ImaniVimeoYoutube

Ni Zipi Nguzo Tano za Uislamu

Nguzo tano za Uislamu ni mfumo wa maisha ya Muislamu. Ndizo ushahidi wa Imani, Swalah, utoaji wa Zakaah (kuwasaidia wernye dhiki), kufunga katika mwezi wa Ramadhaan na kuhiji Makkah mara moja maishani kwa wale wenye uwezo

1) Shahada ya Imani

Ushahidi wa Imani ni kusema kwa kusadikisha, “La ilaaha illAllaah, Muhammadur Rasulullah.” Maana ya matamshi haya ni, “Hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu (Allaah), na kwamba Muhammad ni Mjumbe (Mtume) wa Mwenyezi Mungu.” Sehemu ya kwanza, “Hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki, isipokuwa Mwenyezi Mungu,” inamaanisha kwamba hapana mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu peke Yake, na kwamba Yeye hana mshirika wala mwana. Ushahidi huu wa Imani unaitwa Shahada, ambayo ni kanuni nyepesi ambayo inapaswa itamkwe pamoja na kusadiki ili mtu aweze kuingia katika Uislamu, kama ilivyoelezwa hapo juu. Ushahidi wa Imani ndio nguzo muhimu zaidi katika Uislamu.

2) Swalah

Waislamu huswali Swalah tano kila siku. Kila Swalah huchukuwa muda mfupi wa dakika chache tu. Swalah katika Uislamu ni mawasiliano ya moja kwa moja kati ya mja na Mwenyezi Mungu. Hakuna kishenga baina ya Mwenyezi Mungu na mfanyaji ibada.

Ndani ya Swalah, mtu hujisikia ndani mwake furaha, amani na faraja, na kwamba Allaah yu radhi naye. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Bilaal adhini, ili tufarijike nayo.))[109] Bilaal alikuwa mmojawapo wa Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na alikuwa mwadhini.

Swalah hufanyika wakati wa Alfajiri, Adhuhuri, Alasiri, Magharibi na ‘Ishaa. Muislam anaweza kuswali karibu mahali popote, kama vile mashambani, ofisini, viwandani au vyuoni.

Tafadhali, tembelea www.islam-guide.com/pillars kwa ajili ya maelezo zaidi juu ya Swala katika Uislamu.[110]

3) Kutoa Zakaah (Kuwakunjulia Wenye Dhiki):

Kila kitu ni cha Mwenyezi Mungu, na hata mali zinazohifadhiwa na wanaadamu kama dhamana. Maana khalisi ya neno Zakaah ni zote mbili ‘kutwaharisha’ na ‘kukua.’ Maana ya kutoa Zakaah ni kutoa asilimia iliyotajwa bayana kutokana na mali fulani kwa kuwapatia makundi fulani ya watu wenye dhiki. Asilimia inayopaswa kulipwa kutokana na dhahabu, fedha na pesa taslimu zenye kufikia kiasi kinacholingana na gramu 85 za dhahabu na kubaki katika miliki ya mtu kwa mwaka mmoja wa Kiislamu ni asilimia mbili unusu. Tunavyovimiliki hutakasika kwa kutenga pembeni sehemu ndogo tu kwa ajili ya wenyedhiki, na kama vile kupogoa matawi ya mimea, huku kupunguza salio na kunatia moyo wa ukuaji mpya.

Mtu anaweza kutoa zaidi kadiri atakavyo kama Sadaka.

4) Kufunga katika Mwezi wa Ramadhaan Kila mwaka katika mwezi wa Ramadhaan,[111]Waislamu hufunga tangu Alfajiri hadi kuchwa kwa jua, kwa kujizuia kula, kunywa na tendo la ndoa.

Ingawa Swawm ni yenye faida za kiafya, huchukuliwa kimsingi kuwa ni namna ya kuisafisha nafsi kiroho. Kwa mmojawapo kujizuia dhidi ya starehe za kidunia, japo kwa muda mfupi, mfungaji hupata huruma ya kweli kwa wanaopatwa na njaa, kadhalika na kuongezeka kwa maisha yake ya kiroho.

5) Kuhiji Makkah:

Hija ya kila mwaka Makkah ni faradhi ya kufanywa mara moja tu maishani kwa wenye uwezo wa kimwili na mali katika kuitekeleza. Kadiri ya watu milioni mbili huenda Makkah kila mwaka kutoka kila sehemu duniani. Ingawa mara zote Makkah huwa imesheheni wageni, Hija ya mwaka hufanywa katika mwezi wa kumi na mbili katika kalenda ya kiislamu. Mahaji wa kiume huvaa nguo maalumu na rahisi ambayo huondosha mbali tofauti za kimatabaka na tamaduni kiasi kwamba wote huwa sawa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Mahujaji wakiswali katika Msikiti wa Haram huko Makkah. Msikitini humu mna Ka’abah (jengo jeusi linaloonekana katika picha)­ ambalo Waislamu hulielekea wakati wakiwa katika Swalah. Ka’abah ni mahali pa ibada ambapo Mwenyezi Mungu Aliwaamuru Mitume Ibraahiym na mwanaye, Isma’iyl waijenge.

Ibada za hija ni pamoja na kuitufu Ka’abah mara saba na kwenda mchakamchaka baina ya kilima cha Swafa na Marwa mara saba, sawa na Hajar alivyofanya wakati akitafuta maji. Kisha, Mahujaji husimama pamoja katika uwanja wa ‘Arafah[112]na kumwomba Mwenyezi Mungu wakipendacho na kwa ajili ya maghufira, katika kile ambacho mara nyingi hufikirika kuwa ni onyesho la awali la Siku ya Malipo.

Mwisho wa Hijjah huweza kujulikana kwa sikukuu ya ‘Iydul-Adhw-haa, ambayo husherehekewa kwa Swalah. Sikukuu hii na ‘Iydul-Fitwr, sherehe ya kuadhimisha mwisho wa Ramadhaan ndio sikukuu mbili za kila mwaka katika kalenda ya Kiislamu.

Tafadhali, tembelea www.islam-guide.com/pillars kwa ajili ya maelezo zaidi juu ya nguzo tano za Kiislamu.

[109]Imesimuliwa na Abu Dawuud, Na. 4985, na Musnad Ahmad, Na. 22578
[110]Au rejea kitabu kiitwacho A Guide to Prayer in Islam, M. A. K. Saqib. Tembelea tovuti iliyotajwa hapo juu kwa ajili ya kujipatia nakala
[111]Mwezi wa Ramadhaan ni wa tisa katika kalenda ya Kiislamu (ambayo hufuata mwezi, si jua)
[112]Eneo lililo kadiri ya maili 15 kutoka Makkah

Show More

komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close