Makala

Korosho ni ‘mboni’ ya Tanzania kiuchumi

FEBRUARI mwaka huu Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) ilianza mpango wa kugawa bure miche ya korosho kwa wakulima ili waongeze uzalishaji wa zao hilo.

Katika mkutano wa wadau wa korosho uliofanyika Mtwara mwaka huu, ukiwashirikisha wajumbe wengine wakiwamo wakuu wa mikoa ya Lindi, Pwani, Tanga, Mtwara na Ruvuma inaelezwa umuhimu wa mpango.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CBT, Hassan Jarufu, amewaambia wadau wa korosho kwamba kwa kuanzia jumla ya miche milioni 10 itasambazwa kwa wakulima wa mikoa ya Lindi, Pwani, Tanga, Mtwara na Ruvuma.

Mjumbe wa Bodi ya CBT, Profesa Peter Masawe anasema kwenda mbele utafiti unaendelea kutazama jinsi ya kuanzisha na kupanua kilimo cha korosho katika mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Kigoma na baadhi ya maeneo katika mkoa wa Kilimanjaro.

Profesa Masawe ambaye mtafiti gwiji wa kimataifa wa korosho, anasema Tanzania inasimama katika nafasi nzuri ya kuongeza uzalishaji korosho ambalo ndilo zao lililobaki pekee lenye mipango endelevu na lenye soko lisiloyumba kwa sasa. Lakini, je, mkakati huo wa CBT kugawa bure miche ya korosho kwa wakulima ni endelevu kwa namna gani?

Anasema Profesa Masawe: “ Mkakati huu ni mzuri sana na umetumika hata nchi nyingine kama Ivory Coast kuongeza uzalishaji. Lakini inabidi tuongeze kipengele kinachombana anayepokea miche kuhakikisha inatunzwa. Ni muhimu kila anayepewa miche msimu ujao apewe elimu na mkataba wa kuutunza.

Hatua hiyo ni pamoja na kuhakikisha kuwa miche inayogawiwa bure haitelekezwi. Mkataba uainishe kuwa mche ukifa bila mkulima kutoa taarifa, basi mkulima husika ataulipia mche huo. Kama atatoa taarifa kwa ofisa ugani wake basi anaweza kupewa mche mwingine ikithibitika kuwa haukufa kwa uzembe.

Mkakati huu utakuwa ni endelevu na utakuwa kichocheo cha kupanda mikorosho mipya. Halmashauri husika nazo zitalazimika ziandae mpango mkakati wa kuhakikisha agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kupanda mikorosho 5,000 kila kijiji linatekelezwa kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho Tanzania.

Bodi haitazalisha miche ya kutosha nchi nzima bali inachangia uzalishaji huo wa miche. Halmashauri na NGOs nazo zina fursa ya kuchangia uzalishaji miche pia.” Katika hali ambayo pamba, tumbaku, katani, kahawa, chai na pareto si mazao ambayo yanatajwa tena katika usafirishaji nje ya nchi, wadau wa korosho wanasema sasa zao hilo ndiyo mkombozi wa mkulima na nchi.

Kwa mujibu wa Profesa Masawe, korosho za Tanzania zina soko kubwa duniani, zinapendwa kwa kuwa zina ladha nzuri na zinaingia sokoni katika miezi ambayo huko nje kunakuwa tayari kuna uhaba. Na sasa kuna hoja kwamba pamoja na kuziuza nje, Watanzania wahamasishwe kula korosho, ikibidi kwa kampeni kama ile ya uhamasishaji wa utalii wa ndani, ili kupanua soko lake.

Korosho kubwa huuzwa kwa bei ya juu. Korosho ndogo huuzwa kwa bei ya chini kidogo. Korosho zilizokatika huuzwa kwa nusu ya bei wakati ambapo zikiongezewa thamani na kuuzwa nchini hupata bei ya juu zaidi. Korosho ni zao linalojipambanua na mazao mengine kutokana na kwamba, haliathiriki sana na ukame kama mazao mengine.

Kwa nchi nyingine duniani, uzalishaji korosho unatajwa kushuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo, ukosefu wa mbegu bora; ukosefu kanuni bora za kilimo, kukosekana kwa wataalamu bora wa korosho na kukosekana kwa ardhi ya kutosha.

Tanzania imetoa mbegu bora za korosho 38 na mbegu chotara za korosho 16 na kuwa nchi ya kwanza Afrika kusajili mbegu bora 54 zinazokubalika na kutambuliwa na taasisi ya kimataifa International Union of Protection of Plant varieties (UPOV). Mbegu hizo zina tija katika uzalishaji na zina ubora wa kipekee barani.

Tanzania pia ina wataalamu elekezi waliobobea katika Afrika ambao hutoa huduma ya kitaalamu ya zao la korosho. Taasisi ya Utafiti Naliendele ni kitovu cha Utafiti wa Korosho Afrika. Yapo maoni kwamba, ili mkulima wa korosho wa Tanzania aneemeke zaidi, itabidi zibanguliwe nchini.

Vipo vyama kama Tandahimba and Newala Co-operative Union (Tanecu) ambavyo viko tayari kuanza ubanguaji kuongezea thamani na kupanua ajira. Profesa Masawe anasisitiza: “Ni kweli itabidi korosho zibanguliwe hapa nchini ili kuongeza si thamani na ajira tubali pia kuhakikisha bei ya korosho haiyumbi. Kubangua korosho nchini kutaongeza ushindani katika bei ya korosho.”

Anasema nchi ina mbegu bora za korosho kuliko nchi yoyote barani Afrika; tuna watafiti elekezi wa zao la korosho waliobobea barani Afrika; tuna vituo vya uendelezaji wa zao la korosho vinavyoweza kutumika kuzalisha miche ya korosho maeneo mengi yanayolima korosho Tanzania.

Aidha, tuna vituo na vitalu binafsi vinavyoweza kuzalisha miche ya mikorosho Dodoma na Singida; tuna ardhi ya kutosha kupanua kilimo cha korosho bila kuathiri uzalishaji wa mazao mengine ya chakula. Bei nzuri ya korosho iliyopatikana msimu uliopita imekuwa kichocheo kikubwa cha kuwahamasisha wakulima kutamani kilimo cha korosho.

Mambo mengine yanayohamasisha wakulima ni sera ya serikali ya kuendeleza Tasnia ya Korosho ambayo imeweka mazingira rafiki na ya kuvutia wawekezaji. Anasema yapo maombi mengi ya mbegu za korosho kutoka mikoa ambayo haijawahi kulima korosho huko nyuma hasa kutokana na ukame.

Maeneo hayo ni wilaya za Mwanga, Same (Kilimanjaro), mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Kagera, Rukwa, Mbeya na Kigoma, na mingineyo. Mafanikio huvuta pia changamoto. Na kati ya hizo ni upungufu wa maghala ya kuhifadhia korosho katika mikoa yote ukiondoa Mtwara.

Changamoto nyingine ni mgongano wa maslahi unaotajwa sana kuwahusisha wanasiasa na utitiri wa vyama unaotishia maslahi ya vyama na mkulima. Kama mjumbe wa CBT na mbobezi katika Tasnia ya Korosho, Profesa Masawe anazielezeaje changamoto hizo?

Maghala yanayozungumziwa yako ya aina mbili ambayo ni yale yaliyo katika ngazi ya Chama cha Msingi (AMCOS) na makubwa yaliyosajiliwa na Bodi ya Leseni za Maghala Tanzania kwa ajili ya kutoa stakabadhi ghalani kabla ya mnada. Maghala yote ni muhimu katika kuhifadhi korosho ili zibakie na ubora unaokubalika kimataifa.

Katika Mikoa ya Lindi na Mtwara maghala ya kuhifadhi korosho ghafi yapo pamoja na kwamba baadhi yake yanahitaji ukarabati. Mikoa mingine haina maghala ya AMCOS wala maghala yenye sifa za kusajiliwa na Bodi ya Leseni za Maghala Tanzania kwa ajili ya kupokea korosho na mazao mengine kwa ajili ya Stakabadhi Ghalani kabla ya mnada.

Kukosekana kwa maghala katika mikoa mingine kuna athari kubwa ikiwemo udhibiti ubora wa korosho kushindikana ngazi ya AMCOS. Maghala makuu husaidia uhifadhi wa korosho nyingi kwa wakati mmoja na kuwapunguzia wakulima na manunuzi adha ya kwenda minada yenye kiwango kidogo cha korosho.

Changamoto nyingine ni juu ya wanasiasa kuingilia katika masuala ya korosho. Wajumbe wengi waliokuwa katika mkutano wa wadau wa korosho wanaamini kabisa kuwa wapo wanasiasa wa namna hiyo. Baadhi wanadaiwa ni wamiliki au wana hisa kubwa katika kampuni zinazojihusisha na biashara ya viuatilifu vya zao la korosho au kampuni zinazonunua korosho ghafi na kusafirisha nje ya nchi.

Wengine ni mawakala wa kununulia kampuni za nje na ndani korosho kutoka mnada wa stakabadhi ya mazao ghalani au nje ya minada hiyo. Na hali hiyo inaleta mgongano wa kimaslahi. Pia ipo changamoto ya utitiri wa vyama vya msingi unaoongeza gharama za uendeshaji wa AMCOs.

Wajumbe wanashauri kuwa, kuviunganisha vyama hivyo kutakuwa na tija kwa kuwa gharama za uendeshaji zitapungua na kuwezesha AMCOS kubakia na kiasi cha fedha kitakachosaidia uboreshaji wa miundombinu kama maghala yake na hata kuwa na usafiri wao wenyewe.

Show More

komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close