Home / Habari Za Kitaifa / MUHONGO AITAKA TANESCO KUHAMIA KISIWANI KOME.

MUHONGO AITAKA TANESCO KUHAMIA KISIWANI KOME.

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha wanakuwa na ofisi kwenye Kisiwa cha Kome wilayani Sengerema chenye kata nne zenye vijiji 16 .

Agizo hilo alilitoa alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II) kisiwani humo.

Alisema wananchi wa kisiwa cha Kome hawapaswi kusumbuka kuvuka maji kufuata huduma kwenye ofisi za Tanesco ambazo ziko mbali.

Naye mwakilishi wa mkandarasi ambaye ni kampuni ya Chico CCC inayotekeleza mradi huo, Meck Nziku alisema umeme uliosambazwa kisiwani humo ni kutoka katika kijiji cha Nyakalilo kwa kutumia nyaya zinazopita chini ya maji. Aliongeza kuwa gharama zilizotumika kupitisha umeme huo chini ya maji ni Sh milioni 200.

Akizungumzia suala la uunganishwaji wa umeme kisiwani humo, Nziku alisema mradi huo ulilenga kuwaunganishia wananchi 718, lakini waliojitokeza kuunganishwa ni 579.

Kufuatia maelezo hayo, Waziri Muhongo aliwasisitiza wananchi kisiwani humo kuchangamkia mradi huo ikizingatiwa gharama ya kuunganishwa ni ndogo ambayo ni sh 27,000 sawa na bei ya majogoo wawili.

Alisema ili kuwa na maendeleo endelevu katika sekta mbalimbali za uchumi kisiwani humo ikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji ni lazima kutumia umeme ili kuwa na tija.

Aidha, Waziri Muhongo alizungumza na wananchi na kuelezwa kero mbalimbali kuhusu suala la umeme ikiwemo vitendo vya kuombwa rushwa na mafundi wa mkandarasi ili waunganishiwe huduma.

Kufuatia malalamiko hayo, Waziri Muhongo alisema ni marufuku kwa mafundi hao kuomba fedha, kwani wao hawahusiki na suala la malipo. Aliongeza kuwa mkandarasi yoyote nchini ambaye mafundi wake watabainika kujihusisha na vitendo vya rushwa hatapewa miradi mingine.

Aliiagiza ofisi ya Tanesco mkoa wa Mwanza kukutana na wananchi hao kesho kwa ajili ya mafunzo na pia kuchukua orodha ya wananchi wenye nia ya kuunganishwa na huduma.

“Hawa wataalamu wa Tanesco watakaofika hapa kesho, watakaa nanyi kwa wiki nzima wakishughulikia kero mbalimbali zinazowatatiza,” alisema huku akisisitiza ni marufuku kwa mkandarasi kukusanya fedha kwa wananchi.

SOURCE HABARI LEO

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *