Home / Habari Za Kitaifa / MAKONDA ATAJA JINA AKABIDHI MENGINE 97.

MAKONDA ATAJA JINA AKABIDHI MENGINE 97.

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amemkabidhi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Rodgers Sianga orodha mpya ya majina 97 ya watu wanaosadikiwa kujihusisha na biashara hiyo.

Kamishna huyo amemuahidi Makonda kuwa ataishughulikia na wote waliotajwa katika orodha hiyo hawataonewa na watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Aidha, baada ya kukabidhi orodha hiyo, Makonda ametoa mwito kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kurudisha wazo lake la kuweka kifaa kwa ajili ya kuwapima wabunge kama wanatumia dawa za kulevya.

“Nakumbuka kipindi fulani Spika wa Bunge alitamani kuweka utaratibu wa kuwapima wabunge kabla ya kuingia bungeni, sasa ni wakati wa kufanya hivyo naamini wazo hili hakuliwaza tu kuna kitu aliona.

Nimuombe sasa ule utaratibu auweke tu tukifanya hivyo tutafanikiwa kujenga taifa,” alisema Makonda ambaye jana hakutaja majina ya waliomo katika orodha hiyo kama alivyofanya wakati akitaja orodha mbili za kwanza.

Katika orodha ya kwanza ilikuwa na majina ya baadhi ya watu maarufu hasa jijini Dar es Salaam wakiwamo wasanii wa muziki na maigizo ambao 13 walikwisha fikishwa mahakamani, wakati orodha ya pili ilikuwa na majina 65 wakiwamo wanasiasa, wafanyabiashara, viongozi wa dini na kampuni za mafuta.

Badala yake jana, Makonda alimtangaza kumhitaji mtu mmoja, Rashid Said maarufu Chidi Mapenzi, kufika Kituo Kikuu cha Polisi.

Aidha alisema kwamba wapo ambao wapo katika biashara hiyo kuanzia utawala wa serikali ya awamu ya pili hadi ya sasa.

Aliwataka wote wanaopingana naye kwa jinsi anavyolishughulikia suala hilo, kusoma vyema Sheria ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Namba 5 ya mwaka 2015, kujiridhisha kabla ya kuanza kumtuhumu kwamba anakwenda kinyume cha taratibu.

Aidha, mkuu huyo wa mkoa alitoa mwito kwa viongozi wa dini kuendelea kuwaombea, lakini pia hatosita kumshughulikia kiongozi wa dini atakayehusika na biashara hiyo.

“Niseme tu najua mnaomba endeleeni kuomba lakini sitamvumilia kiongozi yeyote wa dini atakayebainika kuhusika na biashara hii, nitamnyofoa mmoja mmoja ili tuwaondoe wale viongozi wanaotia doa,” aliongeza Makonda katika mkutano wake na viongozi mbalimbali wa mkoa huo jana uliohudhuriwa na Kamishna Sianga na maofisa wake.

Aidha, viongozi wa dini hawakuwa nyuma kupongeza juhudi hizo kwani Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam, Shehe Alhadi Mussa alisema suala la dawa za kulevya ni kubwa na inahitaji mapambano ya pamoja na mtu anayeshughulikia suala hilo asitarajie kupendwa na mtu, bali atarajie kupendwa na Mwenyezi Mungu.

“Ukitaka kupendwa na watu wewe utakuwa ni zaidi ya Yesu, Mtume na Mungu sababu wao hawakupendwa na watu wakati wakisimamia haki, mapambano haya ni mapambano yanayohitaji kumtanguliza Mungu na kuwa muadilifu,” alisema Shehe Alhadi.

Kwa upande wake, mmiliki wa nyumba ya waathirika wa dawa za kulevya (sober house) iliyopo Kigamboni, Nuru Salehe alimpongeza Makonda kwa juhudi zake na kuahidi kumpa ushirikiano, lengo likiwa ni kumaliza matumizi ya dawa za kulevya nchini.

“Watu wanaongea sana na kukuponda, lakini hawazijui athari za dawa za kulevya, kwenye kituo changu niko na watoto wadogo miaka 16 waliharibiwa na dawa hizi wameshindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya dawa. Kwa kweli acha waongee, lakini sisi tutakuunga mkono,” alisema Nuru.

Naye msanii wa muziki wa Bongo fleva, Khaleed Mohamed maarufu TID ambaye alitajwa na Makonda katika orodha yake ya kwanza ya washukiwa wa dawa za kulevya, alikiri kujihusisha na matumizi ya dawa hizo na kuahidi kushirikiana na mkuu wa mkoa katika mapambano hayo.

Wakati huo huo, watu 311 wanaotuhumiwa kujihusisha na uuzaji, usambazaji, na utumiaji wa dawa za kulevya wamekamatwa na Jeshi la Polisi kupitia operesheni ya dawa za kulevya iliyoanza Februari mosi, mwaka huu.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro akitoa taarifa ya operesheni ya mapambano ya dawa za kuevya iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema lengo la operesheni hiyo ni kuwabaini na kuwasaka na kuwakamata watuhumiwa wanaojihusisha na uuzaji, usambazaji, matumizi na udhamini wa dawa za kulevya katika mkoa huo.

Aliongeza kuwa baada ya kuanza kwa operesheni hiyo, Kamati iliundwa na mkuu wa mkoa na iliongozwa na Naibu Kamishna wa Upelelezi Kanda Maalumu kwa ajili ya uchunguzi kwa wale walioitwa kuhojiwa na iliwashirikisha Usalama wa Taifa, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Uhamiaji na Polisi.

Alisema licha ya kukamatwa kwa watu hao, pia vielelezo mbalimbali vilikamatwa ikiwemo dawa za kulevya aina ya kokeni na heroini kete 544, bangi puli 438, magunia matano na nusu, misokoto 37 na mirungi bunda 21.

Kamanda Sirro alisema watuhumiwa waliokamatwa wapo katika makundi matatu ambayo ni watuhumiwa 117 walikutwa na vielelezo na kufunguliwa kesi majalada 42, watuhumiwa 194 ambao hawakukutwa na vielelezo na kufunguliwa majalada ya uchunguzi 48 na wapo watuhumiwa 77 waliotajwa na mkuu wa mkoa wajisalimishe wakiwemo wafanyabiashara, wasanii,viongozi wa dini, waagizaji wa mafuta.

Alisema jumla ya watuhumiwa 32 wakiwemo askari tisa waliotajwa na mkuu wa mkoa wameripoti kituo cha polisi kwa ajili ya mahojiano na juhudi za kuwapata wale ambao hawajafika zinafanyika.

“Kama umeombwa ufike hujaja umekaidi ni lazima tukutafute tukukamate, uhojiwe,” alisema Kamanda Sirro.

Pia alisema jumla ya majalada matatu yenye watuhumiwa 16 yamefikishwa mahakamani na watuhumiwa wengine wanaendelea kuhojiwa na Jeshi la Polisi ili kukamilisha uchunguzi utakaowezesha kuwapata watuhumiwa wengine na vielelezo.

Aliongeza kuwa majalada 28 yanaandaliwa kwa ajili ya kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai.

Akitoa ufafanuzi juu ya kwa nini mkuu wa mkoa anahusika kukamata na kuwaita watu, alisema mkuu wa mkoa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na anapotaka kujua viongozi wa chini yake wanafanya vipi kazi zao, ni lazima ahusike kufanya kazi.

SOURCE HABARI LEO.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *