Home / Habari Za Kitaifa / Mhasibu wa Wizara ya Kilimo kizimbani

Mhasibu wa Wizara ya Kilimo kizimbani

KAIMU Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Peter Musiba amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na uzembe.

Mshitakiwa amefikishwa mahakamani leo mbele ya Hakimu wa mahakama ya wilaya, Kihawa na kusomewa mashitaka na waendesha mashitaka wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Maghela Ndimbo na Gloria Mwainyekule.

Hayo yamebainishwa leo katika taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari na Uhusiano wa Takukuru, Mussa Misalaba kwa vyombo vya habari Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa waendesha mashitaka hao, mashitaka ya kwanza yanayomkabili mhasibu huyo, ni kosa la matumizi mabaya ya nafasi yake kinyume na Kifungu Namba 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.

Inadaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati ya Januari 14 hadi 20, 2009 katika maeneo ya Ofisi za Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika zilizopo wilayani Temeke ndani ya mkoa na Jiji la Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa mwajiriwa wa wizara hiyo kama Kaimu Mhasibu Mkuu kwa makusudi alitumia vibaya nafasi yake kwa kuidhinisha malipo ya Sh milioni 141.6 kwa Kampuni ya Shivlal Tank (Shivlal Tank &Co. LTD).

Malipo hayo yalihusu mkataba namba 016/2007 uliosainiwa baina ya wizara hiyo na Kampuni ya Shivlal Tank &Co. LTD uliohusu kuiuzia wizara pembejeo za kilimo, bila kuhakiki usahihi na uhalali wa malipo hayo, kitendo ambacho ni kinyume cha Kanuni 87(1)(d) na 90 za Kanuni za Fedha za Umma, 2001 GN za 2001.

Katika mashitaka ya pili, mahakama hiyo ilielezwa na upande wa mashitaka kuwa katika tarehe tofauti kati ya Januari 14 hadi 20, 2009 kwenye ofisi za wizara hiyo, mshitakiwa aliisababishia hasara wizara kiasi cha Sh milioni 141.6 kwa kushindwa kwake kuwa mwangalifu.

Mshitakiwa huyo alikana mashitaka yote na dhamana yake ilikuwa wazi na alitakiwa kulipa nusu ya thamani ya fedha aliyoisababishia hasara wizara hiyo au kuweka dhamana ya nyumba yenye thamani sawa na nusu ya hasara hiyo.

Pia mshtakiwa huyo alitakiwa kuwa na wadhamini wawili mmoja akiwa mtumishi wa umma waliotakiwa kusaini dhamana ya Sh milioni 10 kila mmoja.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo hakuweza kutimiza masharti ya dhamana na hivyo kupelekwa mahabusu.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 10, mwaka huu, itakapotajwa tena kwa kuwa bado uchunguzi unaendelea.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *