Home / Habari Za Kitaifa / MBARAWA AIBANA SWISSPORT TANZANIA, AIPA MIEZI MIWILI.

MBARAWA AIBANA SWISSPORT TANZANIA, AIPA MIEZI MIWILI.

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa miezi miwili kwa kampuni ya Swissport Tanzania kuhakikisha inaboresha huduma zake kinyume chake, atafuta leseni ya kampuni hiyo.

Kampuni hiyo ya Swissport ambayo inashughulikia mizigo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam imelalamikiwa kushuka kwa huduma zake katika uwanja huo.

Akizungumza katika ukumbi wa mikutano katika uwanja huo, Waziri Mbarawa alisema, kampuni hiyo imefanya kazi kwa muda mrefu katika uwanja huo na hivyo haiwezi kujulikana kama huduma zake ni nzuri au mbaya kwa kuwa hakuna wa kumpima naye.

Alisema hivi karibuni alipata ripoti iliyokuwa ikionesha kuwa huduma za kampuni hiyo hazikuwa nzuri na kwamba katika kipindi cha mwaka jana Wizara yake ilitoa leseni kwa kampuni nyingine ya Nas-Dar Airco ambayo hata hivyo hadi sasa haijaanza kazi.

“Nakuomba sana, tunakupa miezi miwili kama huduma yako hukuweka vizuri naomba Mamlaka (regulatory) ulete tufute leseni ya huyu bwana, mimi nimepewa mamlaka na kanuni na sheria zipo, kama ukishindwa kutoa huduma hiyo, miezi miwili hukubadilika tutakufutilia mbali,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema tangu kampuni ya Nas- Dar Airco ipewe leseni haijafanya kazi uwanjani hapo na inawezekana kukawa na sababu mbili ambazo ni Swissport kuweka mazingira ambayo yanaifanya kampuni hiyo ishindwe kufanya kazi lakini pia kampuni kutokuwa na uwezo. Hata hivyo, alisema haiwezekani kupima uwezo wake wakati haijapata fursa ya kufanya kazi.

“Sasa mimi nimeshangaa sana kuona wewe ni mpangaji umepanga nyumba halafu hutaki wapangaji wengine waingie, unafanya mambo ya ujanjanja haiwezekani…,”. “Nimemuita mdhibiti nikamwambia lazima aangalie kama Swissport anafanya ujanja wowote kinyume na utaratibu wa leseni yake ili tuifutilie mbali, kama anafanya ujanja wowote kinyume na leseni aliyopewa na kama hukujipanga tutafuta hiyo leseni, unanisikia? tutafuta hiyo leseni,” alisisitiza Mbarawa.

Alisema ni lazima kampuni hiyo ifanye kazi katika uwanja huo pamoja na watu wengine na kwamba kama walizoea kufanya hivyo si kwa wakati huu kwa kuwa hizi ni zama tofauti, hivyo lazima wafuate taratibu na kanuni zilizowekwa, vinginevyo akipewa leseni ya kampuni hiyo ataifuta.

Profesa Mbarawa alisema anaamini kuna makampuni mengi duniani yanayoweza kutoa huduma hizo na kwamba suala hilo halihusiani na moto uliowaka katika chumba cha kuhifadhia mizigo kinachosimamiwa na kampuni hiyo.

Katika hatua nyingine, aliitaka kampuni ya Nas-Dar Airco kuanza kazi mara moja huku akitaka Swissport kuacha ujanja wa kuingia mikataba na kampuni nyingi za ndege kabla ili kuwazuia watu wengine wasipate kazi.

Aidha, aliagiza uchunguzi mikataba hiyo ili kuangalia kama huo utaratibu uliotumika kuingia mikataba hiyo ulifuata utaratibu wa kisheria au ni njia moja ya kuhodhi ili mwingine asipate kazi.

Akizungumzia adhabu zilizopo kisheria kwa atakayebainika kufanya kosa, alisema adhabu hizo ni ndogo kwani adhabu ya juu ni dola za Marekani 5,000 ambazo alisema ni lazima zibadilishwe ili ziwe ni fundisho kwa wakosaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Swissport nchini, Mrisho Yassin alisema, kuwa hawezi kuzungumzia lolote bali atakutana na waziri kwa ajili ya mazungumzo na baada ya hapo ataitisha mkutano na vyombo vya habari kutoa ufafanuzi.

SOURCE HABARI LEO.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *