Home / Habari Za Kitaifa / NHC kukamilisha nyumba 300 za watumishi Dodoma

NHC kukamilisha nyumba 300 za watumishi Dodoma

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC), limejiandaa kuwezesha upatikanaji wa nyumba za watumishi wa Serikali mkoani Dodoma kwa kujenga nyumba 300 katika mradi wa Iyumbu Satellite Center ambazo zinategemewa kukamilika Juni mwaka huu.

Meneja Mauzo wa NHC, Erasto Chilambo alisema tayari wameshajenga nyumba za makazi 153 eneo la Medeli, Mjini Dodoma kwa ajili ya kuuza na kwa sasa bado nyumba 97 zinaendelea kuuzwa kwa wananchi.

Aidha, alisema wamejenga nyumba 44 wilayani Kongwa nje kidogo ya mji wa Dodoma ambazo wanaziuza kwa wananchi.

“Tumeshaanza ujenzi wa nyumba katika mradi wa Iyumbu katika eneo lenye ukubwa wa ekari 234 na ni moja ya sehemu ya mji uliopangiliwa kitaalamu kwa kuzingatia sheria na kanuni za mipango miji na utajengwa katika awamu tatu,” alisema.

Alisema awamu ya kwanza itajumuisha nyumba 300 na zitakuwa na ukubwa tofauti zikiwemo zenye ukubwa wa meta za mraba 79, 85 na 115 zenye vyumba vitatu kila moja na ni mradi wa nyumba za chini zisizoungana.

Alisema mradi huo una huduma zote muhimu ikiwemo mfumo wa maji safi na salama, umeme, maegesho ya magari, maji ya akiba, shule ya awali, zahanati na barabara zinazopitika.

Pia alisema shirika hilo limetenga maeneo kwa ajili ya viwanja vya michezo na maeneo ya biashara za maduka ili kuwapatia mahitaji muhimu wakazi wa Iyumbu.

Hata hivyo, alisema Shirika hilo lina lengo la kujenga nyumba katika maeneo yote ya nchi ili kufikia kila sehemu ya nchi hasa kusaidia kujenga nyumba katika maeneo mapya na wilaya mpya zinazoanzishwa na serikali.

 

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *