Home / Habari Za Kitaifa / Matumizi mkaa kuongezeka nishati mbadala zisipotumika

Matumizi mkaa kuongezeka nishati mbadala zisipotumika

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amesema ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa kupata nishati mbadala, matumizi ya mkaa nchini yataongezeka hadi kufikia tani milioni 4.6 ifikapo mwaka 2030 kutoka tani milioni 2.3 zinazokadiriwa kutumika nchini mwaka 2012.

Profesa Maghembe alisema hayo katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo wakati wa Siku ya Kitaifa ya Upandaji Miti iliyofanyika mkoani Morogoro.

Alisema nchi ina vyanzo mbalimbali vya nishati kwa matumizi ya wananchi, lakini itokanayo na miti inafanya matumizi yanayofikia asilimia 85.

Alisema nishati itokanayo na bidhaa za petroli ni asilimia 9.3, umeme ni asilimia 4.5 na makaa ya mawe na vyanzo vingine ni asilimia 1.2 tu ya mahitaji yote.

“Inajulikana wazi kwamba wakazi wengi wa mijini wanategemea mkaa kwa mahitaji ya nishati katika matumizi ya nyumbani,” alisema Profesa Maghembe, na kuongeza kuwa matumizi ya mkaa yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukuaji wa kasi wa miji na ongezeko la watu, bei kubwa pamoja na uhaba wa nishati mbadala, umeme na gesi.

Profesa Maghembe alisema hali hiyo ya matumizi makubwa ya mkaa itasababisha kupungua kwa eneo la misitu nchini na kuathiri maisha ya wanadamu na wanyama.

Alisema mahitaji ya nishati yanategemea nishati itokanayo na misitu, hivyo hakuna budi kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba nishati hiyo inaendelea kupatikana, lakini katika misingi bora na endelevu kwa kuhakikisha misitu inaendelea kuwepo.

Alisema kaulimbiu ya maadhimisho ya upandaji miti kitaifa mwaka huu ni “Panda miti, Tunza Misitu upate Nishati” ambayo ni zaidi ya kupanda miti inaelekeza kuweka uzito wa kutosha katika suala zima la kutunza miti yote inayopandwa na pia misitu ya asili tuliyonayo.

Alisema kitendo cha kupanda na kutunza misitu, kitahakikishia upatikanaji endelevu wa huduma zote za kiikolojia zinazotokana na misitu ikiwemo maji kwa matumizi ya nyumbani, viwanda, kilimo na uzalishaji wa nishati ya umeme.

Kwa hiyo, alisema kuna haja ya kuweka suala la ulinzi wa misitu kuwa ajenda ya kudumu katika shughuli zote za maendeleo katika mikoa, wilaya na vijiji na mkakati muhimu mmoja wapo ni kushirikisha jamii kama Sera ya Misitu inavyohimiza.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *