchini Marekani, unaonesha kuwa samakiumeme wana uwezo wa kutoa umeme kwa kutumia ogani umeme iliyopo kwenye mikia ya samaki hao. Utafiti huo unaonesha kuwa samaki huyo anaweza kutumia umeme unaozalishwa mwilini mwake kwenye mawindo yake, hata hivyo umeme unaozalishwa na samaki huyo ni kidogo na hauwezi kuleta madhara makubwa.

Hata hivyo utafiti uliofanywa Februari mwaka huu na mtaalamu wa kimataifa, John Sullivan umebaini kuwepo kwa aina mbili za samaki umeme katika nchi ya Gabon. Sullivan anazitaja aina hizo mbili za samaki umeme ambazo amezigundua kwenye mto Ogooue uliopo katikati ya nchi ya Gabon kuwa ni Cryptomyrus jina lenye maana ya samaki aliyejificha na Ogoouensis jina lenye maana ya mto ambao samaki huyo ametoka.

Mtafiti huyo wa kimataifa anabainisha kuwa umeme unaotolewa na samaki umeme ni dhaifu na hauwezi kuleta madhara kwa binadamu na kwamba samaki hao wana seli nyeti juu ya ngozi zao ambazo zinawawezesha kutambua maadui na kuhisi hatari hivyo huzalisha umeme kukabiliana na maadui zao na kwamba hutumia umeme huo pia kwa mawasiliano na samaki wenzao.

Kulingana na Sullivan, tangu mwaka 1977 hadi sasa, kuna zaidi ya aina 200 za samaki umeme waliogundulika kwenye maji ya maziwa na mito katika Afrika. Ni wajibu wa serikali na wadau wengine wa utalii hususani Bodi ya Utalii Tanzania kuhakikisha kuwa samaki huyu adimu duniani anatangazwa kwa kasi ndani na nje ya nchi ili kuwavutia watalii na watafiti. Vikta Komba ambaye ni mkazi wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma anasema wengi hawajui kuhusu samaki umeme katika maziwa ya Tanzania.

Anaamini vyombo vya habari vikitangaza aina hii ya kivutio cha utalii wasomi na watalii wataingia kwa wingi. Idara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na viongozi wa serikali katika mikoa inayozunguka maziwa hayo wanatakiwa kuwahamasisha wananchi kutumia fursa hiyo ya utalii kuongeza kipato.

Wakazi wa maeneo hayo wanaweza kuanzisha utalii wa utamaduni ambao utawaongezea kipato maradufu kutoka kwa watalii ambao watafika kuona utalii wa ikolojia kwa kuwa watauza bidhaa za utalii wa kiutamaduni zikiwemo, ngoma za jadi, vifaa vya jadi na vyakula vya asili. Nchi imebahatika kuwa na maziwa mengi kuliko nchi yeyote katika Afrika.

Maziwa hayo ni Tanganyika, Victoria, Nyasa, Rukwa na mengine madogo. Yana rasilimali nyingi ambazo zinaweza kuiondoa nchi katika umaskini uliokithiri. Tanzania ilipigiwa kura na kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kwa kuwa na mazingira rafiki katika sekta ya utalii huku Afrika Kusini ikishika nafasi ya tano.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Habari la CNN la nchini Marekani unaonesha kuwa Tanzania inashika nafasi ya pili duniani, kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii huku nchi ya Afrika ya Kusini ikishika nafasi ya 14. Hata hivyo, kulingana na utafiti huo, Tanzania katika mapato na miundombinu yanayotokana na sekta ya utalii inashika nafasi ya 110 kati ya nchi 133 duniani.

SOURCE HABARI LEO

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Wabunge watwangana makonde Uganda

Wabunge nchini Uganda wamepigana ndani ya ukumbi wa bunge Wabunge nchini Uganda wamepigana ndani ya …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *