Home / Habari Za Kitaifa / WAZIRI: WAPIGA ‘DILI’ MTAJUTA.

WAZIRI: WAPIGA ‘DILI’ MTAJUTA.

WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge amewatahadharisha watumishi wa idara zilizo katika wizara hiyo na makandarasi wanaojenga miradi ya maji waliozoea kupiga ‘dili’. Lwenge amewaonya kuwa, wasijaribu, na wakithubutu watajuta maisha yao yote.

Lwenge ametoa tahadhari hiyo kwa nyakati tofauti alipokuwa akikagua ujenzi wa upanuzi wa chanzo cha maji cha Mfili na kuzungumza na watumishi wa sekta ya maji wilayani Nkasi.

Ametoa tahadhari kama hiyo baada ya kukagua ujenzi wa majengo ya ofisi za utawala na maabara ya maji, ofisi ndogo ya Bonde la Ziwa Rukwa yanayojengwa mjini Sumbawanga. Pia alizungumza na watumishi wa sekta ya maji na wakandarasi wanaojenga miradi ya maji mjini humo.

“Niwahakikishie kama ulishindwa ‘kula’ au kupiga ‘dili’ huko nyuma sasa huwezi tena, Serikali hii ya Awamu ya Tano imeziba mianya hiyo sasa ili ubaki salama usijaribu kucheza michezo hiyo utajuta,” alisisitiza.

Aidha alionya kuwa hatasita kuchimbua ‘makaburi’ na kuwachukulia hatua watakaoshindwa kuendana na ‘mwendo kasi’ wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo bila ya kumwonea yeyote.

Akiwa ziarani wilayani Nkasi, Waziri Lwenge amesema atatuma timu ya wataalamu kutoka wizarani ambao wataungana na wahandisi kutoka mkoa wa Rukwa, watakagua mradi wa upanuzi wa bwawa la maji la Mfili ambao unalalamikiwa kujengwa chini ya kiwango.

Amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Tixon Zunda aandike tuhuma zinazomkabili Meneja wa Mamlaka ya Maji Mjini Namanyere (Nuwasa) Charles Mwakasege na taarifa hiyo iwasilishwe kwake afanye uamuzi.

Waziri Lwenge pia ameagiza kuwa shughuli za Nuwasa zitasimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi hadi utakapotolewa uamuzi mwingine kwa kuwa mamlaka hiyo (Nuwasa) haina watumishi wenye ujuzi wa kuiendesha.

Pia ameagiza mkandarasi Felix Lyoya, aliyekuwa akijenga mradi wa maji katika kijiji cha King’ombe wilayani Nkasi atafutwe popote alipo, akamatwe na afikishwe katika vyombo vya dola. Mkandarasi huyo kutoka kampuni ya Fully Enterprises Ltd anadaiwa kushindwa kukamilisha ujenzi wa mradi huo na ‘kuingia mitini’.

Awali Katibu Tawala wa mkoa wa Rukwa, Tixon Zunda alimwomba Waziri Lwenge aondoke na Meneja wa Nuwasa, Mwakasege kwa kuwa ameshindwa kwa uzembe wake kusimamia upanuzi wa ujenzi wa bwawa la maji la Mfili na kujengwa chini ya kiwango.

Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Saidi Mtanda alimwomba Waziri Lwenge avunje Nuwasa kwa kuwa imeshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo na shughuli zake zifanywe na Idara ya Maji.

Mtanda pia alimwomba Waziri Lwenge atumie wataalamu wa kukagua matumizi ya fedha zaidi ya Sh milioni 300 zilizotumwa na wizara kwa Nuwasa kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya maji.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Julius Kaondo alimweleza Waziri Lwenge kuwa Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ziliidhinisha zaidi ya Sh bilioni moja kwa ajili ya upanuzi wa bwawa la maji Mfili.

SOURCE HABARI LEO.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *