Home / Habari Za Kitaifa / KILIO CHA DAWA YA YA USINGIZI BOMBO CHAPELEKWA KWA MAGUFULI.

KILIO CHA DAWA YA YA USINGIZI BOMBO CHAPELEKWA KWA MAGUFULI.

BAADHI ya wananchi wenye wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga ya Bombo, wamemuomba Rais John Magufuli kuingilia kati, kumaliza kadhia inayowapata ndugu zao.

Ndugu hao ni wanaokosa matibabu ya upasuaji kwa siku ya nne sasa, kutokana na ukosefu wa dawa ya usingizi.

Wametoa ombi hilo walipozungumza kwa nyakati tofauti jana nje ya hospitali hiyo. Walidai kwamba bado wanashangazwa na kitendo cha uongozi wa hospitali, kushindwa kutoa taarifa rasmi kuhusu ni lini huduma hiyo itarejea tena.

Juma Selemani mkazi wa Msambweni jijini Tanga, katika mahojiano hayo, alidai kwamba mke wake ambaye ni mjamzito wa miezi sita, alifikishwa hospitali hapo jana (juzi) na kulazwa wodini ili kupatiwa huduma hiyo, baada ya kubainika kwamba mtoto alifia tumboni siku kadhaa zilizopita.

“Nilifika hapa Bombo jana (juzi) kwa rufaa ya kutoka Kituo cha Afya Ngamiani baada ya kubaini mtoto aliyeko tumboni kwa mke wangu hachezi, hivyo madaktari hapa Bombo wakaagiza apigwe picha ya X-ray na ndipo wakamweleza kwamba mtoto amefariki, hivyo inalazimu alazwe ili kupatiwa huduma ya kutoa nje kiumbe hicho, “ alisema.

Aliongeza kuwa, “Tangu alivyopewa kitanda mpaka sasa, bado hajapatiwa matibabu zaidi ya kuwekewa dripu, kwa kweli napata hofu kuhusu hatma ya afya ya mke wangu kwa sababu tayari binafsi amepata wasiwasi baada ya madaktari kumthibitishia kwamba mtoto tumboni ameshakufa, hali aliyonayo sio nzuri binafsi naomba Rais Magufuli afanye jambo ili kuokoa wagonjwa hawa.”

Naye Rehema Mohamed aliyedai kufika hospitali hapo wiki moja iliyopita kwa rufaa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kilindi ili kumuuguza mama yake, alisema pamoja na kufanikiwa kununua dawa na vifaa vyote vinavyohitajika wakati wa upasuaji, bado hawajafanikiwa kutibiwa.

“Kwa kweli hatujui siku wala saa rasmi ambayo dawa hiyo itapatikana ili mama yangu aweze kufanyiwa upasuaji, kinachoendelea hapa ni kupewa matumaini tu, kwamba labda kesho au kesho kutwa, lakini hali sio nzuri kwa upande wangu kutokana na umuhimu wa tiba hiyo hasa kwa mzazi wangu huyu ambae ana umri zaidi ya miaka 85,” alisema.

Juhudi za gazeti hili za kuupata uongozi wa hospitali ya Bombo kuzungumzia ukosefu wa matibabu hayo, ziligonga ukuta baada ya walinzi watatu wa hospitali, kukataa na kisha kuweka ulinzi mkali getini dhihi ya waandishi wa habari watano kuingia eneo hilo.

Walinzi hao walidai kwamba uongozi haukufurahishwa na kitendo cha wao kuripoti habari hiyo jana (leo). Waandishi hao ambao ni kutoka Habari- Leo, Mtanzania, Televisheni ya Taifa (TBC1), Clouds Media na Redio ya Tanga Kunani (TK FM) walifika hospitalini hapo majira ya saa 7.30 mchana ili kuzungumza na Mganga Mfawidhi wa Bombo, Dk. Jumanne Karia kutokana na Katibu Tawala Mkoa wa Tanga (RAS), Zena Said kuwaruhusu waandishi hao kwenda kuzungumza na kiongozi huyo ili kupewa kauli ya serikali katika kadhia hiyo.

Tukio hilo lilizuka mara tu baada ya kufika eneo hilo, ambapo walinzi hao walianza kuwazuia na kuwatolea maneno makali na kugoma kufungua geti. Mmoja wao alidai kwamba kamwe hawezi kuwasikiliza kwa sababu Mganga Mfawidhi hajampatia taarifa yoyote kuhusu ujio wao.

Waandishi hao walijitahidi kuwaelewesha walinzi hao kwamba tayari walishawasiliana kwa simu na viongozi wa hospitali, kinachotakiwa ni wao kuwaruhusu kupita ili kwenda ofisi ya utawala, juhudi zao hizo hazikufanikiwa kutokana na walinzi kung’ang’ania msimamo wao huo.

Walidai wanatii amri ya bosi wao, ambaye ni Dk Kariya. Mabishano kati ya walinzi na waandishi hao, yaliendelea kwa muda mpaka alipojitokeza kiongozi wa walinzi hao na kuamua kumpigia simu Dk Karia ili kujiridhisha kuhusu kauli ya waandishi hao kutoka kwa RAS.

Kinyume na matarajio, kiongozi wa walinzi hao alisema, “Jamani Mganga Dk Karia ameniagiza niwajulishe kwamba kwa sasa hana muda wa kuzungumza nanyi, kwa kuwa tayari awali walishaamua kuripoti habari”.

Hivyo, alisema anawataka waandishi hao watoke haraka eneo hilo. Ukosefu wa dawa ya usingizi katika hospitali ya Bombo, ulianza kujitokeza Desemba 28 mwaka huu mchana na kusababisha wagonjwa kuendelea kusubiri wodini bila matumaini.

SOURCE HABARI LEO.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *