Home / Habari Za Kitaifa / Mahakama yakubali rufaa ya The Guardian isikilizwe

Mahakama yakubali rufaa ya The Guardian isikilizwe

MAHAKAMA ya Rufaa imekubali ombi la Kampuni ya The Guardian Ltd la kuomba rufaa yao iliyokatwa nje ya muda kusikilizwa kwa kuwa makosa ya kuchelewesha na kukatwa rufaa hiyo nje ya muda yalikuwa ya kimahakama na si ya kampuni hiyo.

Rufaa hiyo inahusu kesi iliyompa ushindi mfanyabiashara wa madini ya tanzanite, Justine Nyari ya kulipwa mamilioni ya fedha na The Guardian Ltd kutokana na kampuni hiyo kumchafulia jina lake kwenye vyombo vya habari.

Februari 23 mwaka huu wakili wa The Guardian Ltd, Coolman Ngalo aliwasilisha maombi mbele ya majaji watatu wakiongozwa na Mwenyekiti wa jopo hilo, Bernad Luanda, Mussa Kipenka na Stella Mugasha ya kuwaomba majaji hao kuisikiliza rufaa hiyo.

Majaji hao walipokea maombi hayo na wakili Ngalo alitoa sababu nyingi za kuchelewa kukata rufaa ndani ya muda, ikiwa ni pamoja na rufaa iliyotolewa katika Mahakama Kuu chini ya Jaji Kakakusola Sambo kucheleweshwa na watendaji wa mahakama kuitoa, hivyo kuchelewa kukata rufaa ndani ya muda.

Baada ya kusikiliza hoja hizo za wakili Ngalo, majaji hao jana walitoa uamuzi uliosomwa na Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Amri Msumi na kueleza kuwa jopo limekubali ombi hilo na rufaa hiyo sasa itasikilizwa katika kikao kijacho cha mahakama hiyo mkoani Arusha.

Msajili alisema kuwa majaji wameangalia vitu vingi vya msingi na moja ya vitu muhimu ni kitendo cha watendaji kushindwa kutoa hukumu ya Mahakama Kuu kwa wakati muafaka hali iliyofanya mkata rufaa kushindwa kukata rufaa ndani ya muda.

“Sasa rufaa hii inaweza kusikilizwa katika kikao kijacho baada ya majaji kukubali ombi lililowasilishwa na wakili Ngalo,” alisema Msajili.

Akizungumza nje ya mahakama, wakili wa mfanyabiashara wa madini ya tanzanite aliyekuwa na kesi dhidi ya kampuni hiyo, Justine Nyari, Loom Ojare, alidai kuwa hana wasiwasi na maamuzi hayo na wamejiandaa kikamilifu na rufaa hiyo.

Nyari alishinda kesi hiyo katika Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, chini ya Jaji Sambo mwaka 2008 na kuiamuru kampuni hiyo ya The Guardian kumlipa mfanyabiashara huyo mamilioni ya fedha kwa kumchafuliwa jina lake katika vyombo vyake vya habari.

Hata hivyo, mwaka juzi kesi hiyo ilisikilizwa katika mahakama hiyo ya rufaa chini ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Edward Rutakangwa na kuiamuru kampuni hiyo kumlipa Nyari mamilioni ya fedha kwani kesi hiyo ilikatwa katika mahakama hiyo nje ya muda kwa hiyo haikupaswa kusikilizwa.

Hata hivyo, wakili Ngalo aliirudisha tena rufaa hiyo katika mahakama hiyo na kusema kuwa kuchelewa kukata rufaa ndani ya muda hakukutokana na makosa yake bali yalikuwa makosa ya kiutendaji ya mahakama.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

CCM YASHINDA UBUNGE, UDIWANI KWA 100%

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimeshinda kwa asilimia 100 kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Buyungu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *