Home / Habari Za Kitaifa / KESI 4 ZAMKABILI MMILIKI WA JAMII FORUM.

KESI 4 ZAMKABILI MMILIKI WA JAMII FORUM.

MKURUGENZI na Mwanzilishi wa Kampuni ya Jamii Media Limited, Mexence Mubyazi (40) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na kesi tatu zenye mashitaka manne.

Alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa kesi hizo kwa mahakimu watatu tofauti. Hata hivyo, Mubyazi alikosa dhamana katika moja ya kesi hizo na kupelekwa katika Gereza la Keko.

Kesi hizo ziliendeshwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Mohammed Salum mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Thomas Simba, Victoria Nongwa na Godfrey Mwampamba kwa mashitaka ya kuzuia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na kuendesha mtandao kwa usajili usio wa Tanzania.

Katika kesi namba 456 ambayo ilikuwa kwa Hakimu Simba, Salum alidai kuwa kati ya Aprili Mosi mwaka huu na Desemba 13, mwaka huu maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni, mshitakiwa akiwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo inayoendesha tovuti ya Jamii Forum, alishindwa kutoa taarifa kuhusu miliki hiyo huku akijua kwamba jeshi hilo linafanya uchunguzi wa makosa ya jinai yaliyochapishwa kielektroniki kwenye tovuti hiyo.

Salum alidai kuwa kitendo hicho ni kinyume na Kifungu namba 22 (2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao Namba 14 ya mwaka 2015. Wakili wa utetezi wa mshitakiwa, Jebra Kambole alikana mashitaka hayo na kuomba Mahakama itoe dhamana kwa mshitakiwa, ambapo aliachiwa kwa dhamana baada ya Hakimu Simba kutaja masharti hayo kuwa na wadhamini wawili, watakaosaini bondi ya Sh milioni 10.

Katika kesi namba 457 iliyokuwa mbele ya Hakimu Nongwa, pia mshitakiwa alidaiwa kuzuia jeshi hilo kufanya uchunguzi kinyume na Sheria Namba 22 (2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandano Namba 14 ya mwaka 2015.

Salum alidai kuwa kati ya Mei 10 mwaka huu na Desemba 13 mwaka huu maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni, akiwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, alilizuia jeshi hilo kufanya uchunguzi kwa kushindwa kutoa taarifa zilizochapishwa na tovuti hiyo.

Wakili wa utetezi, Kambole alikana mashitaka hayo na kuomba mahakama itoe dhamana, ambapo Hakimu Nongwa alisema mshitakiwa atatakiwa kuwa na wadhamini wawili, watakaosaini bondi ya Sh milioni moja.

Aidha, katika kesi ya tatu ambayo ilikuwa mbele ya Hakimu Mwampamba, mshitakiwa alikabiliwa na mashitaka mawili ikiwemo la kusendesha mtandao kwa usajili usio wa Tanzania na kuzuia jeshi kufanya uchunguzi.

Wakili Salum alidai kuwa, kati ya Desemba 9, 2011 na Desemba 13 mwaka huu, maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni, akiwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo, aliendesha mtandao wa jamiiforum.com bila usajili wa Tanzania kwa kutumia Tanzania Country Code Top Level Domain (ccTLD) ambayo ni do-tz.

Alidai alifungua kampuni hiyo kwa Sheria ya Makampuni Namba 212 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kutumia cheti namba 66333.

Alidaiwa katika mashitaka ya pili, kati ya Januari 26 mwaka huu na Desemba 13 mwaka huu, maeneo ya Mikocheni akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media inayoendesha mtandao wa jamiiforums huku akijua kwamba jeshi la polisi linafanya uchunguzi wa makosa ya jinai, yaliyochapishwa kwenye mtanao huo, alizuia jeshi hilo kwa kushindwa kutoa taarifa.

SOURCE HABARI LEO

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *